1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vita vya Israel kwenye Ukanda wa Gaza vyaingia siku ya saba

13 Oktoba 2023

Jeshi la Israel limeushambulia tena Ukanda wa Gaza kutokea angani, huku likitayarisha vikosi vya ardhini na kuapa mzingiro wake dhidi ya eneo hilo kuendelea hadi Hamas itakapowaachilia mateka wote iliowachukuwa Israel.

Israel Angriffe auf Gaza
Picha: Saleh Salem/REUTERS

Hayo yanakuja wakati ziara ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Antony Blinken, sambamba na shehena ya silaha kutoka nchi yake, vikiashiria idhini kwa Israel kuendelea na mashambulizi yake kwenye Ukanda wa Gaza, katika kile kinachoitwa "ulipizaji kisasi" kwa uvamizi uliouwa raia na wanajeshi kadhaa siku ya Jumamosi.

Mashirika ya misaada ya kimataifa yameonya kwamba hali ya kibinaadamu inazidi kuwa mbaya kwenye ukanda huo, ambao hata kabla ya mzingiro wa sasa ulishakuwa taabani kutokana na mzingiro wa kudumu wa Israel.

Soma zaidi: Vita vya Gaza: Blinken afanya mazungumzo na Netanyahu

Tangu Jumatatu (Oktoba 9), Israel imezuwia kabisa ufikishwaji wa bidhaa muhimu na umeme kwa mamilioni ya watu wanaoishi kwenye ukanda huo na imekataa kupitisha chochote kutokea Misri.

"Hakutakuwa na swichi hata moja ya umeme itakayowashwa, wala gari lolote la mafuta litakaloingia hadi mateka wote wa Israel warejeshwe nyumbani." Alisema Waziri wa Nishati Israel Katz kupitia mtandao wa kijamii.

Tuhuma za matumizi ya mabomu ya fosforasi

Shirika la haki za binaadamu la Human Rights Watch (HRW) limeituhumu Israel kwa kutumia mabomu ya fosfarasi kwenye operesheni yake ya kijeshi katika Ukanda wa Gaza na Lebanon, likisema matumizi ya silaha kama hizo yanawaweka raia kwenye hatari ya kuwa na majeraha makubwa na ya muda mrefu.

Roketi likirushwa kutoka Ukanda wa Gaza kuelekea Israel siku ya tarehe 11 Oktoba 2023.Picha: Fatima Shbair/AP/picture alliance

Lilipotakiwa kuzugumzia madai hayo, jeshi la Israel limesema kwa sasa halina taarifa za matumizi ya silaha zenye madini ya fosforasi nyeupe kwenye Ukanda wa Gaza.

Soma zaidi: Scholz: Ujerumani kupiga marufuku shughuli za Hamas

Hata hivyo, jeshi hilo lilikataa kutoa maoni yake juu ya madai ya Human Rights Watch kwa upande wa Lebanon.

HRW inadai kuwa limethibitisha video zilizochukuliwa nchini Lebanon tarehe 10 Oktoba na Gaza tarehe 11 Oktoba zikionesha mabomu ya angani yakipasuka na kutowa fosforasi nyeupe.

Shirika la habari la Reuters halikuweza kuthibitisha ukweli wa madai hayo.

Silaha hizo zimepigwa marufuku duniani kwa kuwa ni silaha zinazounguza na kusababisha majeraha kwa waathirika.

Israel kutuma wanajeshi wa ardhini

Luteni Kanali Richard Hecht, msemaji wa jeshi la Israel, aliwaambia waandishi wa habari siku ya Alkhamis (Oktoba 12) kwamba vikosi vya ardhini vinajitayarisha kuingia kwenye Ukanda wa Gaza muda wowote baada ya viongozi wa kisiasa kukamilisha majadiliano yao.

Kifaru cha Israel kwenye mpaka na Ukanda wa Gaza siku ya tarehe 12 Oktoba 2023.Picha: Ronen Zvulun/REUTERS

Uvamizi wa ardhini dhidi ya Gaza, kipande cha ardhi chenye urefu wa kilomita 40 tu na kinacokaliwa na watu milioni 2.3 chini ya utawala wa kundi Hamas, utasababisha maafa zaidi kwa pande zote mbili, kwani yatakuwa mapigano ya nyumba kwa nyumba. 

Soma zaidi: Mashambulizi Israel, Gaza yaingia siku ya sita

Uvamizi wa Hamas dhidi ya Israel hapo Jumamosi umesababisha vifo vya zaidi ya watu 1,300, wakiwemo wanajeshi 247 - idadi ambayo haijawahi kushuhudiwa nchini Israel kwa miongo kadhaa.

Kwa upande wake, mashambulizi mfululizo ya Israel yameuwa hadi sasa zaidi ya watu 1,530 katika Ukanda wa Gaza, kwa mujibu wa takwimu ya pande zote mbili.

Israel inadai kuwa wapiganaji 1,500 wa Hamas wameuawa ndani ya Israel, na kwamba mamia kati ya wale waliouawa Ukanda wa Gaza ni wananchama wa kundi hilo, ambalo linatambuliwa na mataifa kadhaa ulimwenguni kuwa kundi la kigaidi. 

Pande zote mbili zina idadi kubwa zaidi ya majeruhi, huku Umoja wa Mataifa ukisema walioyakimbia makaazi yao katika Ukanda wa Gaza wamefikia 430,000. 

Chanzo: AP, Reuters
 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW