1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vita Sudani kuligawa taifa pande mbili?

20 Novemba 2023

Vita nchini Sudan vimekuwa vikiendelea, zaidi ya miezi saba sasa na maelfu ya watu wameuwawa huku wengine mamilioni wakiachwa bila makaazi.

Mapigano | Mgambo wa RSF akiwa katika usafiri wa ngamia
Mapigano | Mgambo wa RSF akiwa katika usafiri wa ngamiaPicha: Hussein Malla/AP/picture alliance

Hivi sasa wataalamu wanaonya kwamba nchi hiyo  inakabiliwa na kitisho cha kugawika,na kufuata mfano wa nchi kama Libya ambayo imegawika pande mbili.

Sudan iko kwenye vita vya wenyewe kwa wenyewe, vinavyohusisha jeshi la serikali na kundi la wanamgambo la RSF linaloongozwa na jenerali Mohammed Dagalo.

Na ripoti zinasema kuna mauaji mapya ya watu wengi katika jimbo la Magharibi la Darfur.

Watalaamu wanazungumzia khofu ya vita hivyo kugeuka kuwa vibaya zaidi kama ilivyotokea nchini Libya na kusababisha kugawika mapande mawili.

Libya nchi ya Kaskazini mwa Afrika ambayo hadi sasa inakabiliwa na machafuko imegawika ikishuhudiwa kuwepo serikali mbili zinazokinzana, moja ya Mashariki na nyingine Magharibi na kila serikali ina watawala wake.

Soma pia:Wasiwasi wa mafuriko watanda Sudan kufuatia shambulizi katika bwawa

Msemaji wa kundi kubwa la kiraia nchini Sudan,linalopigania uhuru na mabadiliko, na  ambalo liliondolewa kwa nguvu madarakani mwaka 2021 kupitia mapinduzi yaliyofanywa na majenerali wote wawili wanaovutana hivi sasa, Khaled Omar Youssef amesema mapigano yanayoendelea nchini Sudan yanaweza kusababisha hali ya kutisha ikiwemo kutokea mpasuko.

Ameliambia shirika la habari la AFP, kwamba kuongezeka kwa mapambano ya kijeshi yanayojifungamanisha na mitizamo ya kikabila na kimaeneo,ni mambo yanayozidisha mpasuko wa kijamii ndani ya Sudan.

Mtawanyiko katika udhibiti wa maeneo muhimu

Mpaka hivi sasa kundi la wanamgambo la RSF linadhibiti sehemu kubwa ya mji mkuu Khartoum na jimbo la Darfur wakati jeshi likidhibiti maeneo ya Kaskazini na Mashariki mwa nchi hiyo.

Wanamgambo wa RSF wakiwa katika doria SudanPicha: Hussein Malla/AP/picture alliance

Jeshi ambalo linaongoza serikali ya Sudanlimekimbilia katika mji wa Masharikiwa Port Sudan,huku pia ikielezwa kwamba pande zote mbili zimeshindwa kupiga hatua yoyote katika mazungumzo yaliyosimamiwa na Marekani na Saudi Arabia mwezi huu na baadhi ya watu wanahofia juu ya kutokea hali mpya ya mgawanyiko.

Mwishoni mwa wiki iliyopita Martha Ama Akyaa Pobee,naibu wa katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Afrika, anayehusika na masuala ya kisiasa na amani aliizungumzia hali ya Sudan katika kikao maalum cha baraza la usalama la Umoja wa Mataifa na huu ulikuwa mtazamo wake.

''Mgogoro nchini Sudan umeendelea kwa zaidi ya miezi saba huku kukiwa hakuna dalili ya kumalizika." Alikiambia kikao maalum.

Soma pia:Ujumbe wa UN watakiwa kumaliza shughuli zake Sudan

Aliongeza kwamba badala yake, vita vimeongezeka katika wiki za hivi karibuni, wakati pande zote zinazovutana zikitangaza kuwa tayari kushiriki mazungumzo ya kusitisha vita, lakini vitendo ndani ya Sudan vinaonesha hali tofauti.

Tangu tarehe 15 mwezi Aprili vita kati ya mkuu wa majeshi Abdel Fattah al Burhani na aliyekuwa makamu wake ambaye ni kamanda wa kundi la wanamgambo la RSF Mohammed Dagalo vimesababisha watu milioni 6 kukimbia makaazi yao,wengine wakibakia Sudan na wengine wakiwa wamevuka mipaka na kuingia nchi jirani.

Kufikia mwishoni mwa mwezi uliopita zaidi ya watu 10,000 waliuwawa kwa mujibu wa makadirio yaliyotolewa na Taasisi moja inayofuatilia migogoro ya kijeshi na ukusanyaji data duniani, ACLED.

Mauaji ya raia kufuatia oparesheni za RSF

Hata hivyo katika mwezi huu wa Novemba, ripoti mpya zilianza kujitokeza  juu ya kutokea mauaji ya watu wengi kufuatia operesheni kubwa iliyoanzishwa na kundi la wanamgambo la RSF katika eneo kubwa la jimbo la Darfur, na kuchukua udhibiti wa kambi za kijeshi katika miji yote kasoro mji mmoja mkubwa.

Katika mji wa Ardamata peke yake huko Magharibi mwa Darfur, Umoja wa Mataifa uliripoti kwamba takriban maeneo 100 ya kuhifadhi waliokimbiamakaazi yao yaliharibiwa kabisa huku wapiganaji wakiingia nyumba hadi nyumba kuua raia,na zaidi ya watu elfu 8 wakikimbilia nchi jirani ya Chad.

Mashirika na raia wote walililaumu kundi la RSF na washirika wao,wanamgambo wa kiarabu ambao wameendesha kampeini ya kuwalenga watu wa jamii ya kabila la Massalit ikiwemo kuwauwa viongozi wa kabila hilo.

Nchi kadhaa zaondoa raia wake Sudan

01:21

This browser does not support the video element.

Soma pia:Umoja wa Ulaya wahofia kutokea mauaji mengine ya kimbari huko Darfur

Kutokana na hali hiyo,kwa mujibui wa mchambuzi wa kisiasa na mwandishi habari Fayez al Salik ikiwa hakuna suluhu ya kisiasa itakayopatikana nchini Sudan hali ya taifa hilo inaweza kuwa kama iliyoko Libya,akimaanisha kwamba huenda zikawepo zaidi ya serikali moja,zitakazoshindwa kuwa na uthabiti au kutambuliwa kimataifa.

Japokuwa Dagalo ana marafiki wenye nafasi kubwa katika nchi kadhaa ikiwemo katika Umoja wa Falem za kiarabu,wataalamu wanasema Burhani bado ameendeleza dhima yake kama mtawala wa serikali ya Sudan katika jukwaa la kimataifa.

Hivi karibuni ameshuhudiwa akishiriki mikutano ya kilele kote katika Umoja wa Mataifa na katika Jumuiya ya Umoja wa nchi za Kiarabu.

Kwa upande mwingine Umoja wa Mataifa umeonya kwamba historia inajirudia na mahakama ya ICC imeanzisha uchunguzi mpya kuhusu mauaji nchini humo.

         

 

     

   

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW