1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
FilamuUjerumani

Vita vya Israel-Hamas vyazua mvutano tamasha la Berlinale

20 Februari 2024

Tamasha la kimataifa la filamu la Berlin siyo geni tena kwa siasa. Mzozo wa Mashariki ya Kati ulitazamiwa kusababisha mijadala na maandamano katika tamasha la mwaka huu.

Berlinale | Filamu | No Other Land
Picha mnto kutoka filamu ya 'No Other Land,' iliyoongozwa na kundi la Wapalestina na Waisraeli na kuonyeshwa kwenye Tamasha la Kimataifa la Filamu la Berlin.Picha: Berlinale

Berlinale inajulikana kama tamasha la filamu ambalo linashughulikia masuala ya kisiasa na kutetea maadili ya kibinadamu. Mijadala na maandamano yanayohusu vita vya Israel na Hamas bila shaka yalitarajiwa kuwa sehemu ya tamasha la mwaka huu. Wakati mabango machache yaliokuwa na ujumbe wa "Uhuru wa Gaza " yalionekana kwenye zulia jekundu, sherehe ya ufunguzi mnamo Februari 15 ilifanyika bila usumbufu.

Kisha siku ya Jumapili, bila kutarajia, wafuasi wapato 50 wanaoiunga mkono Palestina walifanya maandamano katika Soko la Filamu la Ulaya, kulingana na ripoti za mtandao wa Deadline.com. Soko la filamu lina uhusiano wa karibu na tamasha hilo, lakini tofauti na maonyesho mengi ya kwanza ya Tamasha la Filamu la Berlin, jukwaa hilo la biashara linahusisha wataalamu wa tasnia ya filamu pekee na kwa hivyo halionekani kwa umma.

Wafanyakazi wa Berlinale watoa wito wa tamko zito

Ukosoaji pia ulitoka ndani ya waandaji wa tamasha hilo. Barua ya wazi, ambayo kwa sasa imetiwa saini na mawakala 60 wa Berlinale - ikiwa ni pamoja na wasimamizi wa sehemu mbalimbali za tamasha - inatoa wito kwa tamasha hilo kuimarisha taarifa yake rasmi juu ya mgogoro wa sasa wa kibinadamu huko Gaza.

Walipowasilisha programu yao, wasimamizi wawili wa Berlinale, Mariette Rissenbeek na Carlo Chatrian, walisisitiza kwamba huruma yao inaenda kwa waathiriwa wote wa machafuko katika kanda ya Mashariki ya Kati, na kwamba wanataka "mateso ya kila mtu yatambuliwe na kwa mpango wetu kufungua  mitazamo tofauti juu ya masuala magumu ya ulimwengu."

Mariette Rissenbeek na Carlo Chatrian pia walielezea wasiwasi wao juu ya kuongezeka kwa chuki, chuki dhidi ya Uislamu na matamshi ya chuki.Picha: Jens Kalaene/dpa/picture alliance

Kwa waliotia saini, hata hivyo, hii haitoshi: "Tunajiunga na vuguvugu la mshikamano wa kimataifa kutaka kusitishwa mara moja kwa mapigano na kutoa wito wa kuachiliwa kwa mateka wote," inasema barua hiyo. "Wakati dunia inashuhudia upotevu usiofikirika wa maisha ya raia Gaza - ikiwa ni pamoja na waandishi wa habari, wasanii, na wafanyakazi wa filamu - pamoja na uharibifu wa urithi wa kipekee wa kitamaduni, tunahitaji misimamo imara ya kitaasisi."

Vuguvugu la #Strike Germany' laitisha ususiaji

Barua nyingine ya wazi ilitoka kwa washiriki wa kitengo cha 'Forum Expanded', mojawapo ya programu huru zilizoratibiwa za tamasha hilo. Kikiangaliwa kama kitengo cha majaribio zaidi cha Berlinale, Forum Expanded inaakisi filamu kama chombo cha habari kupitia taaluma mbalimbali za kisanii.

