Viongozi wakuu wa EU wakutana kuelekea Brexit
23 Februari 2018Mkutano huo wa kilele usio rasmi wa Ijumaa (23 Februari) uliwaleta pamoja wakuu 27 wa serikali za mataifa wanachama wa Umoja wa Ulaya, ambao ndio watakaobakia baada ya Uingereza kujiondoa rasmi mnamo Machi mwakani, ukitajwa kuwa mwazo wa mijadala mirefu na ya kina kuelekea muda huo.
Viongozi hawa wakuu sio tu walitakiwa kuamua juu ya njia za kuziba pengo la dola bilioni 14 litakaloachwa na Uingereza itakapojiondoa, bali pia kukubaliana juu ya vipaumbele vya matumizi kuanzia mwaka 2020, ambapo masuala ya uhamiaji, ugaidi na ulinzi wa mipaka yakiwa yanaonekana kama changamoto mpya kwa Umoja wa Ulaya.
Suala jengine muhimu lililowakutanisha pamoja wakuu wa Umoja wa huo, ni namna ya kumchaguwa mrithi wa mkuu wa sasa Kamisheni ya Ulaya, Jean-Claude Juncker.
Uingereza yataka makubaliano bora zaidi
Licha ya kwamba Waziri Mkuu wa Uingereza, Theresa May, hakuwa sehemu ya kikao hiki cha Brussels, waziri wake wa masuala ya afya, Jeremy Hunt, alisema Uingereza iko tayari kuziowanisha kanuni zake za ndani na zile za Umoja wa Ulaya kwenye baadhi ya maeneo, kama vile sekta ya vyombo vya usafiri, hata baada ya kuondoka kwenye Umoja huo hapo Machi mwakani.
Hili likifanyika, linatazamiwa kupunguza uzito wa gharama za kibajeti kwenye Umoja wa Ulaya.
Kabla ya hapo, waziri wa masuala ya utawala nchini Uingereza, David Lidington, alisema uwezekano wa kufikia makubaliano yanayozipendeza pande zote mbili upo.
"Ikiwa unaangalia yaliyotokea huku nyuma, kabla ya mkutano wa kilele wa Umoja wa Ulaya wa Disemba, kulikuwa na mashaka mengi kwamba yumkini baraza la mawaziri la Uingereza, halitaweza kufikia makubaliano. Sote tulikubaliana juu ya msimamo ambao Waziri Mkuu angelikwenda nao Brussels na tukafanikiwa sana. Sote kwenye baraza la mawaziri tuna dhamira ya kuona kuwa Uingereza inafikia makubaliano yaliyo bora zaidi kwa kila sehemu ya nchi hii," alisema Lidington.
Hata hivyo, mkutano huu wa viongozi wakuu wa Umoja wa Ulaya haukutazamiwa kuchukuwa uamuzi wowote rasmi, ingawa ungeliweka msingi wa kile kinachotajwa kuwa kitakuwa majadiliano makali, hasa juu ya pengo la kibajeti liachwalo na Uingereza.
Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa anasukuma mbele ajenda yake ya kile anachokiita mpango mkuu, ambao unahusisha kuupa nguvu mpya Umoja wa Ulaya, baada ya Uingereza kuondoka.
Mwandishi: Mohammed Khelef/dpa/AFP
Mhariri: Saumu Yussuf