1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaIsrael

Vita vya Israel-Hamas: Hamas yarusha roketi kuelekea Israel

7 Desemba 2023

Jeshi la Israel limesema Alhamisi kwamba kundi la Hamas limefyatua makombora kadhaa kutoka eneo ambalo si la kivita kusini mwa Ukanda wa Gaza kuelekea Israel.

Machafuko katika mpaka wa Israel na Lebnon kati ya vikosi vya Israel na vuguvugu la Hezbollah yatajwa kuwa mabaya zaidi tangu vita vya pili vya Lebanon mwaka 2006.
Machafuko katika mpaka wa Israel na Lebnon kati ya vikosi vya Israel na vuguvugu la Hezbollah yatajwa kuwa mabaya zaidi tangu vita vya pili vya Lebanon mwaka 2006.Picha: Jalaa Marey/AFP

Kulingana na jeshi la Israel, kundi la Hamas lilifyatua roketi 12 Jumatano jioni katika mji wa Beersheba kusini mwa Israel.

Kundi hilo la wanamgambo wa Kiislamu linaripotiwa kurusha makombora hayo katika eneo lililoko karibu na mahema ya Umoja wa Mataifa na kusababisha raia kukimbia.

Tukio hilo limeripotiwa kufanyika katika eneo la al-Mawasi si mbali na mpaka na Misri.

Vyombo vya Israel vimeripoti kuwa roketi moja lilishambulia eneo la kuegesha magari, lakini hakuna vifo vilivyoripotiwa.

Hamas, jeshi la Israel wapambana kusini mwa Gaza

Mara kwa mara jeshi la Israel limewatuhumu wanamgambo wa Hamas kwa kuwatumia raia wa Gaza kama ngao. Madai ambayo Hamas inakanusha. Eylon Levy, amabye ni msemaji wa serikali ya Israel na amesema:

 ''Huku Israel ikiondoa miundombinu ya kigaidi ya Hamas iliyotengenezwa katika maeneo ya kiraia, Hamas imehamia kuanzisha mashambulizi dhidi ya watu wa Israel kutoka ndani ya eneo lililotengwa la kibinadamu.''

Haya yanajiri wakati mapigano yakipamba moto Alhamisi katika mpaka wa Israel na Lebanon.

Kilio cha Waandishi Habari huko Gaza

03:08

This browser does not support the video element.

Mapigano yapamba moto katika mpaka wa Israel na Lebanon

Ndege za kivita za Israel zimeshambulia maeneo ya ndani ya Lebanon, baada ya makombora kurushwa na vuguvugu la Hezbollah la Lebanon linaloungwa mkono na Iran kuvilenga vituo vya Israel.

Ndege za kivita za Israel zilijibu mashambulizi hayo kwa kulishambulia eneo la Kounine kusini mashariki mwa Lebanon. Jeshi la Israel limethibitisha kufanya mashambulizi dhidi ya kile walichokitaja kuwa maeneo ya magaidi wa Hezbollah ndani ya Lebanon.

Kulingana na afisa wa usalama wa Lebanon, mashambulizi hayo yalipenya ndani kabisa upande wa taifa lao, na kusababisha hofu miongoni mwa Walebnon wanaoishi kwenye vijiji vya kusini mwa nchi hiyo.

Ameongeza kuwa mashambulio ya Israel yamepiga pia miji ya Alma al-Shaab, Dhaira na Wadi al-Saluki na viunga vyake. Hakukuwa na taarifa yoyote ya moja kwa moja kuhusu vifo au majeruhi.

Tangu kuanza kwa vita vya Gaza baada ya shambulizi baya la kushtukiza la Hamas kusini mwa Israeli mnamo Oktoba 7, kumekuwa na makabiliano ya mara kwa mara kati ya Jeshi la Israel na makundi ya wapiganaji katika mpaka wa Israel na Lebanon.

Israel, Marekani na Umoja wa Ulaya miongoni mwa nchi nyingine zimeliorodhesha Hamas kuwa kundi la kigaidi.

Makabiliano hayo yametajwa kuwa mabaya zaidi katika mpaka wa Lebanon na Israel tangu vita vya pili vya Lebanon mwaka 2006.

Msafara mwingine wa malori ya misaada waingia Gaza

01:57

This browser does not support the video element.

Hilal Nyekundu: Maafisa wetu 280 wameuawa tangu Oktoba 7

Wakati hayo yakijiri, shirika la Hilal Nyekundu la Mamlaka ya Palestina, limesema jumla ya maafisa wake 280 wameuawa Gaza tangu vita vilipoanza Oktoba 7.

Aidha, waziri wa afya ya Mamlaka ya palestina inayotawala Ukingo wa Magharibi, amesema wafanyakazi 30 wa shirika hilo la misaada pia wanashikiliwa.

Kulingana na taarifa ya Hilal Nyekundu iliyochapisha kwenye ukurasa wake wa Facebook, kuna ukosefu wa mafuta.

Hapo jana katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa AntonioGuterres alirelejea ibara ya 99 ya katiba ya Umoja huo ili kulitahadharisha Baraza la Usalama la umoja huo juu ya maafa makubwa yanayoweza kuwakumba binadamu.

Kutumiwa kwa ibara hiyo ni hatua ya nadra. Juu ya hatua hiyo waziri wa mambo ya nje wa Israel Eli Cohen ameukosoa vikali uongozi wa Guterres kwenye Umoja wa Mataifa na amesema unatishia amani ya dunia.

Vyanzo: DPAE, APTN

Ruka sehemu inayofuata Gundua zaidi