1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vita Gaza vyawanufaisha watawala wa kiimla Mashariki ya Kati

4 Septemba 2024

Mzozo wa Gaza umewaruhusu watawala wa kiimla katika eneo hilo kung'arisha taswira zao, kutetea heshima ya Waarabu, na kutumia maandamano dhidi ya Israel kuzitimua NGOs za kigeni na kukandamiza wapinzani wao.

Rais wa Misri Abdel-Fattah al-Sisi
Rais wa Misri Abdel-Fattah al-Sisi ni mmoja wa watawala wa Mashariki ya Kati wanaonufaika na mzozo wa Mashariki ya Kati.Picha: THIBAULT CAMUS/AFP via Getty Images

Katika siku za hivi karibuni, baada ya mashambuliano makubwa ya makombora kati ya Israel na Hezbollah, kiongozi wa Misri Abdel-Fattah el-Sissi alizungumza na mmoja wa majenerali wakuu wa Marekani, ambapo alitahadharisha juu ya hatari ya kuongezeka zaidi kwa mgogoro wa Gaza.

Rais huyo wa Misri amesema jumuiya ya kimataifa inapaswa kufanya juhudi zote na kuongeza shinikizo ili kuepusha kuongezeka kwa uhasama unaotishia usalama na utulivu wa eneo la Mashariki ya Kati.

Rais el-Sisi amesema hayo baada ya ziara ya jenerali wa Marekani, Charles Quinton Brown nchini Misri. Kiongozi wa Misri alitoa kauli hiyo muda mfupi baada ya Israel na wapiganaji wa Hezbollah kushambuliana.

Pamoja na Marekani na Qatar, Misri ni sehemu ya wajumbe wa wapatanishi wanaojaribu kufanya mazungumzo juu ya kusimamisha mapigano kwenye Ukanda wa Gaza, ambako Israel imeendeleana operesheni yake ya kijeshi tangu Hamas walipofanya mashambulio ya Oktoba 7.

Kauli hizo zinamsaidia el-Sissi kuijenga haiba yake. Hayo ameyasema Hossam el-Hamalawy, mtafiti na mwanaharakati wa Misri anayeishi nchini Ujerumani ambaye anaandika jarida linaloangazia siasa za Misri.

Rais Abdel Fattah El-Sisi akizungumza katika kikao cha mawasilisho wakati wa mkutano wa "Wito wa Hatua: Mwitikio wa Haraka wa Kibinadamu kwa Gaza", kwenye Bahari ya Chumvi, Jordan Juni 11, 2024.Picha: Alaa Al Sukhni/REUTERS

Mtafiti huyo ameeleza kwamba vita vya Gaza kimsingi vimesaidia kuimarisha zaidi utawala wa el-Sisi. Vita hivyo vya Gaza vimekuwa njia ya Misri ya kuingiza vipato baada ya sekta za utalii na usafirishaji wa meli kukwama.

Soma pia: 

Kutokana na hali hiyo Marekani na Umoja wa Ulaya zinajibiidisha kuinusuru Misri. Vitega uchumi vyenye thamani ya dola bilioni 50 vimewekezwa nchini Misri ambavyo vimeiwezesha  sarafu ya Misri, kuepuka kusambaratika.

"Vita vya Gaza kimsingi vimesaidia kuimarisha utawala wa el-Sissi hata zaidi. Utawala huu ambao kwa miaka michache iliyopita umelegalega katika nyanja ya utawala, na umeshindwa katika nyanja ya Uchumi hatua ambayo imeiingiza nchi katika kiwango cha kutisha cha deni ambacho hakijawahi kuonekana katika historia ya Misri," alisema Hossam el-Hamalawy. 

Soma pia: Vita Gaza ni mtaji wa kisiasa kwa watalawala wa kikanda?

"Lakini ghafla, kutokana na kuzuka kwa vita, hata ingawa wakati mwingine hali hii imetishia utulivu wa nchi pamoja na maandamano ya hapa na pale yaliyotokea mwanzoni mwa vita ambayo yalizimwa kikatili – hali hii imemsaidia el- Sisi kuimarisha utawala wake kutokana na Marekani na mataifa mengine yenye nguvu ya duniani kukimbilia kumwokoa kwa kutangaza fedha kutolewa zaidi ya dola bilioni 57 kwa Misri mwaka huu katika miezi michache iliyopita."

Kupambana na ugaidi vs ukandamizaji

Mtafiti al-Hamalawy amesema rais el-Sisi anakwenda nchi za magharibi kusema kwamba anapambana na ugaidi na kwa hivyo yeye ni muhimu kwa utulivu wa Mashariki ya Kati. Lakini wakati huo huo anawakandamiza wapinzani wa ndani ya nchi yake.

Amesema miongoni mwa waliokamatwa hivi karibuni ni Ashraf Omar, mchoraji wa vibonzo. Msanii huyo anashilikiwa kwa sababu ya vibonzo anavyochora. Anashikiliwa kwa tuhuma za ugaidi kama ilivyo kwa waandishi wengine wa habari wa Misri na wafanyakazi wa vyombo vya habari kwa jumla.

El-Sissi anatumai kuona hasira za wananchi zikielekezwa kwa Israel na pia kwa Marekani kwa sababu ya kuwaunga mkono waisraeli katika vita vya Gaza.

Mtaalamu wa Mashariki ya Kati al-Hamalawy akiwa katika mjadala na DW.Picha: DW

Alia Brahimi na Karim Mezran watafiti waandamizi katika Baraza la Atlantiki, waliandika katika chapisho la taasisi yao la mwezi Julai kwamba el-Sisi si mtawala pekee katika Mshariki ya Kati anayenufaika na vita Gaza. Wamesema watawala wa Algeria,Tunisia, Libya na Morocco pia wameweza kutumia masuala ya vita, wakimbizi, migogoro ya kimataifa na siasa za hamasa barani Ulaya kwa lengo la kunusuru uchumi wa nchi zao.

Algeria imeutumia mgogoro wa Gaza, kwenye baraza la usalama la Umaoja wa Mataifa kuonesha mshikamano na nchi za kiarabu. Lakini wakati huo huo Algeria inawaandama wanaharakati wanaotetea demokrasia na haki za binadamu nchini humo.

Nchini Tunisia, wanaharakati wanasema rais Kais Saied amekuwa akitumia msimamo wa kuiunga mkono Palestina kuwavuruga raia kutokana na mzozo wa kiuchumi huku akiendelea kuukandamiza upinzani nchini Tunisia.

Marc Lynch, profesa wa sayansi ya siasa na masuala ya kimataifa katika Chuo Kikuu cha George Washington, amesema haamini kwamba mambo yanaweza kuendelea hivi. Amesema, tawala zinatakiwa kuwa makini zaidi katika kujibu masuala kama vile vita vya Israel na Wapalestina.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW