1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Viongozi kuendelea kuyaunga mkono makubaliano ya Minsk

20 Februari 2015

Viongozi wa Ukraine, Ujerumani, Ufaransa na Urusi wameahidi kuendelea kuyaunga mkono makubaliano tete ya kusitisha mapigano mashariki mwa Ukraine licha ya ukiukaji mkubwa wa makubaliano hayo

Picha: Reuters/G. Garanich

Huku viongozi hao wa pande nne wakilaani mapigano yanayoendelea mashariki mwa Ukraine na kuzitaka pande mbili zinazozana kuheshimu makubaliano ya kusitisha mapigano, Urusi na waasi wamepinga vikali ombi la Rais wa Ukraine Petro Poroshenko la kupelekwa kwa wanajeshi wa kimataifa wa kulinda amani mashariki mwa Ukraine.

Marekani imesema waasi hao wanaoungwa mkono na Urusi wameyavunja makubaliano ya kusitisha mapigano mara 250 tangu makubaliano hayo ya Minsk kuanza kutekelezwa siku ya Jumapili iliyopita.

Wanajeshi wamekamatwa na waasi

Wakati huo huo, jeshi la Ukraine limesema wanajeshi wake 90 wamekamatwa na waasi hao na wanajeshi wengine 82 hawajulikani waliko baada ya waasi kuwashinda nguvu wanajeshi na kuudhibiti mji wa Debaltseve. Waasi hao wamedai kuwakamata zaidi ya wanajeshi 300 wa serikali.

Rais wa Ukraine Petro Poroshenko akizungumza na wanajeshi waliotoka DebaltsevePicha: Reuters/Palinchak

Kushindwa kwa jeshi la Ukraine katika mji wa Debaltseve kumeibua maswali miongoni mwa raia wa Ukraine kuhusu uwezo wa jeshi hilo hadi kiasi cha Rais Poroshenko kuiomba jumuiya ya kimataifa kutuma wanajeshi wa kulinda amani mashariki mwa Ukraine.

Msemaji wa katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Stephanie Dujjaric amesema hawajapokea rasmi ombi la Ukraine.

Poroshenko aliliwasilisha tena ombi hilo katika mazungumzo ya simu kati yake na viongozi wa Ujerumani, Ufaransa na Urusi ambapo ombi hilo halikupata uungwaji mkono kutoka kwa viongozi hao.

Badala yake viongozi hao wametaka kutekelezwa kikamilifu wa makubaliano yaliyofikiwa mjini Minsk ikiwemo kusitisha mapigano, kuondolewa kwa silaha nzito, kuachiwa huru kwa wafungwa na kuruhusiwa kwa wachunguzi wa shirika la usalama na ushirikiano barani Ulaya OSCE kutekeleza majukumu yao.

Huku viongozi wa nchi za magharibi wakisema wanaunga mkono makubaliano ya kusitisha mapigano, kamati ya bunge la Uingereza imetoa ripoti inayozishutumu Uingereza na Umoja wa Ulaya kwa kuutathmini visivyo mzozo huo wa Ukraine ambao umedumu kwa miezi kumi na kusababisha vifo vya zaidi ya watu 5,600.

Uingereza yasema hatua zilizopo hazitoshi

Mwenyekiti wa kamati hiyo Christopher Tugendhat amesema Uingereza na Umoja wa Ulaya zimeshindwa kung'amua kuwa Urusi haiko katika njia kuelekea kuwa na demokrasia na kwa hivyo hakuna matumaini ya kufikiwa makubaliano thabiti ya kuutatua mzozo wa Ukraine.

Viongozi waliofikia makubaliano ya MinskPicha: Reuters/Grigory Dukor

Urusi imekuwa ikishutumikwa kwa kuwapa silaha na kutuma majeshi yake kuwasaidia waasi ikiwa na lengo la kuiyumbisha Ukraine ili isiweze kujiunga na Umoja wa Ulaya wala jumuiya ya kujihami ya NATO, madai ambayo Urusi imeyakanusha.

Marekani imekuwa ikitafakari kuipa Ukraine silaha kujihami dhidi ya waasi iwapo hali itazidi kuzorota. Waziri wa mambo ya nje wa Uingereza Philiph Hammond amesema nchi yake inasalia kulipinga pendekezo hilo lakini akaongeza ni suala linaloweza kufikiwa na nchi binafsi.

Kulingana na wanahabari walioko mashariki mwa Ukraine, mapigano makali yaliendelea jana nzima katika jimbo la Donetsk huku msafara wa magari ya umoja wa Mataifa ukiwasili na misaada ya kibindamu.

Mwandishi: Caro Robi/Afp/Ap

Mhariri:Josephat Charo

Ruka sehemu inayofuata Gundua zaidi
Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW