Visiwa vya Maldives kufanya uchaguzi mkuu
15 Novemba 2013Mahakama kuu ya nchi hiyo imeahirisha zoezi la uchaguzi huo mara tatu sasa na kuufanya Umoja wa Ulaya kutoa onyo ikiwa uchaguzi huo hautafanyika.
Huku raia wakiwa kwenye maandalizi ya kumpata rais mpya wa nchi hiyo, rais wa sasa, Mohamed Waheed, ameondoka nchini humo kwenda mjini Hong Kong, nchini Singapore kwa kile kilichoolezwa kuwa amemsindikiza mke wake kwenda kupata matibabu.
Msemaji wa rais huyo, Masood Imad, ameliambia shirika la habari la AFP kuwa rais huyo amelazimika kusafiri kwa ajili ya matibabu ya macho ya mke wake, ambapo wasingeweza kuahirisha na atarejea nchini humo baada ya mwezi mmoja.
Tamko lililotolewa na Mkuu wa sera za nje wa Umoja wa Ulaya, Catherine Ashton, ikiwa kutatokea sababu zozote za kutaka kuahirishwa au kucheleweshwa kwa uchaguzi huo, Umoja huo utachukulia kuwa ni suala linalofanywa kwa makusudi ili kuwanyima wapiga kura haki yao ya kidemokrasia.
Hatua ya Umoja wa Ulaya imefuatia hatua ya rais wa sasa wa nchi hiyo, Mohamed Waheed Hassan, ya kuamua kusogeza siku sita zaidi za kuendelea kukaa madarakani kwa madai ni haki yake ya kimsingi kikatiba, baada ya nchi hiyo kushindwa kufanya uchaguzi mara tatu sasa.
Umoja wa Ulaya watoa onyo ikiwa utaahirishwa
Bila kutaja hatu gani itachukua, taarifa hiyo ya Umoja wa Ulaya imesema Umoja huo utachukua hatua madhubuti, ikiwa uchaguzi huo hautaleta matokeo yenye mafanikio au kuahirishwa tena, kwa lengo la kuwalinda raia wa Maldives.
Rais wa kwanza kuchaguliwa kidemokrasia nchini humo ambaye ni kaka wa kiongozi wa zamani aliyetawala kiimla, Yaamin Abdul Gayoom, alipitishwa kugombea kiti hicho kufuatia kura zilizopigwa wiki iliyopita.
Lakini mahakama kuu iliingilia kati na kupinga matokeo hayo kwa mara nyingine na kuahirisha zoezi zima la uchaguzi kufanyika siku iliyofuatia, jambo ambalo hata waangalizi wa uchaguzi wa ndani na wa kimataifa walilipinga ambao walitangaza kuwa uchaguzi huo ulikuwa huru na wa haki.
Uchaguzi huo ukapangwa kufanyika tena mwanzoni mwa mwezi huu, lakini mahakama hiyo ikaingilia kati na kuahirisha hadi Jumamosi Novemba 16, ambapo wananchi wanatarajiwa kupiga kura zao.
Awali uchaguzi huo ulipangwa kufanyika Jumapili iliyopita, siku ambayo rais wa zamani wa nchi hiyo, Mohamed Nasheed, alitangazwa mshindi katika hatua ya kwanza ya kupitishwa kugombea, ingawa kuna madai kuwa, wengi hawakuiunga mkono hatau hiyo.
Mahakama kuu yaahirisha uchaguzi mara tatu
Jambo lililoifanya mahakama kuu ya nchi hiyo kubadilisha tarehe kamili iliyokuwa imepangwa kufanyika kwa uchaguzi huo, na kusogeza hadi Novemba 7.
Hatua ya kuahirishwa tena kwa uchaguzi huo kumewafanya wananchama wa Jumuiya ya Madola wanaokutana mjini Colombo nchini Sri Lanka kuingilia kati na kutangaza kuanza kufanya uchunguzi wa kile iliyokiita kuwa vurugu za kisiasa kwa madai kuwa mahakama ya nchi hiyo inaingilia kati na kujaribu kuvuruga uchaguzi.
Taarifa ya Jumuiya hiyo imesema kuwa Mawaziri katika Jumuiya hiyo wataendelea kufuatilia kwa karibu hali ya mchakato wa uchaguzi wa Maldives katika siku zilizosalia, huku wakiendelea na mkutano wake wa siku tatu huko mjini Colombo, Sri Lanka.
Uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi nchini humo ulifanyika kwa mara ya kwanza mwaka 2008, kufuatia Maumoon Abdul Gayoom kuiongoza nchi hiyo miaka 30 ya utawala wa kiimla.
Mwandishi: Flora NzemaAFP
Mhariri: Josephat Charo