Soma pia: Yanayojiri Tamasha la Kimataifa la Filamu la Berlin 2024

Watia saini zaidi ya 100 wa barua hii walionyesha kuunga mkono wenzao wanne ambao waliondoa kazi zao kwenye uteuzi kabla ya hafla hiyo. Wasanii hawa wanne walitaja kwenye Instagram mshikamano wao na vuguvugu la "Strike Germany", ambalo linatoa wito wa kususia taasisi za kitamaduni zinazofadhiliwa na serikali nchini Ujerumani, kupinga kusita kwa nchi hiyo kuunga mkono usitishaji wa mapigano.

Kutokana na historia yake ya unazi, Ujerumani inaliona kuwa ni jukumu lake la kihistoria kuiunga mkono Israel. Wakati huo huo, watengenezaji filamu wa Israel waliopo kwenye tamasha hilo hawasiti kuikosoa serikali ya nchi yao.

Filamu ya kuchekesha ya Israel yaigiza ongezeko la ufashisti

Muongozaji mashuhuri wa Israel Amos Gitai alizindua filamu yake mpya ya makala "Shikun" katika ukumbi wa Berlinale." Filamu hiyo yenye mwelekeo wa kisiasa inatokana na tamthilia ya Eugene Ionesco ya 1959 ya "Rhinoceros," ambayo olikuwa hekaya iliyotoa maoni juu ya kuongezeka kwa ghafla kwa ufashisti kabla ya Vita vya Pili vya Dunia.

Gitai alibuni mradi wa filamu hiyo huku kukiwa na vuguvugu kubwa la maandamano dhidi ya marekebisho tata ya mfumo wa mahaka yalioshinikizwa na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu, ambayo wapinzani wanayaona kama mashambulizi dhidi ya demokrasia ya nchi hiyo.

Tukio kutoka filamu ya "Shikum" likimuonyesha Bahira Ablassi (alievyaa nyeusi) na Iren Jacob.Picha: Agav Films

"Shikun" (ambayo ina maana ya "makazi ya kijamii" katika Kiebrania) huleta pamoja mfululizo wa vijiti vyote vilivyowekwa katika jumba moja la ukiwa. Matukio yanayowahusisha Waisraeli na Wapalestina, pamoja na Waukraine na wageni wengine, yanaonyeshwa katika vyumba tofauti vya jengo hilo.

Gitai huwapa changamoto watazamaji wake kwa muundo wa masimulizi usio wa kawaida, akieleza katika mahojiano ya mezani kwamba amechoshwa na ulinganifu wa aina ya usimulizi wa hadithi unaotawala majukwaa ya uoneshaji filamu.

Filamu hiyo pia inaunganisha nukuu kutoka kwa baadhi ya wanafikra wakubwa duniani, kuanzia Umberto Eco hadi Robert Musil, pamoja na sehemu ya kitabu cha mwandishi wa habari wa Israel Amira Hass, kiitwacho "'Nilikuwa Nafuata tu Amri': Utawaambia Nini Watoto Wako? ", ambacho aliwaandikia Waisraeli wenzake ili kuongeza ufahamu wao kuhusu masaibu ya Wagaza.

(Hass, binti wa waathirika wa mauaji ya Holocaust, alikuwa miongoni mwa wakosoaji wa awali wa msimamo wa Ujerumani kwa Israel baada ya mashambulizi ya Oktoba 7, akichapisha chini ya siku 10 baada ya mshtuko huo, makala ya maoni katika gazeti la Israel la Haaretz yenye kichwa cha "Ujerumani, Umesaliti Wajibu wako kwa Muda Mrefu").

Filamu ya Gitai inamalizia kwa kunukuu shairi la "Fikiria Wengine," maneno ya huruma yaliyoandikwa na mshairi wa Kipalestina Mahmoud Darwish (1941-2008).

