Viongozi wakigeni wampongeza Merkel
28 Septemba 2009
Salamu za pongezi zimeanza kumiminika mjini Berlin, baada ya Bibi Angela Merkel kuchaguliwa tena kuwa Kansela kwa kipindi cha pili cha miaka minne.
Rais Barack Obama wa Marekani alimpigia simu Bibi Markel na taarifa ya Ikulu ya Marekani ikasema viongozi hao wawili waliafikiana kwamba kwa kuwepo serikali imara ya Ujerumani, ushirikiano wa nchi zao mbili utaimarika zaidi.
Akimpongeza Bibi Merkel, Rais Nikolas Sarkozy wa Ufaransa alimtakia kila la kheri katika jukumu lake muhimu ambalo wajerumani wamemtwika kwa kipindi cha pili. Kiongozi huyo wa Ufaransa akasema anatarajia kushirikiana na Bibi Merkel katika masuala ya kimataifa na ya kikanda, kama mabadiliko ya hali ya hewa na msukosuko wa kiuchumi.
Na akimpongeza Bibi Merkel kwa ushindi wake huo katika uchaguzi wa Jumapili, Waziri mkuu wa Uingereza Gordon Brown alisema anamatumaini ya kuendeleza ushirikiano mzuri wa kikazi na wa karibu na Kansela.
Ushindi wa Kansela Merkel na chama chake cha CDU/CSU umempa nafasi ya kuunda serikali ya mseto na chama cha FDP kinachoongozwa na Guido Westerwelle na kumaliza muungano wa miaka minne na chama cha SPD ambacho sasa kitakua upande wa upinzani.
Mwandishi:M.Abdul-Rahman
Mhariri:Sekione Kitojo