1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaIsrael

Viongozi watoa wito wa njia salama kwa wanaohama Gaza

13 Oktoba 2023

Waziri wa Ulinzi wa Marekani Lloyd Austin amewasili leo Ijumaa katika mji wa Tel Aviv nchini Israel kukutana na maafisa wakuu wa serikali.

Palästinenser Flucht Gaza
Wapalestina wakimbia GazaPicha: Mohammed Salem/REUTERS

Austin anatarajiwa kukutana na Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu, Waziri wa Ulinzi Yoav Gallant na Baraza la Mawaziri la Vita vya Israel.

Kwa mujibu wa maafisa wa ulinzi wa Marekani walioandamana na Austin ziara hiyo inalenga kusisitiza uungaji mkono usioyumba wa Marekani kwa Israel na dhamira yake ya kuhakikisha nchi hiyo ina kila inachohitaji kujilinda.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani Annalena Baerbock na Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen pia wanatarajiwa kuwasili Israel hii leo.

Lula asisitiza njia salama 

Kwa upande wake Rais wa Brazil Luiz Inacio Lula da Silva, ambaye anashikilia urais wa zamu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, ameitaka Israel kuweka njia itakayozingatia maslahi ya kibinadamu kwa ajili ya wakazi wa Gaza kuhama kuelekea Misri.

Kupitia mtandao wa kijamii ya X Rais Lula amesema amezungumza kwa simu na rais wa Israel Isaac Herzog na kutoa wito wa kuzingatia hali ya kibinadamu ili watu wanaotaka kuondoka Ukanda wa Gaza kupitia Misri wawe salama.

Mbali na Lula, viongozi mbali mbali wa Ulaya na Shirika la Afya Ulimwenguni wametoa wito wa kuundwa njia ambayo watu wanaweza kutumia kuondoka eneo la Palestina na kuruhusu misaada ya kibinadamu kuingia.

Brazil pia imeitisha mkutano wa Baraza la Usalama siku ya Ijumaa kujadili mzozo unaoendelea.

Athari ya wito wa Israel kwa raia

Data ya wakimbizi waliosajiliwa wa Palestina

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuwahudumia wakimbizi wa Kipalestina (UNRWA) limesema limehamishia makao yake makuu kusini mwa Ukanda wa Gaza kufuatia wito wa Israel wa kuwahamisha.

Shirika hilo linawapa hifadhi zaidi ya asilimia 60 ya watu 423,000 waliokimbia makazi yao katika siku za hivi karibuni katika Ukanda wa Gaza.

Huku haya yakijiri Umoja wa Mataifa umetoa ombi la dharura la dola milioni 294 kushughulikia "mahitaji ya dharura" ya watu huko Gaza na Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu huku mapigano kati ya Israel na kundi la wanamgambo wa Hamas yakiendelea.

Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu (OCHA) imesema fedha hizo zitatumika kusaidia zaidi ya watu milioni 1.2.

Aidha OCHA imeeleza kwamba vituo vya matibabu pia vimejaa ikiwa ni pamoja na wanawake wajawazito 50,000 ambao sasa wanakabiliwa na matatizo ya kupata huduma muhimu za afya.

 

https://p.dw.com/p/4XTdy

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW