1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uvamizi wa Urusi nchini Ukraine waendelea

30 Mei 2022

Viongozi wa Umoja wa Ulaya wanakutana mjini Brussels ili kuonyesha mshikamano kwa Ukraine.

Brüssel | Sitzung Europaparlament zur Ukraine
Picha: John Thys/AFP/Getty Images

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy, ambaye jioni ya leo atahutubia kwa njia ya mtandao viongozi wa nchi 27 wa Umoja wa Ulaya, amekuwa mara kwa mara akidai Umoja wa Ulaya kuilenga sekta ya nishati na yenye faida kubwa ya Urusi ili kuizuia Moscow kujipatia malipo ya mabilioni ya dola kila siku kutokana na usambazaji wake wa nishati.

Lakini Hungary inaongoza kundi la nchi pamoja na Slovakia, Jamhuri ya Czech na Bulgaria, ambazo zinategemea mafuta ya Urusi na haziwezi kuchukua hatua kama hizo. Hungary hutegemea zaidi ya asilimia 60 ya mafuta yake kutoka Urusi na asilimia 85 ya gesi yake asilia. Waziri Mkuu wa Hungary, Viktor Orban amekuwa akisisitiza kuwa vikwazo vya mafuta havifai kujadiliwa katika mkutano huo.

Umoja wa Ulaya tayari umeiwekea Urusi vikwazo kwa awamu tano kutokana na

uvamizi wake nchini Ukraine. Vikwazo hivyo vinawalenga zaidi ya watu 1,000 akiwemo Rais wa Urusi Vladimir Putin na viongozi wakuu wa serikali, benki, sekta ya makaa ya mawe na  kadhalika.

Soma zaidi: UN: Vita vya Ukraine kusababisha mgogoro wa chakula duniani

Mkutano huo wa siku mbili huko Brussels utazingatia pia muendelezo wa misaada ya kifedha ya Umoja wa Ulaya kwa Ukraine, na huenda kukaidhinishwa msaada wa euro bilioni 9 ambao utatolewa kwa awamu ili kutoa msaada wa kijeshi pamoja na uchunguzi wa uhalifu wa kivita.

Usalama wa chakula nchini Ukraine

Picha: Fanny Facsar/DW

Suala la usalama wa chakula litakuwa mezani kesho Jumanne, ambapo viongozi wa Ulaya wametakiwa kuzihimiza serikali zao kuharakisha hatua za mshikamano ili kuisaidia Ukraine kuuza nafaka na mazao mengine nje ya nchi.

Wakati mashambulizi yakiendelea mashariki mwa Ukraine ambapo mji wa Sievierodonetsk unaelekea kuwa kama Mariupol baada ya huduma za misaada kusitishwa, Urusi inaonekana kudhamiria kulidhibiti eneo lote la viwanda la Ukraine la Donbas.

Igor Konashenkov, Msemaji wa Wizara ya Ulinzi ya Urusi amesema operesheni yao ya kijeshi inaendelea: "Vikosi vya wanajeshi wa Urusi vinaendelea na operesheni maalum ya kijeshi nchini Ukraine. Makombora ya angani yenye usahihi wa hali ya juu yalilenga eneo la udhibiti wa vikosi vya wanajeshi wa Ukraine, kituo kimoja cha mawasiliano, pamoja na maeneo 34 ya mkusanyiko wa wafanyakazi wa Ukraine na vifaa vya kijeshi.''

Soma zaidi:Amnesty: Urusi imefanya uhalifu wa kivita, Ukraine

Waziri mpya wa mambo ya nje wa Ufaransa, Catherine Colonna atasafiri leo kuelekea Kiev ili kuonyesha mshikamano wa Ufaransa kijeshi, kifedha na msaada wa kibinadamu kwa Ukraine inayokumbwa na vita kutokana na uvamizi wa Urusi. Colonna atakutana pia na waziri mwenzake wa Ukraine Dmytro Kuleba, ambaye watajadili vizuizi vinavyowekwa na Urusi kwa nafaka za Ukraine.

(APE, DPAE)

 

Ruka sehemu inayofuata Gundua zaidi
Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW