Vita vya Gaza: Ufaransa, UK na Canada zaikosoa vikali Israel
20 Mei 2025
Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron, Waziri Mkuu wa Uingereza Keir Starmer na mwenzake wa Canada Mark Carney walichukua hatua ya nadra ya kuikosoa vikali Israel na kutaja kushtushwa na harakati zake huko Gaza , wakisema iwapo haitositisha mashambulizi yake kijeshi na kuondoa vikwazo vya uingizwaji misaada ya kiutu, watachukua hatua madhubuti zaidi.
Viongozi hao wamesema hatua ya sasa ya Israel ya kuruhusu malori kadhaa kuingia Gaza haitoshi ukilinganisha na mahitaji ya watu wa Gaza hasa ikizingatiwa kuwa wakati wa utekelezaji wa mpango mfupi wa usitishwaji mapigano, karibu malori 600 ya misaada yaliruhusiwa kuingia Gaza kwa siku. Keir Starmer alifafanua kauli hiyo ya pamoja:
" Naomba niseme jambo kuhusu hali ya kutisha ya Gaza ambapo kiwango cha mateso kwa watoto wasio na hatia wanaoripuliwa tena kwa mabomu hakivumiliki kabisa. Mimi na rais wa Ufaransa na Waziri Mkuu wa Canada tunasisitiza ombi letu la kusitishwa kwa mapigano kama njia pekee ya kuwakomboa mateka, tunapinga uwepo wa makazi ya walowezi katika Ukingo wa Magharibi, na kuongeza kiwango cha misaada ya kibinadamu huko Gaza, kwa sababu kiwango cha sasa hakitoshi hata kidogo. Ni lazima turatibu majibu yetu, kwa sababu vita hivi vimedumu kwa muda mrefu mno na hatuwezi kuruhusu watu wa Gaza wafe njaa.”
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu aliwajibu viongozi hao kwamba kauli yao hiyo ni sawa na kulipatia "tuzo" kundi la Hamas ambalo pia limetakiwa kuwaachia huru mateka waliosalia.
Hatua ya kuruhusiwa misaada na mashambulizi Gaza
Shirika la Umoja wa Mataifa la huduma za kibinaadamu OCHA limesema hivi leo kuwa limepokea kibali kutoka Israel kinachowaruhusu kupeleka malori 100 ya msaada huko Gaza.
Jens Laerke, msemaji wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Uratibu wa Masuala ya Kibinadamu huko Geneva, alielezea matumaini yake kwamba msafara huo wa dharura utakaguliwa haraka na kuruhusiwa kuingia Gaza kufikia kesho Jumatano.
Licha ya shinikizo la kimataifa kuongezeka , Israel imeendeleza hivi leo mashambulizi yake huko Gaza na kusababisha vifo vya Wapalestina 50 wakiwemo wanawake na watoto.
Hayo yanajiri wakati waziri wa Mambo ya Nje wa Qatar Mohammed bin Abdulrahman Al Thani amesema mazungumzo ya kusitisha mapigano Gaza yanayoendelea mjini Doha nchini Qatar yamekwama kutokana na tofauti kubwa zinazoshuhudiwa kati ya pande mbili hasimu huku akiongeza kuwa mashambulizi mapya yanahujumu mchakato huo wa amani.
(Vyanzo: Mashirika)