Amos Gitai anamuona Netanyahu kama kitisho kwa Israel

Ingawa filamu hiyo itaonekana kama fumbo kwa watazamaji ambao hawafahamu marejeleo haya yote, Gitai anatumia maneno yaliyo wazi sana kueleza maoni yake kuhusu serikali ya sasa ya Israel katika mahojiano ya mezani na waandishi wa habari kwenye tamasha la Berlinale.

Mtengenezaji filamu wa Kiisrael Amos GitaiPicha: Ottavia Da Re/Sintesi/Photoshot/picture alliance

Baada ya kusisitiza kwamba mashambulizi ya kikatili ya kigaidi ya Hamas hayawezi kuhalalishwa kwa vyovyote vile, mkosoaji huyo wa itikadi kali anasema kwamba nchi yake ni "mateka wa muungano wa mrengo wa kulia wa Netanyahu."

Gitai anamwona Netanyahu kama "mdanganyifu wa ngazi ya juu," na anahisi kwamba waziri Mkuu huyo "anaweza kuiangamiza Israel," aliiambia DW.

"Kwa kuwa hana vikwazo vyovyote vya kimaadili, aliiweka pamjoja sehemu mbaya zaidi za jamii ya Israeli: watu wenye msimamo mkali wa kizalendo, wabaguzi wa rangi, wachochezi wenye msimamo mkali, watetezi wa itikadi kali za Kiorthodoksi ambao ni dhidi ya wanawake, dhidi ya LGBT. Hivyo yeye ni sehemu muhimu ya msiba huu."

Wito kwa Ujerumani kuchukua msimamo imara zaidi wa kimaadili

Filamu nyingine kati ya zile zinazotoa maoni kuhusu mzozo wa Mashariki ya Kati katika tamasha la Berlin ni "Hakuna Ardhi Nyingine," iliyoongozwa na kundi la Wapalestina na Waisraeli.

Soma pia: Tamasha la Berlinale lagubikwa na vita vya Gaza

Filamu hiyo inasimulia jinsi Basel Adra, mwanaharakati kijana wa Kipalestina na mmoja wa waongozaji-wenza wa filamu hiyo, amekuwa akipigana kwa miaka mingi dhidi ya kutokomezwa kwa Masafer Yatta, kijiji chake katika eneo la Ukingo wa Magharibi la Israel, ambapo nyumba zinabomolewa na wakaazi kufurushwa. Uwanja wa mafunzo ya kijeshi umepangwa rasmi kujengwa hapo.

Filamu hiyo inaonyesha jinsi alivyoungwa mkono katika juhudi zake na mwandishi wa habari wa Israeli, Yuval Abraham, ambaye aligeuka mwanaharakati baada ya kujifunza lugha ya Kiarabu na kushuhudia dhuluma za ukaliaji wa Israeli.

Waongozaji wa 'Hakuna Ardhi Nyingine' (kutoka kushoto kwenda kulia): Yuval Abraham, Hamdan Ballal, Rachel Szor na Basel AdraPicha: Monika Skolimowska/dpa/picture alliance

Kwa wanaharakati hao, ukandamizaji bila shaka unasababisha athari za vurugu, na ndiyo maana wanahisi nchi za Magharibi zinapaswa kuweka shinikizo zaidi kwa serikali ya Israel kukomesha ukaliaji huo.

"Najua Wajerumani wanajihisi kuwa na hatia kubwa kutokana na kilichotokea katika Vita vya Pili vya Dunia," Abraham aliiambia DW,  na kuongeza kuwa jamaa zake wengi waliuawa wakati wa mauaji ya Holocaust.

"Msitumie hatia hii sasa na kuigeuza silaha na kukataa kuitisha usitishaji wa mapigano; itumieni kutusaidia kufikia suluhu la kisiasa! Itumieni kushinikiza taifa la Israel kukomesha ukaliaji," anasema mtengenezaji huyo wa filamu wa Israel. "Huo ungekuwa kwangu msimamo wa kimaadili zaidi kwa serikali kuchukua."

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW