1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Virusi vya Corona: China yakabiliwa na changamoto asema Xi

Zainab Aziz Mhariri Yusra Buwayhid
26 Januari 2020

Rais wa China Xi Jinping amesema nchi yake inakabiliwa na "hali mbaya," wakati ambapo virusi vya corona vinaendelea kuenea huku watu wapatao 1,975 wakiliripotiwa kuwa wameambukizwa.

China Peking Arbeiter messen Temperatur der Reisenden vor dem Bahnhof
Picha: Reuters/T. Peter

China mnamo siku ya Jumapili ilizidisha vizuizi vya usafiri ili iweze kupambana na virusi vya corona ambavyo Rais Xi Jinping amesema ni tishio kubwa. Kwa mujibu wa shirika la habari la taifa, serikali ya China imesimamisha shughuli  za kuwatembeza watalii kutoka mataifa ya nje, pia hakutakuwepo na safari za mabasi yanayotoka na kwenda mikoani kuanzia Jumapili katika juhudi za kupunguza kuenea kwa ugonjwa unaosabbabishwa na virusi vya corona.

Mlipuko huo unaaminika kuwa ulianzia katika eneo la mashariki mwa China katika mji wa Wuhan na umesambaa hadi katika nchi zingine kadhaa kama Marekani, Ufaransa, Japan na Australia.

Watu wapatao 1,975 wanaaminika kuwa wameambukizwa, na takriban vifo 56 vimeripotiwa. Taarifa ya serikali  imesema watu 324 wamo katika hali mbaya. Wakati huo huo serikali ya China imechukua hatua ya kuweka marufuku ya kuingia au kutoka kwenye mkoa wa Hubei ulio katikati mwa nchi hiyo ambao pia umeathiriwa vibaya, hii ikiwa ni katika juhudi za kudhibiti maambukizi zaidi.

Rais wa China Xi JinpingPicha: AFP/A. Messinis

Kiongozi wa Hong Kong, Carrie Lam, ametangaza hali ya dharura kuhusu virusi vya corona katika jiji hilona serikali yake imetangaza kufungwa shughuli za usafiri, shule na vyuo vikuu. Visa vitano vya maambukizi ya virusi vya corona vimeripotiwa katika jiji la  Hong Kong na watu zaidi ya 122 wanadhaniwa kuwa na virusi hivyo.

Shughuli mbali mbali zimefungwa wakati ambapo raia wengi wa Hong Kong wanasherehekea mwaka mpya huku kukiwa na mivutano inayoendelea baada ya miezi saba ya maandamano dhidi ya serikali. Ndege na safari za reli ya mwendo wa kasi kati ya Hong Kong na Wuhan zimesimamishwa, wakati ambapo shule na vyuo vikuu vitaendelea kufungwa hadi Februari 17.

Katika mji wa Wuhan, ambako karibu visa 2000 vya mambukizi na vifo vimeripotiwa, matumizi ya gari yamepigwa marufuku na usafiri wa kuingia na kutokanje umezuiwa.

Serikali ya China mnamo Jumamosi ilitangaza kwamba mji wa Wuhan utajengewa hospitali yenye takriban vitanda 1,000 ili kukabiliana na janga hilo, ambayo ujenzi wake utakamilika Februari 3. Ujenzi huo ni sawa na ujenzi wa hospitali iliyojengwa kwa ajili ya kupambana na ugonjwa wa SARS iliyojengwa ndani ya siku sita mjini Beijing mnamo 2003 wakati mlipuko wa ugonjwa huo ulipozuka.

Vyanzo: AP/AFP

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW