1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Viongozi walaani kukamatwa mwanaharakati wa Belarus

24 Mei 2021

Belarus iliilazimu ndege ya abiria iliyokuwa imembeba mwanaharakati wa upinzani kuubadili mkondo na kutua katika mji mkuu Minsk na kuzusha hasira kutoka kwa viongozi wa ulimwengu waliokiita kitendo cha ugaidi wa serikali

Polen Danzig 2020 | Roman Protasevich, Blogger
Picha: Michal Fludra/NurPhoto/picture alliance

Mwandishi wa habari mkosoaji Raman Protasevich alikamatwa jana baada ya ndege aliyokuwemo ya Ryanair kuondolewa kwenye njia yake ya Athens kuelekea Vilnius – ikiandamana na ndege ya kivita ya Belarus – na kugeuzwa hadi mji mkuu Minsk baada ya kupewa taarifa za kitisho cha usalama.

Abiria walielezea kumuona Protasevich aliye na umri wa miaka 26, ambaye amekuwa akiishi Poland, akionekana mwenye hofu wakati ndege ilipogeuzwa kuelekea Minsk. 

Soma pia: UN kuchunguza ukiukaji wa haki za binadamu Belarus

Uwanja wa ndege wa Minsk ulisema ndege hiyo ilipekuliwa na hakuna bomu lililopatikana na abiria wote wakapelekwa kwa uchunguzi mwingine wa usalama.

Ndege ya Ryanair ilikuwa na watu 123Picha: Getty Images/AFP

Idara ya habari ya rais Lukashenko ilisema rais alitoa amri ya kuigeuza safari ya ndege hiyo na kuamuru ndege ya kivita aina ya MiG-29 kuandamana nayo. Hatua hiyo imekuja wakati mamlaka za Belarus zikizidisha ukandamizaji dhidi ya upinzani kufuatia maandamano ya kihistoria yaliyoikumba nchi hiyo baada ya uchaguzi wa rais mwaka jana ambao ulipingwa

Tukio hilo linakuja wakati Umoja wa Ulaya ukitarajiwa kujadili kuimarisha vikwazo vyake ilivyoiwekea Belarus, kuhusiana na ukandamizaji unaofanywa na Rais Alexander Lukashenko dhidi ya waandamanaji wa upinzani, katika mkutano wa kilele leo uliopangwa kabla.

Mkuu wa Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen amesema tabia hiyo mbaya na inayokwenda kinyume cha sheria ya utawala wa Belarus itakuwa na madhara. Ametaka Protasevich aachiwe huru akiongeza kuwa waliohusika lazima wawekewe vikwazo.

Wafuasi wa Protasevich wanahofia usalama wakePicha: Andrius Sytas/REUTERS

Waziri Mkuu wa Poland Mateusz Morawiecki alilaani hatua hiyo ya Belarus akisema ni kitendo cha ugaidi wa serikali wakati waziri wa mambo ya kigeni wa Ufarans Jean-Yves Les Drian akitoa wito wa kuwepo na hatua Kali kutoka Umoja wa Ulaya. Lithuania na Latvia zimetoa wito wa ndege za kampuni za kimataifa kutotumia anga za Belarus. Shirika la Kimataifa la Safari za Anga – ambalo ni taasisi ya Umoja wa Mataifa – limesema hatua hiyo ya kulazimishwa kutua kwa ghafla huenda inakiuka Mkataba wa Chicago, ambao unalinda uhuru wa anga za kila taifa.

Soma pia: Walioteswa Belarus wamshtaki Lukashenko Ujerumani

Marekani imelaani vikali kukamatwa kwa mwanahabari huyo huku waziri wa mambo ya kigeni Antony Blinken akitaka aachiwe huru. Amesema hatua hiyo ilihatarisha Maisha ya abiria 120 waliokuwemo kwenye ndege hiyo wakiwemo Wamarekani.

Waziri Mkuu wa Ugiriki Kyriakos Mitsostakis alisema kulazimishwa kutua ndege ya abiria na kumkamata mwandishi wa habari ni kitendo kisicho cha kawaida na cha kutisha. Rais wa Lithuania Gitanas Nauseda amesema hatua hiyo ya Belarus ni ya kuchukiza na waendesha mashitaka wamesema wameanzisha uchunguzi wa uhalifu kwa utekaji nyara wa ndege.

AFP/AP/Reuters

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW