1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vita vya Israel-Hamas: Israel yaua mateka wake kimakosa

16 Desemba 2023

Jeshi la Israel IDF, limekiri kuwa asakri wake waliwaua kimakosa mateka watatu huko Gaza,licha ya kubeba fimbo ikiwa na bendera nyeupe kama ishara ya amani. IDF imesema askari walioua mateka hao walikiuka kanuni za vita.

Israel, Tel Aviv | Maandamano ya kutaka kuwachiwa kwa mateka wanaoshikiliwa Gaza.
Jeshi la Israel, IDF, limesema askari wake waliwaua kimakosa mateka watatu waliokuwa wanashikiliwa Gaza.Picha: Maja Hitij/Getty Images

Mateka watatu wa Israel waliouawa kimakosa na vikosi vya jeshi la Israel, IDF, katika Ukanda wa Gaza walikuwa wamebeba fimbo iliyofungiwa kitambaa cheusi waakti wa tukio hilo, amesema msemaji wa jeshi la Israel, kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters, shirika la habari la Uhispania EFE na vyombo vya habari Israel.

Tukio hilo lilitokea katika eneo la mapigano makali ambako wapiganaji wa Hamas wanaendesha operesheni zao katika nguo za kiraia na kutumia mbinu za ulaghai, alisema. Mateka hao walikuwa na umari wa miaka 25 hadi 28.

Mwanajeshi aliewapiga risasi mateka hao aliamini wanaume hao walikuwa wanaelekea kwake katika jaribio la Hamas kawaingiza wanajeshi wa IDF mtegoni, alisema afisa wa IDF.

Picha ya Alon Shamriz ikionekana katika uwanja wa mateka, Desemba 16, 2023 katika eneo la Kirya, mjini Tel Aviv, Israel. Shamriz na mateka wengine, Yotam Haim na Samer Talalka wameripotiwa kuuawa na askari wa IDF wakiwadhania ni Hamas.Picha: Maja Hitij/Getty Images

Afisa huyo alisema pia kwamba wanajeshi walikuta karatasi yenye maandishi ya SOS katika jengo la karibu.

Soma pia:Hali ya kibinadamu kusini mwa Gaza inakaribia kuwa 'mbaya zaidi' 

Wote walikuwa hawana shati, na mmoja alikuwa amebeba bendera nyeupe ya kutengeneza. Mwanajeshi huyo alifyatua risasi mara moja na kupiga kelele za "magaidi" ili kuwashtua wanajeshi wengine, liliripoti gazeti la Times of Israel.

Kulingana na vyombo vya habari vya Israel, uchunguzi huo ulihitimisha kwamba mwanajeshi aliuwa mateka wawili, huku wa tatu akijeruhiwa na kurejea katika jengo, akiomba msaada kwa Kiebrania. Hapo ndipo kamanda wa bataliani alipoamuru kusitisha ufyatuaji risasi.

Baadae mateka wa tatu alitoka nje, na kupigwa risasi na mwanajeshi mwingine.

"Hili lilikuwa kinyume na sheria zetu za mapambano," Reuters ilimnukuu afisa huyo akisema. Alisema wanajeshi wote wawili waliofyatua risasi na kuwauwa mateka watatu, walifanya hivyo kwa kuvunja protokali.

Kuuawa kwa mateka kunaweza kuongeza shinikizo kwa serikali ya Israel kufanya makubaliano na Hamas.Picha: Yahel Gazit/Middle East Images//abaca/picture alliance

Mamia waandamana Tel Aviv kupinga mauaji hayo

Mamia ya watu waliingia barabarani mjini Tel Aviv kupinga vifo mateka watatu waliouawa kimakosa na wanajeshi wa Israel huko Gaza, kulingana na ripoti za vyombo vya habari.

Ripoti za vyombo vya habari vya ndani na picha kwenye televisheni zilionyesha waandamanaji wakifunga barabara kuu katikati mwa jiji, wakiitaka serikali kuchukua hatua za haraka kuhakikisha kuwa mateka wengine wanaachiliwa.

Soma pia:Gaza ni 'jehanamu ya dunia' - Lazzarini 

"Muda unayoyoma! Warudisheni nyumbani sasa!" umati ulisikika ukiimba, kulingana na ripoti ya The Times of Israel. "Hakuna ushindi hadi kila mateka wa mwisho aachiliwe!" ilisikika pia.

Waandamanaji hao walibeba mabango yenye picha za mateka hao walipokuwa wakiandamana kuelekea makao makuu ya jeshi la Israel, shirika la habari la DPA liliripoti.

Israel na Hamas wameanza tena mapigano

00:56

This browser does not support the video element.

Baadhi ya waandamanaji waliikosoa serikali ya Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu kwa kutofanya vya kutosha kuwaokoa mateka hao. Kadhaa walishinikiza makubaliano mengine ya kuwachiliwa mateka, kama yalivyotekelezwa mwishoni mwa Novemba kama sehemu ya usitishaji vita wa muda mfupi.

Soma pia:Waislamu wajihisi hawako salama UIaya 

Kati ya mateka 240 waliochukuliwa na Hamas wakati wa mashambulizi yake ya Oktoba 7 kusini mwa Israel, 110 waliachiliwa kama sehemu ya mpango wa kusitisha mapigano, pamoja na raia kadhaa wa wenye asili ya Urusi na Israeli na raia wa Thailand na Mfilipino waliachiliwa huru katika makubaliano tofauti.

Israel, Marekani, Ujerumani, Umoja wa Ulaya na serikali nyingine huitaja Hamas kuwa shirika la kigaidi.