Vita sio tu mabomu na mizinga, habari potofu pia
17 Mei 2022Uvamizi wa Urusi nchini Ukraine umesababisha kuenea kwa taarifa potofu kwenye mitandao ya kijamii ambayo inawapa changamoto waandishi wa habari nawadadisi wa ukweli kote ulimwenguni, hilo pia limetoa mwanga juu ya kampeni za taarifa potofu barani Afrika.
Justin Arenstein mwanzilishi na Mkurugenzi Mtendaji wa mradi teknolojia ya uchunguzi na uandishi wa habari wa takwimu Afrika CFA.
Amezungumza na DW jinsi ya mikakati ya upotoshaji wa habari unavyofanywa kuhusiana na Ukraine inavyotumiwa na Urusi barani Afrika kwa miaka kadhaa sasa.
Justin ameiambia DW katika uchunguzi wao walioanza tangu mwaka 2012 walifuatilia kwa kina makundi ya wahalifu kama vile akina Gupta na wataalamu wao wa mikakati kutoka Uingereza waliohusika katika ufisadi Afrika Kusini.
Soma zaidi:Je unaweza kubaini habari za uwongo?
Kadhalika walitazama kampeni za upotoshaji zinazoambatana na uasi, migogoro inayotengenezwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe katika eneo la Sahel, Ethiopia, Jamhuri ya Afrika ya Kati , Niger, Mali na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Alisema waasi wapo vizuri katika kusambaza ujumbe wa kuashiria kushindwa kwa serikali au michakato ya kidemocrasia, lakini waligundua kulikuwa na uratibu mkubwa wa ujumbe wa upotoshaji.
Aliongeza, mataifa makubwa yanajiingiza katika nchi ndogo na kutoa maoni ya kupotosha kwa umma.
Urusi kuusaka Urafiki wa kimaslahi Afrika.
Analiangalia taifa la Urusi namna lilivyojihusisha na Sudan kabla ya mapinduzi, huku likiusaidia utawalana pia kujaribu kutaka jeshi lake la majini lipate ushawishi mkubwa katika bandari ya Shamu, kampeni zilizokwenda sawia huko Afrika ya kati, Mali na hivi karibuni Burkina Faso.
Walitumia mbinu kama hizo katika nchi hizo ikiwa ni pamoja na msemo " Urusi haijatawala Afrika" na kujiweka kama rafiki wa karibu wa Afrika akisaidia kupambana na ukoloni na ubeberu.
Hii ikijionesha utofauti wake na wakoloni kama Ufaransa, Uingereza na mataifa mengine ya Ulaya ambayo yanahistoria pana ya utumwa.
Urusi kuivamia Ukraine na wanafunzi wenye asili ya Afrika waliojaribu kuvuka mpaka hadi Poland wakikumbana na ubaguzi mkubwa wa rangi,hatua hii imewafanya waafrika wengi kuamini Putin yupo sahihi na kile kinachoendelea Ukraine. Aliongeaza mkurugenzi huyo kutoka CFA.
Soma zaidi:Mitandao ya Kijamii yalaumiwa kusambaa kwa Habari za Uongo
Katika mahojiano hayo maalum na DW mtaalamu huyo aliendelea kueleza kwamba kwa upande mwingine Ulaya na washirika wake, kushiriki vita vya ukombozi huko Syria na Iraq vilizua swali lingine kwamba Urusi iliwahi kufanya kitendo kama hicho? alijibu mwenyewe hapana akimaanisha Urusi haijatendewa haki ya kulaumiwa kuivamia Ukraine.
Mbinu ya kutumiwa waafrika kusambaza propaganda
Hapo awali walituma ujumbe mbaya kwa kutumia majukwaa ya kimtandao, ujumbe ambao haukuandikwa na waafrika, ilikua ni rahisi kuzitambua na kutoziamini, lakini badae mbinu ya kuwatumia waafrika katika propaganda hiyo ilishika hatamu na hata waafrika kuanza kuamini kile kilichokuwa kikiandikwa katika majukwaa ya mtandaoni.
Alitolea mfano wa sinema ya mtindo wa Hollywood ijulikanayo kwa jina la the Tourist, filamu ya kivita inayowaonyesha mamluki wa Urusi kama watu wema wanaopigana na wanajihadi wabaya na serikali zilizotzopea kwenye rushwa na ufisadi.
Ndani ya mahojiano hayo anazidi kuitazama mitandao ya kijamii inayosambaza maudhui mbalimbali kwa kutumia teknolojia ya kisasa pamoja na akaunti fake.
Soma zaidi:Msalaba Mwekundu laonya kuhusu habari za uongo za chanjo ya COVID-19
Alisisitiza, maudhui hayo yanatumiwa na wanablog wa Urusi na Afrika ambao hunukuu kwamba habari hizo zinatoka katika vyanzo tofauti.
Hizi zote anataja ni kampeni zinazoendeshwa ili Urusi kupata uungwaji mkono barani Afrika, kiuchumi na hata kijeshi.
Alikwenda mbali na kueleza kwamba ni kubadilisha hali ya inachotokea Ukraine ili kujipatia soko la bidhaa za Urusi na huduma mbalimbali.
Aliongeza kwamba maslahi ya Urusi barani Afrika yanaanzia kwenye upatikanaji wa madini na rasilimali nyingine hadi biashara ya nje na miradi mikubwa ya miundombinu kama vile miradi ya kinu cha nyuklia katika nchi kama vile Afrika Kusini, pamoja na kuendeleza dhana ya Afrika kutotengamana na upande wowote.