1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Viongozi wakosa kufikia muafaka kuhusu hatma ya Maassen

Caro Robi
14 Septemba 2018

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel na viongozi wa vyama vingine viwili vinavyounda serikali ya mseto walifanya mazungumzo ya dharura kujadili hatma ya mkuu wa shirika la ujasusi Hans-Georg Maassen.

Hans-Georg Maaßen
Picha: picture-alliance/dpa/O. Dietze

Maassen anashinikizwa ajiuzulu tangu alipotoa kauli kuwa serikali ilikuwa inasambaza taarifa zisizo za kweli kuhusu ghasia zinazodaiwa kufanywa na wafuasi wa makundi ya mrengo wa kulia dhidi ya wageni mashariki mwa Ujerumani. 

SPD imesema msimamo wao ni wazi kuwa wanamtaka Merkel kumfuta kazi Maassen. Lakini Waziri wa Mambo ya Ndani Horst Seehorfer anayeongoza chama cha Christian Social Union - CSU, amesema ana imani na utendaji wa Maassen na hivyo haoni sababu ya kumfuta kazi.

SPD yamtaka Maassen ajiuzulu

Baada ya mazungumzo yaliyodumu dakika 90 kati ya Merkel, kiongozi wa SPD Andrea Nahles na Seehofer hakuna muafaka uliofikiwa. Viongozi hao watakutana tena na uamuzi unatarajiwa Jumanne wiki ijayo.

Mkuu wa shirika la Ujasusi Hans-Georg Maassen na waziri wa mambo ya ndani Horst SeehoferPicha: Getty Images/AFP/T. Schwarz

Hayo yanakuja huku ikidaiwa kuwa mkuu huyo wa shirika la Ujasusi alitoa taarifa nyeti za kijasusi kwa chama chenye msimamo mkali wa mrengo wa kulia Alternative für Deutschland AfD.

Shirika la ujasusi limekanusha ripoti hiyo iliyotolewa na kituo cha televisheni cha ARD kuwa Maassen aliwaeleza wabunge wa AfD sehemu ya ripoti yake ya kila mwaka kuhusu masuala ya kijasusi kabla kuchapishwa rasmi.

Suala hilo kuhusu hatma ya siku za usoni ya Maassen linachochea zaidi mjadala mkali unaojiri hapa Ujerumani kuhusu wahamiaji, jambo linaloitikisa serikali ya Kansela Merkel ambayo nusura isambaratike mwaka huu kutokana na mzozo kati yake na Seehofer, aliyechukua msimamo mkali dhidi ya wahamiaji.

Waziri wa fedha Olaf Scholz ambaye ni mwanachama wa SPD amesema Maassen amepoteza uaminifu na hivyo lazima awajibike. Mkuu huyo wa shirika la ujasusi siku ya Jumatano alifika mbele ya kamati ya bunge kuhusu masuala ya ndani kujieleza.

Seehofer amesema maelezo ya Maassen bungeni yalikuwa ya kuridhisha na alikanusha vikali madai kuwa anaegemea upande wa mrengo wa kulia.

Uhamiaji suala tete Ujerumani

Magazeti mawili yameripoti kuwa Maassen alimuandikia Seehofer mapema wiki hii kusema kuwa video zinazoonesha wafuasi wa siasa kali za mrengo wa kulia wakiwashambulia watu wanaodhaniwa kuwa wageni Chemnitz hazikuwa za uongo na kuwa kauli yake ilitafsiriwa visivyo.

Waandamanaji mjini Chemnitz Picha: picture-alliance/AP Photo/J. Meyer

Waziri wa mambo ya nje Heiko Maas ambaye ni mwanachama wa SPD amesema maandamano ya kuwapinga wahamiaji yanaitia doa hadhi na sifa ya Ujerumani nje ya nchi lakini akaongeza kuwa watu pia wanatambua kuwa raia wengi wema nchini Ujerumani wana uhuru wa kujieleza.

Maas amesema misimamo mikali ya mrengo wa kulia inatikisa misingi ya demokrasia yao na kutishia mshikamano wa kijamii na hivyo ni sharti kuepusha mgawanyiko wa jamii.

Huku hayo yakijiri, mwanamume mmoja wa umri wa miaka 33 aliyeshiriki katika maandamano ya wanaopinga wahamiaji mjini Chemnitz hapo jana alikutwa na hatia ya kupiga saluti ya kinazi na kujaribu kumpiga polisi alipokuwa akikamatwa. Mahakama imemhukumu mtu huyo miezi minane ya kifungo cha nje na kumtoza faini ya euro 2,000.

Wiki hii, Merkel amesema anachukulia kwa uzingatifu mkubwa wasiwasi wa Wajerumani kuhusu uhalifu unaofanywa na baadhi ya wahamiaji lakini amesisitiza hakuna kisingizio cha kuonesha chuki, ghasia wala kuunga mkono vitendo vya kinazi.

Mwandishi: Caro Robi/Reuters/Dpa/Afp

Mhariri: Iddi Ssessanga

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW