Vita,njaa na mivutano ya kisiasa yaikabili Somalia
3 Mei 2017Katika ripoti yake iliyoangazia maswala 10 yanayopaswa kupewa kipambauele, Somalia kuhusiana na haki za binadamu, Shirika la human rights watch limesema matatizo mengine yanapaswa kushughulikiwa kwa haraka pamoja na yale yanayotokana na vita, njaa na mivutano ya kisiasa. Tangu kuchaguliwa rais na wabunge na maseneta, Mohamed Abdullahi Farmajo amekabiliwa na changamoto chungu nzima katika kutafuta suluhu ya matatizo yanayoikabili Somalia.
Ugaidi, uchumi unaoyumba, uhaba wa chakula na mivutano ya kisiasa kati ya koo mbalimbali ni miongoni tu mwa matatizo hayo. Kwa mujibu wa shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch, uongozi mpya Somalia haujachukua hatua za haraka kuwalinda raia wote hasa walio katika hatari ya kudhulumiwa kwa kuwachukulia hatua wahusika. Mapigano kati ya vikosi vya serikali na wapiganaji wa kundi la Al-Shabaab, pia yametajwa kuwaumiza zaidi raia.Uchunguzi uliofanywa na Human rights Watch umebaini kuwa pande zote mbili, zimesababisha mauaji na ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu miongoni mwa raia katika maeneo wanayodhibiti.Serikali ya Somalia inapanga kuimarisha operesheni zake za kijeshi ili kuwaangamiza kabisa wapiganaji wa kundi la al-shabaab, na hilo limelitia wasiwasi shirika la human rights watch huku maafisa wake wakisema itakuwa muhimu kwanza kuwepo utaratibu wa kuhakikisha kuzingatiwa nidhamu na kwa vikosi vya usalama kuwalinda raia dhidi ya dhulma.
Idara ya ujasusi nchini Somalia inadaiwa kuwanyima wafungwa haki zao za kimsingi, kuwazuilia washukiwa kwa muda mrefu bila kuwafungulia mashtaka, kuwazuia kupata huduma za kisheria na kuwatesa washukiwa ili kupata ushahidi. Mazungumzo yanayoendelea kwa sasa kuhusu kuundwa mfumo wa kitaifa wa usalama pia yanadaiwa kupuuza utendakazi wa idara ya ujasusi.Katika miaka ya hivi karibuni, utawala nchini Somalia umetegemea zaidi mahakama za kijeshi kushughulikia kesi mbalimbali ambazo zinapaswa kushughuliwa na mahakama za kawaida kuanzia kesi za ugaidi na nyingine nyingi dhidi ya raia swala ambalo ni kinyume na sheria za kimataifa.Kwa mujibu wa shirika la kutetea haki za kibinadamu la Human rights Watch wahusika wote katika vita nchini Somalia pia wamekuwa wakiwatumia watoto walio chini ya umri wa miaka 18 katika vikosi vyao licha ya kuwa ni ukiukwaji mkubwa wa sheria za kimataifa. Huku pia taifa hilo likikabiliwa na baa la njaa, serikali mpya imetakiwa kutokiuka haki za watu waliochwa bila makao ikiwemo pia kutowafurusha kwa nguvu raia kutoka maeneo wanamoishi.
Mwandishi:Jane Nyingi/Human rights Watch
Mhariri:Josephat Charo