1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vita vya Gaza na Ukraine vyatia kiwingu sikukuu ya Krismasi

25 Desemba 2023

Waumini wa kikristo duniani wanasherehekea sikukuu ya Krismasi leo inayokumbuka kuzaliwa kwa Yesu Kristo zaidi ya miaka 2000 iliyopita.

Iran Tehran | Duka la Krismasi
Duka la bidhaa za Krismasi mjini TehranPicha: Morteza Nikoubazl/NurPhoto/picture alliance

Sherehe za mwaka huu zinafanyika chini ya kiwingu cha mizozo duniani hususani vita huko Ukanda wa Gaza na ile inayoendelea nchini Ukraine. Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani Papa Francis amefungua pazia la sherehe hizo kote duniani kwa kutoa mwito wa amani.

Kwenye mahubiri yake ya mkesha wa sikukuu ya Krismasi, Baba Mtakatifu Francis amesema "mioyo yetu iko Bethlehem, ambako mwanamfalme wa amani kwa mara nyingine amekataliwa kwa kushamiri kwa vita, mapigano ya kutumia silaha ambayo hata leo yanamzuia kupata nafasi ulimwenguni."

Mapema wakati wa ibada ya asubuhi siku ya Jumapili, Papa Francis alisema kichwani mwake anauwaza umma unaoteseka kwa vita huko Palestina, Israel na Ukraine.

Bethlehem yafuta sherehe za Krismasi kuomboleza vifo vya mapigano ya Gaza 

Mji wa Bethlehem inaoaminika Yesu Kristo alizaliwa zaidi ya miaka 2000 iliyopita.Picha: Mahmoud Illean/AP Photo/picture alliance

Mjini Bethlehem inakoaminika Yesu Kristo alizaliwa zaidi ya miaka 2000 iliyopita, sherehe za kila mwaka za Krismasi zimefutwa ikiwa ni pamoja na shamra shamra na mapambo ya mji mzima ambayo huwavutia maelfu ya watalii.

Hakuna mti mkubwa wa Krismasi ambao huwekwa kila mwaka kwenye mji huo wala maandamano ya vikundi vya kwaya na muziki. Mji umepooza na ni taa chache tu ndiyo zimetundikwa kuashiria msimu wa Krismasi.

Katikati mwa mji huo uliopo eneo la Ukingo wa Magharibi, bendera kubwa ya Palestina imetandazwa juu ya bango lenye ujumbe unaosomeka "kengele za Bethlehem zinagongwa kuhimiza usitishaji mapigano Ukanda wa Gaza"

"Watu wengi wanakufa kwenye ardhi hii," amesema Nicole Najjar, mwanafunzi wa miaka 18 alipozungumza na Shirika la Habari la AFP. "Ni ngumu kusherehekea wakati watu wetu wanakufa"

Syria na Uturuki nako maandalizi ya Krismasi yagubikwa na simanzi 

Michezo msimu wa KrismasiPicha: Bruna Prado/AP

Nchini Syria, makanisa yamepunguza shamrashamra na badala yake yameamua kufanya ibada kuonesha mshikamano na Wapalestina.

Huko Ukraine,  ambako Urusi iliivamia nchi hiyo karibu miaka miwili iliyopita, watu wanasherehekea Krismasi ya Disemba 25 kwa mara ya kwanza, ikiwa ni hatua ya kujitenga na ile ya tarehe 7 Januari chini ya madhehebu ya Orthodox. Mabadiliko hayo ni sehemu ya juhudi kubwa za nchi hiyo kujitenga na ushawishi na urithi wa Urusi.

Kusini mwa Uturuki, sehemu kubwa ya eneo hilo iliharibiwa na tetemeko la ardhi la mnamo mwezi Februari, waumini wamesherehekea misha ya mkesha kwenye mabaki ya kanisa huko Antakya.

"Ni muhimu kwetu kusherehekea kuzaliwa Yesu Kristo, lakini ni Krismasi ya huzuni sana," amesema Vehbi Tadrasgil, mwenye umri wa miaka 55 ambayo alipoteza mke na watoto wake wawili kati ya watu kwenye tetemeko la ardhi lililowauwa takribani watu 50,000 nchini Uturuki na zaidi ya 50,000 nchini Syria.