1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Viongozi wahutubia Mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa

20 Septemba 2023

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres amesema watu wanatarajia kuwa viongozi watachukua hatua za kuondokana na kile alichokiita "vurugu" zilizopo duniani.

USA | UN Generalversammlung New York
Picha: Bianca Otero/ZUMA Wire/IMAGO

 

Mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa umeanza rasmi siku ya Jumanne kwenye Makao Makuu ya umoja huo mjini New York, Marekani. 

Viongozi wa ulimwengu unaokabiliwa na changamoto za vita, mabadiliko ya tabia nchi na kuendelea kukosekana kwa usawa kati ya mataifa tajiri na masikini, walizokusanyika siku ya Jumanne na kusikiliza kwa makini hotuba ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa akiwatolea wito wa kuchukua hatua za pamoja kwa maslahi ya walimwengu.

Aidha Guterres amesema Umoja wa Mataifa ndio chombo kinachowezesha usharikiano baina ya nchi duniani, na lazima mfumo wake ubadilike ili kuendana na zama hizi. Aidha Guterres amezitaja changamoto zingine zinazoikabili dunia kama kupanda kwa gharama ya maisha, umasikini na ongezeko la njaa huku akitoa onyo kuhusu hatari zinazoikabili dunia ambayo amesema "imevurugwa":

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres akihutubia mkutano huo: 19.09.2023Picha: Caitlin Ochs/REUTERS

" Dunia yetu inazidi kuyumba, mivutano ya kisiasa na changamoto za kimataifa vinaongezeka. Tunaonekana hatuna uwezo wa kuja pamoja kutoa majibu kwa yote haya. Tunakabiliwa pia na changamoto ya mabadiliko ya hali ya hewa na hitilafu za teknolijia, yote haya yanajiri tukiwa katika wakati wa mpito. Sasa hivi tunaelekea katika mfumo jumuishi Ulimwenguni, ni jambo zuri na litatoa fursa kwa haki na usawa katika mahusiano ya kimataifa."

Hotuba ya Rais Joe Biden wa Marekani

Kwa mara ya kwanza baada ya miaka mingi, Rais wa Marekani amezungumza mara baada ya hotuba ya Guterres. Joe Biden amekuwa kiongozi pekee kutoka mataifa matano yenye nguvu na yenye kura ya turufu kwenye Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhudhuria mjini New York katika  mkutano huo wa wanachama 193.

Soma pia: Mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kufungua pazia leo

Biden amezungumzia kuhusu mzozo wa Ukraine na kutoa wito kwa mataifa kushirikiana na Kyiv kukabiliana na uvamizi wa Urusi. Biden amesema pia kuwa Marekani iko tayari kuzisaidia nchi zinazoendelea ili kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia nchi.

Rais wa Marekani Joe Biden, akizungumza katika Mkutano huo: 19.09.2023Picha: Mike Segar/REUTERS

Rais wa China Xi Jinping, Vladimir Putin wa Urusi, Emmanuel Macron wa Ufaransa na Rishi Sunak wa Uingereza wote hawatohudhuria mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mwaka huu.

Baadae leo,  Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy  atatoa hutoba kwenye jukwaa hilo kwa mara ya kwanza. Viongozi wengine kama rais Inácio Lula da Silva wa Brazil, rais Miguel Diaz-Canel wa Cuba, Rais Recep Tayyip Erdogan wa Uturuki, Ebrahim Raisi wa Iran na Waziri Mkuu wa Japan, Fumio Kishida ni miongoni mwa wale walio kwenye orodha ya kusimama jukwaani hii leo.

Viongozi wa nchi zinazoendelea wanatarajia kuzishinikiza nchi zilizoendelea kutimiza ahadi zao za ufadhili katika miradi mbalimbali ikiwa ni pamoja na mabadiliko ya tabia nchi na maendeleo endelevu. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, alitoa wito wa kuwepo "mpango mbadala" wa kufikia malengo hayo, na kukiri kwamba ni asilimia 15 pekee ya malengo hayo ndiyo yanayoweza kufikiwa kikamilifu ifikapo 2030.