Viongozi wa vyama vya siasa Zimbabwe, wakutana, Afrika kusini.
15 Agosti 2008►Mazungumzo ya kugawana madaraka kati ya vyama vya siasa nchini Zimbabwe, yanaanza tena leo, Afrika kusini, wakati wa mkesha wa mkutano wa viongozi wa nchi za Jumuia ya Maendeleo kusini mwa Afrika SADC, ambao pia Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe na mpinzani wake Morgan Tsvangirai wamepanga kuhudhuria, mkutano huo, ambao Botswana imetangaza kuususia kutokana na ushiriki wa rais Mugabe.
◄
Naibu Katibu Mkuu wa chama cha Movement for Democratic Change MDC, Tapwa Mashakada amefahamisha kuwa mazungumzo yalianza toka asubuhi na kwamba yanaendelea.
Naye Kiongozi wa chama kilichojitenga na MDC, Arthur Mutambara ambaye pia yupo Afrika kusini kushiriki mazungumzo hayo, amethibitisha kuwepo kwa mazungumzo hayo kati ya chama cha Rais Mugabe ZANU PF na vyama hivyo viwili vya MDC, na kuongeza kuwa mazungumzo hayo hayajavunjika.
Mazungumzo ya siku tatu ya viongozi wa vyama hivyo yaliyokuwa yakifanyika Harare Zimbabwe, chini ya usuluhishi wa Rais Thambo Mbeki wa Afrika kusini, yalimalizika Jumanne kwa Tsvangirai kujitoa kwa kutoafikiana na Rais Mugabe kuhusu wadhfa gani kila mmoja angekuwa nao katika serikali ya muungano.
Bwana Tsvangirai aliwasili mapema leo mjini Johannesburg kwa ajili ya kuhudhuria mkutano wa siku mbili wa Jumuia ya Maendeleo ya kusini mwa Afrika SADC, ambao unaanza kesho.
Jana serikali ya Zimbabwe ilimnyang'anya kwa muda kiongozi huyo wa upinzani nyaraka zake za kusafiria, hali iliyosababishwa kushindwa kusafiri jana hiyo kuelekea Afrika kusini kama alivyopanga.
Kwa upande wa Rais Mugabe alitarajiwa kuwasili leo nchini humo kwa ajili ya kuendelea na mazungumzo hayo ya kutafuta suluhu.
Akizungumzia mazungumzo hayo ya kugawana madaraka msuluhishi wa SADC, katika mazungumzo hayo Rais Thabo Mbeki wa Afrika kusini alisema anamatumaini kwamba pande hizo mbili zinazopingana kisiasa zitafikia suluhu.
Katika hatua nyingine Rais Ian Khama wa Botswana atagomea mkutano wa viongozi wa Jumuia ya Maendeleo kusini mwa Afrika SADC, unaoanza kesho, kutokana na kwamba nchi yake haimtambui Rais Robert Mugabe, aliyechaguliwa kuiongoza Zimbabwe katika duru ya pili ya uchaguzi nchini humo.
Badala yake nchi hiyo itawakilishwa kwenye mkutano huo na na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa kimataifa.
Taarifa iliyotolewa nchini humo, imesema katika hali ya sasa ilivyo nchini Zimbabwe, haikupaswa kushiriki katika vikao vya siasa vya SADC, kwani kufanya hivyo ni sawa na kuhalalisha hali hiyo.
Awali Botswana ilitishia kugomea mkutano huo, iwapo Rais Mugabe, aliyechaguliwa tena katika duru ya pili ya uchaguzi wa Rais wa Zimbabwe, atahudhuria mkutano huo bila ya kufikia suluhisho la mzozo wa nchi yake.
Duru ya pili ya uchaguzi wa Zimbabwe ilifanyika June 27 na kulaniwa na jumuiya ya Kimataifa.