Viongozi wa upinzani Katumbi na Bemba kurejea nyumbani
31 Julai 2018Halikadhalika mbabe wa zamani wa kivita Jean-Pierre Bemba anatarajiwa kuwasili nchini humo kesho akiwa na dhamira ya kuwania pia kiti cha urais katika uchaguzi mkuu unaosubiriwa kwa hamu kubwa mwezi Desemba mwaka huu.
Katumbi amesema katika mahojiano kwa njia ya simu na shirika la habari la Ufaransa AFP kwamba yuko mjini Johannesburgh na ameiandikia mamlaka ya safari za anga kuomba ruhusa kwa ndege yake ya binafsi kutua siku ya Ijumaa mjini Lubumbashi , mji mkuu wa jimbo la Katanga.
Katumbi mwenye umri wa miaka 53, gavana wa zamani wa jimbo hilo lenye utajiri mkubwa wa madini, amekuwa akiishi uhamishoni nchini Ubelgiji tangu Mei 2016 baada ya kutofautiana na rais Joseph Kabila.
Ameapa kurejea kwa ajili ya uchaguzi ambao umecheleweshwa mno hapo Desemba 23 licha ya kuhukumiwa kifungo cha miaka mitatu jela katika kesi ambayo anadaiwa kufanya udanganyifu wa majumba.
Pia amefunguliwa mashitaka kwa kile kinachoonekana kuwa ni kukodisha mamluki na kuwa na hati ya kusafiria ya Italia, ambapo sheria ya Congo hairuhusu kuwa na uraia pacha, wa mataifa mawili.
Kabila ambaye ni mwanajeshi wa zamani , amekuwa madarakani tangu mwaka 2001, wakati alipochukua madaraka kutoka kwa baba yake aliyeuwawa. akiongoza serikali ambayo imekosolewa kwa kiasi kikubwa kwamba ametapakaa rushwa na isoyofanyakazi , alikuwa aondoke madarakani Desemba 2016 kwa mujibu wa katiba ya nchi hiyo mwishoni mwa muhula wake wa pili.
Bemba anarejea
Lakini aliendelea kubaki madarakani hadi pale mrithi wake atakapochaguliwa, hatua ambayo imechochea maandamano mitaani na kukandamizwa kwa nguvu pamoja na mamia ya watu kuuwawa.
Hasimu mwingine mkubwa wa Kabila ni mbabe wa zamani wa kivita na makamu wa rais Jean-Pierre Bemba, mwenye umri wa miaka 55, ambaye mwezi Juni alifutiwa mashitaka ya uhalifu wa kivita katika mahakama ya kimataifa ya uhalifu mjini The Hague.
Chama chake hapo mwanzo kilisema atawasili katika mji wa Gemena, mji ulioko katika ngome yake kuu upande wa kaskazini magharibi mwa nchi hiyo leo Jumanne. Lakini chama hicho kilisema jana kuwa hajapata ruhusa ya ndege yake kutua katika mji huo. maelfu ya watu walikuwa wakimsubiri mjini Gemena jana.
Bemba ameapa kurejea mjini Kinshasa kesho Jumatano Agosti mosi kutangaza nia yake ya kugombea katika uchaguzi. Jana gavana wa mji wa Kinshasa amesema atahakikisha usalama na kuamuru polisi 10 , kumlinda Bemba wakati atakaporejea, afisa wa chama cha Bemba cha MLC amesema.
Mwandishi: Sekione Kitojo /afp
Mhariri: Iddi Ssessanga