Vita vya Iran vyapamba moto
4 Machi 2026
Sauti za miripuko ya makombora imesikika mjini Tehran leo Jumatano wakati vita kati ya Iran na washirika wawili Marekani na Israel vikiingia siku ya tano. Iran imekuwa ikijibu kwa kushambulia mataifa mbali mbali ya Ghuba na ndani ya Israel.
Wanamgambo washirika wa Iran walioko Iraq, pia wamefyetuwa makombora dhidi ya Jordan wakiisaidia Iran. Yote hayo yanashuhudiwa katika wakati Tehran inajiandaa leo Jioni kuanza kipindi cha siku tatu cha maomboleza kabla ya mazishi ya kiongozi wa juu zaidi wa nchi hiyo Ayatollah Ali Khamenei aliyeuwawa na Marekani.
Mashambulizi ya anga ya Marekani na Israel yameendelea mfululizo yakilenga maeneo mbali mbali ya Iran, kwa mujibu wa kituo cha televisheni ya taifa cha Iran, miripuko imesikika alfajiri leo kaskazini mashariki mwa mji mkuu Tehran lakini kituo hicho hakikutowa maelezo zaidi.
Miripuko ya mashambulizi ya makombora ya Iran ilisikika pia katika mji wa Jerusalem nchini Israel wakati Jeshi la nchi hiyo kwa upande wake likiripoti kwamba mifumo yake ya ulinzi wa anga iliwashwa kuzuia makombora ya Iran.
Mwandishi habari wa shirika la AFP amesimulia alivyoona moshi mzito ukifuka kaskazini mashariki mwa Tehran huku kishindo cha madege ya kivita yanayopita kwenye anga kikisikika kwenye majira ya alfajiri.
Hospitali ya shirika la hilali nyekundu ilishambuliwa na waokoaji wameripotiwa kuondowa wagonjwa katika mji wa Bushehr kufuatia mashambulizi ya Marekani na Israel.
Hospitali hiyo ya magharibi mwa Iran imeharibiwa kwa mashambulio ya anga yaliyofanywa jana.
Katika kile kinachoonekana ni kuongezeka kwa mapambano hivi leo Jumatano jeshi la walinzi wa mapinduzi ya Iran limesema limedhibiti kikamilifu mlango bahari wa Hormuz, hatua ambayo imetangazwa baada ya rais wa Marekani Donald Trump kunadi kwamba jeshi la wanamaji la Marekani liko tayari kuzisindikiza meli kupita kwenye eneo hilo.
Ikumbukwe kwamba jeshi la kimapinduzi la Iran liliweka wazi kwamba meli yoyote itakayothubutu kupita eneo hilo itaripuliwa.
Tehran imenadi kupitia kituo chake cha televisheni kwamba imefyetuwa makombora 40 ya masafa ya kati ikiyalenga maeneo kadhaa yanayofungamanishwa na jeshi la Marekani katika eneo la Mashariki ya kati.
Netanyahu: Tutashambulia kila eneo la Iran
Na katikati ya mashambulizi ya Marekani na Israel ambayo kwa mujibu wa jeshi la Israel yamekuwa yakilenga maeneo ya kiusalama ya Iran, Tehran imejiandaa kuanzia leo jioni kuanza siku tatu za maombolezi ya umma na maziko ya kiongozi mkuu wa taifa hilo Ayatollah Ali Khamenei ambapo jeneza litakalokuwa na maiti ya kiongozi huyo aliyeuwawa akiwa na umri wa miaka 86 litapelekwa kwenye msikiti mkubwa unaojulikana kama Imam Khomeini Mosalla mjini Tehran.
Wakati hali ya mambo ikifuatiliwa katika pande zote za vita hivi, kupitia ujumbe kwenye mtandao wa X, waziri wa ulinzi wa Israel hivi leo ametoa kitisho kwa Iran kwamba yoyote atakayechaguliwa kuwa kiongozi mpya wa juu nchini humo ataangamizwa.