Visa vya maambukizi ya virusi vya corona vyapungua China
12 Februari 2020
China imesema idadi ya visa vipya vya maambukizi ya homa ya virusi vya corona vilivyosajiliwa leo Jumatano ni ya chini zaidi tangu mwezi Januari. Hali hiyo inaupa uzito utabiri wa maafisa wakuu wa afya nchini humo, kwamba mripuko wa ugonjwa huo waweza kuwa umemalizika ifikapo mwezi Aprili. Wataalamu wa kimataifa hata hivyo, wameonya kwamba bado ni mapema kuwa na matumaini ya namna hiyo.
Taarifa iliyotolewa na mshauri mkuu wa masuala ya afya nchini China Zhong Nanshan, imeeleza kuwa ripoti zinaonyesha kupungua kwa maambukizi mapya ya virusi vya corona katika mikoa mbali mbali ya nchi hiyo, na kwamba dalili zinaashiria kuwa baada ya mwezi huu wa Februari kasi ya maambukizi ya ugonjwa huo itapungua.
Matumaini yenye tahadhari
Masoko ya fedha na mitaji ulimwenguni yamepokea vyema taarifa hiyo, licha ya tahadhari kutoka kwa wataalamu wa kimataifa waliotishwa na namna homa hiyo ilivyoenea kwa kasi na kuuwa watu zaidi ya 1,100, wote, isipokuwa wawili tu, wakiwa wakaazi wa China Bara.
Zhong ambaye utabiri wake wa siku zilizopita haukuwa sahihi, ameliambia shirika la habari la Reuters kuwa anaamini ifikapo mwezi Aprili mwaka huu, mripuko wa homa hii hatari utakuwa umemalizika, ingawa kuanza tena kwa shughuli za usafiri kunawapa wasiwasi baadhi ya watu.
''Kwa wakati huu, watu wengi wanaanza safari kurejea sehemu zao za kazi, na hili linasababisha wasiwasi juu ya uwezekano wa kuzidisha kitisho cha maambukizi mapya. Lakini kwa kuzingatia hali ya sasa, siamini kwamba hofu yao ina msingi.'' Amesema Zhong.
Mashaka mitandaoni
Tangazo la matumaini la viongozi halijazuia mashaka miongoni mwa watumiaji wa mitandao ya kijamii nchini China juu ya uaminifu wa takwimu zinazotolewa, baada ya hatua ya serikali kubadili maelekezo katika mfumo wa kukusanya data za maambukizi ya homa ya virusi vya corona.
Wakati huo huo, idadi ya wasafiri walioambukizwa virusi vya corona katika meli ya anasa ya Diamond Princess imepanda na kufika watu 175, kufuatia kugunduliwa kwa visa vipya 39. Meli hiyo iliwekwa chini ya karantini nje ya bandari ya Yokohama, Japan tarehe 3 Februari. Afisa mmoja wa kufuatilia karantini hiyo ni miongoni mwa wagonjwa wapya.
rtre, ape