1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaIsrael

Ujerumani yahimiza kuendelea mazungumzo ya amani huko Gaza

6 Mei 2024

Ujerumani imezitaka pande zinazohusika na mzozo wa Gaza kuendeleza mazungumzo ili kufikia makubaliano ya kusitisha mapigano huko Gaza baada ya awamu nyingine ya mazungumzo kati ya Israel na Hamas kushindwa.

Vita vya Gaza |
Picha iliyopigwa Mei 6, 2024 inaonyesha moshi ukifuka kufuatia mashambulizi ya mabomu mashariki mwa Rafah kusini mwa Ukanda wa Gaza katikati ya mzozo unaoendelea kati ya Israel na Hamas.Picha: AFP/Getty Images

Wizara ya Afya ya Gaza inayoongozwa na Hamas imesema Jumatatu kwamba karibu watu 34,735 wameuawa katika eneo hilo la Palestina katika vita baina ya Hamas na Israel vilivyodumu kwa miezi saba sasa. 

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Ujerumani amesema hakuna sababu ya kuhujumu mazungumzo hayo na pande zote zinatakiwa kufanya jitihada za kila hali kuhakikisha misaada ya kiutu inawafikia watu wa Gaza lakini hatimaye kufikiwe makubaliano ya kuchiliwa mateka.

Soma pia: Mazungumzo ya kusaka mkataba wa usitishwaji mapigano Gaza kuendelea mjini Cairo

Siku ya Jumapili, wanajeshi wanne wa Israel waliuawa na wengine kujeruhiwa, lilisema jeshi la Israel baada ya msururu wa makombora kurushwa kuelekea mpaka wa Kerem Shalom, uliopo kati ya Israel na Gaza. Tawi la kijeshi la Hamas lilidai kufanya shambulizi hilo lililosababisha mamlaka za Israel kufunga kivuko kilichotumika kupitisha misaada kuingia Gaza.

Waziri wa wizara ya Mambo ya Nje wa Ujerumani Annalena Baerbock akiwa ziarani huko Fiji amesema leo kwamba shambulizi hilo limeonyesha "sura halisi" ya Hamas na kuongeza kuwa kukishambulia kituo muhimu cha kupitisha misaada ya kiutu kunaonyesha kwa mara nyingine kwamba magaidi wa Hamas hawajali chochote kuhusu mahitaji ya kiutu ya watu wa Gaza.

Soma pia:Ujerumani yasema mazungumzo ya Gaza hayapaswi 'kuhatarishwa'

rais Joe Biden wa Marekani anatarajiwa kuzungumza na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu juu ya uvamizi kwenye mji wa Rafah.Picha: Brendan Smialowski/AFP

Rais Joe Biden wa Marekani anatarajiwa kuzungumza na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu hii leo baada ya jeshi la taifa hilo kuwataka Wapalestina kuondoka mashariki mwa Rafah kabla ya kuanzisha mashambulizi kwenye eneo hilo, imesema Ikulu ya White House. Msemaji wa Baraza la Usalama wa Taifa amesema Marekani tayari iliweka wazi juu ya uvamizi huo kwenye mji wa Rafah.

Msemaji wa serikali ya Israel David Mencer amesisitiza ni lazima wachuke hatua hiyo ili kuwaangamiza kabisa Hamas na kuahidi kwamba watahakikisha mateka wanaoshikiliwa na kundi hilo wanarejea nyumbani.

Alisema, "Lengo la hatua hii ni kuangamiza vikosi vinne vya Hamas vilivyoko huko Rafah. Walisema wazi wazi kabisa kwamba watajiunda upya, kuichukua tena Gaza na kufanya shambulizi kama la Oktoba 7 mara nyingine, na mara nyingine. Linapokuja suala la mateka wetu, tutafanya kila liwezekanalo kwa uwezo wetu kuwarejesha nyumbani kwa njia ya kidiplomasia na kijeshi. Lakini kitu kimoja ambacho hatutaruhusu ni Hamas kubaki imara hadi mwishoni mwa vita hivi. Na ikitokea hivyo, litakuwa ni janga kubwa sana kwa Israel." 

Israel yashambulia maeneo ya kusini mwa Gaza

Anasema hayo, wakati ripoti za mchana wa leo zikisema jeshi la nchi hiyo, IDF limefanya shambulizi kwenye baadhi ya maeneo kusini mwa Gaza ambako zaidi ya watu milioni moja waliokimbia mapigano walikuwa wamejihifadhi.

Wapalestina waliofurushwa makwao wakiondoka huko Rafah kusini mwa Ukanda wa Gaza kufuatia amri ya jeshi la Israel kuwahamisha, Mei 6, 2024.Picha: AFP/Getty Images

Hofu inazidi kutanda ya uvamizi kamili kwenye mji wa Rafah. Afisa wa Hamas Izzat al-Rashiq ametahadharisha akisema kwenye taarifa kwamba operesheni yoyote ya Israel huko Rafah itahujumu mazungumzo ya amani. Misri nayo kwa upande wake imeonya juu ya operesheni kama hiyo, ikisema itasababisha kitisho kikubwa kabisa cha kibinaadamu.

Soma pia:Israel yaanza kuwahamisha raia 100,000 kutoka Rafah

Katika hatua nyingine, gazeti la Marekani la The Times limearifu hii leo kwamba mkuu wa idara ya ujasusi nchini humo William Burns anatarajiwa kuzungumza na Netanyahu, kujaribu bahati yake katika juhudi za kufikia makubaliano ya kuachiliwa mateka, wakati atakapozungumza na Netanyahu hii leo.

Burns ambaye pia ni miongoni mwa ujumbe wa wapatanishi kutoka Marekani, Misri na Qatar anajaribu kusaka njia ya kuongeza matumaini ya kufikiwa makubaliano hayo licha ya Israel kuanza kuwaondoa wakazi kutoka kwenye baadhi ya maeneo ya mji wa Rafah.

Kutoka huko New York, Umoja wa Mataifa nao unapanga kulaani machafuko yasiyokubalika yanayofanywa na Israel dhidi ya wanawake na watoto katikati ya vita vinavyoendelea kwenye Ukanda wa Gaza na hasa unyanyasaji wa kingono na kuwapoteza watu kinguvu. Ripoti ya ujumbe maalumu unaoteuliwa na Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa umesema kwenye taarifa yake kwamba wanasikitishwa na hatua ya Israel ya kuwalenga wanawake kiholela, hatua inayowanyima haki zao za kimsingi za kibinadamu.