Viongozi walishutumu shambulizi la Barcelona
18 Agosti 2017Shambulizi la Barcelona limeuhuzunisha ulimwengu kwa ujumla. Viongozi mbalimbali na watu wa tabaka mbalimbali wametuma risala zao za rambirambi huku wakilaani shambulio hilo. Miongoni mwa waliotuma jumbe zao ni pamoja na wakuu wa nchi, waimbaji, waigizaji na wachezaji maarufu.
Wanasiasa nchini Ujerumani wamekubaliana kusitisha kampeni zao leo kufuatia shambulizi hilo la jana mjini Barcelona Uhispania. Mshindani mkuu wa Kansela Angela Merkel Martin Schulz amewaambia waandishi wa habari mjini Berlin kuwa amezungumza na bibi Merkel na wakakubaliana kusitisha kampeni kwa muda kama ishara ya kuonesha umoja na waathirika wa shambulizi hilo. Schulz ameongeza kuwa wote wanakubaliana kuwa ugaidi hauna nafasi na Ulaya itaendelea kuwa ya jamii huru.
Raia 26 wa Ufaransa wajeruhiwa
Watu 26 miongoni mwa 100 waliojeruhiwa wakiwa raia wa Ufaransa, 11 wakiwa wamejeruhiwa mno, waziri wa mambo ya ndani wa Ufaransa Jean-Yves Le Drian amesema ataelekea Barcelona leo kutembelea waathirika. Hapo awali, rais wa Ufaransa Emmanuel Macron alisema kuwa hata baada ya shambulizi hilo, Ufaransa na Uhispania zinasalia kuwa pamoja.
Rais wa Marekani Donald Trump kupitia ukurasa wake wa Twitter amelaani shambulio hilo la Barcelona, huku akinukuu kauli ya generali wa zamani wa Marekani aliyekabiliana na waasi wa Kiislamu nchini Ufilipino karne iliyopita kuwa wauaji wanapaswa kupigwa risasi iliyotumbukizwa kwenye damu ya nguruwe.
Nchi kuimarisha ushirikiano
Waziri Mkuu wa Pakistan Shahid Khan Abbasi ambaye ametuma risala zake za rambirambi kwa Wahispania, pia amelaani shambulio hilo la kutumia gari kuwagonga na kuua watu. Abbasi ameongeza kuwa visa kama hivyo vya kigaidi haviwezi vikawatisha raia jasiri wa Uhispania na kwamba kadri magaidi wanavyokosa kuelewa nia za jamii ambazo wanajaribu kuhujumu, ndivyo watakavyozidi kushindwa.
Naye Waziri Mkuu wa Australia Malcolm Turnbull amesema: "Tunasiamama pamoja na watu wa Uhispania katika vita dhidi ya ugaidi wa itikadi kali za Kiislamu. Uhispania ni mshirika wetu dhidi ya kundi la DAESH mashariki ya kati na hivyo maafisa wetu wa ujasusi wanashirikiana na wenzao jinsi tufanyavyo kila mara na nchi nyinginezo. Hivi ni vita vya ulimwengu dhidi ya ugaidi."
Naye Waziri Mkuu wa Sweden, Stefan Lofven amesema amesikitishwa mno na shambulizi hilo la Barcelona, mwenzake kutoka Norway Erna Solberg akilitaja shambulizi hilo kuwa la watu waoga, huku Waziri Mkuu wa Estonia Juri Ratas akilitaja kuwa shambulizi la kikatili.
Ronaldo na Messi watuma rambirambi
Katika mitandao ya kijamii, ujumbe kuhusu mauaji hayo ya Barcelona umetawala.
Wanamuziki, waigizaji na wachezaji maarufu wa kandanda pia wamewasilisha rambirambi zao. Lionel Messi wa Barcelona amesema kila timu itatoa heshima kwa dakika moja uwanjani kabla kuanza mechi wikendi hii. Christiano Ronaldo wa Real Madrid amesema ameshangazwa na mkasa huo na yuko pamoja na wote walioathiriwa. Julio Iglesias wa Barcelona amesema mji wa Barcelona umekumbwa na huzuni huku Jennifer Lopez akituma ujumbe wa mapenzi na amani kwa wakaazi wa Barcelona.
Miongoni mwa waliouawa na waliojeruhiwa ni raia kutoka nchi 34 zikiwa ni pamoja na Italia, Venezuela, Australia, Ireland, Algeria, China na Ubelgiji. Jumla ya watu 13 wameuawa na wengine 100 kujeruhiwa.
Mwandishi: John Juma/APE/AFPE
Mhariri: Iddi Ssessanga