1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaIsrael

Vita vya Israel-Hamas: Guterres atumia ibara ya 99 ya UN

7 Desemba 2023

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres, amelihimiza Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuchukua hatua ili kuepusha janga la kibinadamu katika Ukanda wa Gaza na tishio la usalama na amani ya kimataifa.

Antonio Guterres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa
Antonio Guterres, Katibu Mkuu wa Umoja wa MataifaPicha: Craig Ruttle/AP/picture alliance

Katika tukio la nadra, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres, amelihimiza Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, kuchukua hatua ili kuepusha janga la kibinadamu katika Ukanda wa Gaza.

Kupitia barua aliyoliandikia baraza hilo jana Jumatano, kwa mara ya kwanza tangu kuchukua ofisi mwaka 2017, Guterres alitumia sheria ya 99 ya mkataba wa Umoja wa Mataifa.

Kifungu hicho cha sheria ambacho hakijatumiwa kwa miongo kadhaa kimechochewa na maafa makubwa ndani ya Ukanda wa Gaza na Israel katika kipindi kifupi. Hali ya kibinadamu kusini mwa Gaza inakaribia kuwa 'mbaya zaidi'

Kwa kukitumia, Guterres analifahamisha Baraza la Usalamakuhusu kile anachokitizama kuwa hali inayoweza kuhujumu usalama na amani ya kimataifa.

Israel imeendelea na mashambulizi yake makali ya kulisambaratisha kundi la Hamas katika Ukanda wa Gaza.

Mlipuko ulisababisha moshi mkubwa kutanda katika anga ya Gaza mapema Alhamisi, mnamo wakati Israel ikiendelea na mashambulizi katika eneo hilo.

Moshi watanda katika anga ya Gaza, wakati wa mashambulizi ya vikosi vya Israel dhidi ya kundi la Hamas, Disemba 6, 2023.Picha: Jack Guez/AFP

Mashambulizi ya Israel yasambaratisha maeneo makubwa ya Ukanda wa Gaza

Katika vita hivyo vya Israel dhidi ya kundi la Hamas, vikosi vya Israel vimekuwa vikifanya mashambulizi makali ya makombora ambayo yamesambaratisha maeneo makubwa ya Ukanda wa Gaza.

Soma pia: Jeshi la Israel lauzingira mji wa Khan Younis

Mashambulizi ya anga na ardhini ya Israel katika eneo la kusini mwa Gaza, yamesababisha maelfu ya Wapalestina kuyahama makazi yao, na kuzidisha hali mbaya ya kibinadamu katika eneo hilo.

Eyad al-Hobi, ambaye ni mkaazi wa Gaza ambaye nyumba ya ndugu yake ilishambuliwa amesema "Kulitokea milipuko mitatu mikubwa. Kisha tukaona shambulizi kwenye ghorofa huko, anakoishi ndugu yangu. Iliharibiwa kabisa hadi sehemu ya chini. Kuna idadi kubwa ya waliouawa, takriban mashahidi 20, ukiondoa waliojeruhiwa". Ameongeza kuwa "wengi wa waliouawa walikuwa watoto na wanawake."

Soma pia: Vita vya Israel-Hamas vyazusha hofu ya ugaidi katika EU

Mapigano hayo pia yamedhoofisha juhudi za usambazaji vyakula, maji na dawa nje ya eneo la kusini mwa Gaza mnamo wakati tahadhari mpya za kijeshi kwa watu kuondoka katika maeneo yanayolengwa kushambuliwa, zikisababisha watu kubanana kwenye maeneo madogo zaidi ya kusini.

Kulingana na Umoja wa mataifa, makumi ya maelfu ya wakaazi wa Gaza wameyakimbia makaazi yao kufuatia vita vya Israel dhidi ya wanamgambo wa Hamas.Picha: Mohammed Dahman/AP/picture alliance

Maelfu wameyakimbia makaazi yao Gaza

Umoja wa Mataifa umesema tangu vita kuanza Oktoba 7, watu milioni 1.87 wameyakimbia makaazi yao. Hiyo ikiwa ni zaidi ya asilimia 80 ya idadi jumla ya watu wa Gaza.

Soma pia: Mzozo wa Gaza hauna mithili ukiangalia vifo vya wanahabari

Vita hivyo vilivyochochewa na shambulizi baya la kushtukiza la wanamgambo wa Hamas kusini mwa Israel na kusababisha vifo vya watu 1,200. Kundi hilo ambalo Israel, Marekani, Umoja wa Ulaya na nchi nyingine kadhaa zimeliorodhesha kuwa la kigaidi, pia liliwateka nyara takriban watu 240 na kuwapeleka Gaza.

Hadi sasa zaidi ya mateka wengine 100 wangali wanashikiliwa na Hamas.

Kulingana na wizara ya Afya ya Gaza inayodhibitiwa na Hamas, idadi ya watu ambao wameuawa Gaza kufuatia mashambulizi ya Israel, imezidi 16,200 na zaidi ya 42,000 wamejeruhiwa.

Wizara hiyo haitofautishi kati ya vifo vya raia na vya wanamgambo, lakini imesema asilimia 70 ya vifo hivyo ni vya wanawake na watoto.

Vyanzo: APTN, DPAE, APAE