1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Viongozi wa Umoja wa Ulaya wamtaka Assad ang'oke madarakani

14 Desemba 2012

Viongozi wa taifa na serikali wa nchi 27 za umoja wa ulaya wamemaliza mkutano wa siku 2 kwa kukubaliana kuhusu mikakati ya kumaliza migogoro ya fedha katika kanda ya Euro,na kuhimiza umwagaji damu ukome Syria

Mwenyekiti wa baraza la Ulaya Van Rompuy akizungumza na waandishi habari mjini BrusselsPicha: Georges Gobet/AFP/Getty Images

Viongozi wa taifa na serikali wa Umoja wa Ulaya wanahisi mapambano yao dhidi ya migogoro ya fedha yamepata nguvu.Wameonyesha kuridhika kwao hii leo na makubaliano kadhaa yaliyofikiwa katika muda wa saa 48 za majadiliano kwa lengo la kuleta utulivu zaidi katika kanda ya Euro.

Umoja wa Ulaya bado haujazungumzia namna ya kugharimia kwa muda mkakati wa aina moja wa kulipia madeni ya benki za kanda ya Euro hadi michango itakayokusanywa na benki itakapotosha kudhamini kikamilifu shughuli za benki hizo.

"Bado kuna mengi ya kufanya na majadiliano kuendelezwa" amesema mwekiti wa baraza la Ulaya Herman Van Rompuy wakati wa mkutano pamoja na waandishi habari.

Kwa upande wake kansela Angela Merkel amesema:"Tumedhamiria hadi mwezi June mwakani tufafanue kwa upande mmoja kuhusu mikataba kati ya halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya na mataifa wanachama pamoja na kuimarisha mbinu za kushindana kibiashara na kwa upande wa pili tubuni njia ya namna ya kupatikana fedha."

Mwenyekiti wa halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya Jose Manuel BarrosoPicha: Reuters

Halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya inapanga kuwasilisha pendekezo lake kuhusu mkakati huo mapema mwakani.

Katika kikao cha jana viongozi wa taifa na serikali wa Umoja wa Ulaya walikubaliana mkakati huo ugharimiwe kutokana na michango ya sekta binafsi ya fedha na liundwe fuko maalum kwaajili hiyo.

Kansela Angela Merkel (mbele)akiondoka mkutanoni mjini BrusselsPicha: dapd

Baada ya kuzungumzia mbinu za kuimarisha utulivu katika zoni ya Euro viongozi wa Umoja wa Ulaya waliliingilia pia suala la Syria.Kama ilivyokuwa ikitarajiwa viongozi wa mataifa 27 ya taifa na serikali za umoja wa ulaya wametoa mwito wa kukomeshwa umwagaji damu na kung'oka madarakani rais wa Syria Bashar al Assad."Mustakbal wa Syria utawezekana tu ikiwa Assad hatokuwepo madarakani" amesema kansela Angela Merkel mwishoni mwa mazungumzo ya viongozi wa Umoja wa Ulaya mjini Brussels,huku rais Francois Hollande akitilia mkazo lengo linabidi kuwa "kumuona Assad aking'oka haraka madarakani".

Hata hivyo suala la kupunguza makali ya vikwazo vya silaha kwa Syria halijazungumzwa amesema kansela Merkel.

Mwandishi: Hamidou Oummilkheir/dpa/AFP/Reuters

Mhariri: Josephat Charo

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW