1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Viongozi wa Umoja wa ulaya wakutana kwa dharura Brussels

27 Mei 2014

Viongozi wa Umoja wa Ulaya wanakutana kwa dharura mjini Brussels kusaka jibu litakalotuliza hofu zilizojitokeza wakati wa uchaguzi wa bunge la Ulaya Jumapili iliyopita na kupelekea makundi ya siasa kali kupata nguvu

KItambulisho cha Umoja wa UlayaPicha: DW

"Wakati umewadia wa kurekebisha sera za Ulaya" ameshadidia waziri mkuu wa Italia Matteo Renzi. Akijivunia ushindi mkubwa wa mrengo wa kati kushoto nchini mwake wakati wa uchaguzi wa bunge la Ulaya,dhidi ya chama cha Beppe Grillo anaeuangalia kwa jicho la wasi wasi Umoja wa Ulaya,na kumvunja nguvu Silvio Berlusconi na chama chake cha mrengo wa kulia,Renzi anataka lipatikane jibu la haraka.Anataka kuitumia zamu yake kama mwenyekiti wa Umoja wa ulaya,kuanzia julai mosi ijayo,kuanzisha mikakati inayohitajika.

Waziri mkuu wa Italia atahitaji lakini uungaji mkono wa viongozi wenzake pamoja pia na ule wa kansela Angela Merkel wa Ujerumani ambao bado si dhahir.

"Kupata nguvu makundi yanayoupinga umoja wa ulaya ni jambo la kusikitisha-kilichobakia ni kuwazinduwa wapiga kura kupitia sera zitakazopalilia mashindano ya kiuchumi,zitakazochochea ukuaji wa kiuchumi na kubuni nafasi zaidi za kazi-hilo likiwa jibu bora zaidi kwa hasira za wapigakura." Amesema kansela Angela Merkel.

La muhimu anahisi waziri mkuu wa Italia ni kuwachagua viongozi wepya wa Umoja wa Ulaya ili kuweza kupanga ratiba ya mikakati itakayosaidia kubuni nafasi zaidi za kazi na kushughulikia wimbi la wakimbizi.

Malengo yanatofautiana na kiongozi huyo kijana wa Italia atajaribu kutafuta uungaji mkono wa rais Francois Hollande wa Ufarasa.Lakini kiongozi huyo wa kasri la Elysee anafika Brussels akiwa katika hali ya unyonge,akidhoofishwa kwa ushindi mkubwa wa chama cha siasa kali za mrengo wa kulia Front National FN.Chama hicho kinachoongozwa na wakili Marine Le Pen kinataka kulazimisha sera zake zifuatwe na hasa kuhusu suala la uhamiaji.

Mageuzi ya sera za umoja wa ulaya hayawezekani kabla ya kwanza kuteuliwa mwenyekiti wa halmashauri kuu ya umoja wa Ulaya.

Wakuu wa makundi ya kisiasa yanayowakilishwa katika bunge la Ulaya wamekutana hii leo mjini Brussels na kuwatolea wito viongozi wa Umoja wa Ulaya wamwachie mgombea wa wahafidhina waziri mkuu wa zamani wa Luxembourg,Jean-Claude Juncker atafute wingi wa viti 376 kuweza kuteuliwa mwenyekiti wa halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya.Chama chake cha wahafidhina wa Ulaya kimejikingia viti 213-kinahitaji angalao viti 60 kuweza kuteuliwa kushika nafasi itakayoachwa na Jose Manuel Barroso.

Waziri mkuu wa Zamani wa Luxemburg Jean-Claude Juncker anaepigania kuwa mwenyekiti wa halmashauri kuu ya Umoja wa UlayaPicha: Getty Images

Viongozi wa Umoja wa Ulaya watalizungumzia suala la nani ateuliwe kumrithi Barroso katika kikao chao leo usiku mjini Brussels.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/AFP

Mhariri: Josephat Charo