Vita Iran: Mataifa ya Ghuba hayataki kuhusika moja kwa moja
11 Machi 2026
Zaidi ya siku kumi baada ya kuishambulia Iran kwa pamoja, Marekani na Israel zimeshuhudia pengo linaloongezeka katika maoni ya umma, huku Rais Donald Trump akikabiliwa na ukosoaji mkubwa ukiwemo kutoka kwa wanachama wa chama chake cha Republican wanaosema vita hivyo vinapingana na ahadi yake ya "Marekani Kwanza" aliyoitoa wakati wa kampeni yake.
Wachambuzi wanaonya kwamba vita hivyo vinapingana na ahadi ya Trump ya kukomesha migogoro ya nje na vinaongeza wasiwasi wa kiuchumi.
Rais wa Iran Masoud Pezeshkian, ameandika kwenye mitandao ya kijamii kwamba "baadhi ya nchi" zimeanza juhudi za upatanishi, bila kufafanua zaidi.
Qatar imezihimiza pande zote zinazohusika kujizuia ili kutoa nafasi kwa mazungumzo ya kidiplomasia. Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Qatar, Majed Al-Ansari, pia amesisitiza kwamba katika mzozo huo pande zinazohusika zinapaswa kuacha kuilenga miundombinu ya kiraia, akibainisha kuwa shambulio lolote dhidi ya miundombinu hiyo halikubaliki.
Kwa upande wake Urusi imesema pendekezo lake kuhusu kuwa mpatanishi bado lipo mezani. Msemaji wa Ikulu, Dmitry Peskov amesema Urusi iko tayari kusaidia kuvimaliza vita katika eneo la Mashariki ya Kati hasa baada ya Rais wa Urusi Vladimir Putin kuzungumza na kwa njia ya simu na Rais wa Marekani Donald Trump, siku ya Jumatatu.
China inataka kukomeshwa mara moja kwa operesheni za kijeshi katikaeneo la Mashariki ya Kati, imesema imempeleka mjumbe wake huko Mashariki ya Kati kwa ajili ya juhudi za upatanishi.
Wakati huo huo Mawaziri wa nishati wa G7 leo Jumatano wamesema wako tayari kuchukua "hatua zote muhimu" kwa ushirikiano na Shirika la Nishati la Kimataifa (IEA) ili kukabiliana na kupanda kwa bei ya mafuta ghafi kutokana na vita vya Mashariki ya Kati.
Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron, ambaye nchi yake inashikilia urais wa kupokezana wa Kundi la Nchi Saba zenye uchumi mkubwa, anatarajiwa kuongoza mkutano utakaojadili athari ya vita katika eneo la Mashariki ya Kati.