1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vita vya Mashariki ya Kati: Hamkani si shwari

15 Machi 2026

Mataifa ya Ghuba ya Kiarabu yameripoti mashambulio mapya ya makombora na ndege zisizo na rubani siku ya Jumapili baada ya Iran kutishia kupanua kampeni yake ya kijeshi kwenye kanda hiyo.

Moshi ukifuka kutoka kituo cha kuhifadhi mafuta huko Umoja wa Falme za Kiarabu baada ya kushambuliwa na droni inayoaminika ilirushwa kutoka Iran
Moshi ukifuka kutoka kituo cha kuhifadhi mafuta huko Umoja wa Falme za Kiarabu baada ya kushambuliwa na droni inayoaminika ilirushwa kutoka Iran.Picha: AFP

Siku ya Jumamosi Iran ilitoa onyo kwa watu kutozisogelea bandari tatu kuu za Umoja wa Falme za Kiarabu katika kile kilichotafsiriwa kuwa dhamira ya kutaka kuzishambulia.

Vita hivyo vya Mashariki ya Kati, vimeingia katika wiki yake ya tatu sasa na hakuna ishara ya kupungua makali. 

Israel na Marekani ziliishambulia Iran mnamo Februari 28, zikisema zilikuwa zikishambulia vutuo vya nyuklia na kijeshi na kuuhimiza umma wa Iran kujitokeza kuwapinga viongozi wao.

Tangu wakati huo, Iran imejibu mashambulizi dhidi ya Israel na nchi jirani katika Ghuba ya Uajemi ambazo zinahifadhi kambi za jeshi la Marekani.

Vita hivyo, ambavyo havionyeshi dalili za kumalizika hivi karibuni, vimetatiza usafiri wa anga duniani, na  usafirishaji wa mafuta kutoka eneo hilo hali iliyopelekea kupanda kwa bei ya nishati hiyo kote duniani.

Rais wa Marekani Donald Trump alisema anatumai washirika wake watatuma meli za kivita ili kuulinda mlango wa bahari wa Hormuz.

Hakuna hata nchi moja kati ya zile alizozitolea rai na ambazo zinategemea zaidi mafuta na gesi yanayopita kwenye ujia huo wa bahari, iliyojibu kwa uhakika kwamba itatuma meli za kivita. Baadhi zimesema zinatafakari pendekezo hilo lililotolewa na Marekani.

Iran yazilenga nchi za eneo la Ghuba, mvutano wazidi makali 

Bahrain, Saudi Arabia na Umoja wa Falme za Kiarabu zilitoa hadhari kwa wakaazi wake siku ya Jumapili huku zikisema zinafanya  kazi ya kuzuia makombora kutoka Iran.

Hiyo ni baada ya Tehran kutishia kuzishambulia bandari za Umoja wa Falme za Kiarabu, ikiwa ni mara ya kwanza kufanya hivyo dhidi ya mali isiyo ya Marekani katika nchi jirani.

Awali Iran ilikuwa imeshutumu Marekani kwa kutumia "bandari na maeneo ya maficho" ndani ya Umoja wa  Falme za Kiarabu, UAE, kukishambulia kisiwa chake cha Kharg, kinachotumika kwa zaidi ya asilimia 90 kusafirisha hazina ya mafuta ya Iran kimataifa. Iran hata hivyo haikutoa ushahidi wa madai hayo.

UAE na nchi nyingine za Ghuba ambazo zina kambi za jeshi la Marekani zimekana kuruhusu ardhi yao au anga yao kutumika kwa operesheni za kijeshi dhidi ya Iran.

Tangu kuanza kwa vita hivyo, mashambulizi ya Iran yamesababisha vifo vya takriban raia kumi na wawili kwenye mataifa ya Ghuba, wengi wao wakiwa ni wafanyakazi wahamiaji.

Nchini Iran, Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu imesema zaidi ya watu 1,300 wameuawa hadi sasa.

Uharibifu nchini Iran baada ya mashambulizi ya Marekani na Israel.Picha: IRCS/ZUMA/IMAGO

Wizara ya Afya ya Iran imesema wanawake 223 na watoto 202 ni miongoni mwa waliouawa, kulingana na Mizan, wakala rasmi wa habari wa mahakama.

Nchini Israel, watu 12 wameuawa kwa makombora yaliyofyetuliwa na Iran tangu vita hivyo kuanza na wengine zaidi wamejeruhiwa, wakiwemo watatu siku ya Jumapili.

Wanajeshi wasiopungua 13 wa jeshi la Marekani pia wameuawa tangu vita kuanza; sita kati yao walifariki katika ajali ya ndege nchini Iraq wiki iliyopita.

Wakati huo huo, mzozo wa kibinadamu wa Lebanon unazidi kuongezeka, na zaidi ya watu 820 wameuawa nchini humo, kulingana na Wizara ya Afya.

Imeelezwa pia watu 850,000 wameyakimbia makazi tangu Hezbollah inayoungwa mkono na Iran kuanza kuipiga Israeli na Israeli ilijibu kwa mashambulizi makali ya anga na kutuma wanajeshi wake kusini mwa Lebanon.

 Iran inasema Marekani ilishambulia kutoka UAE

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi.Picha: Jean Marc Ferré/MAXPPP/picture alliance

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi, amesema visiwa viwili vya nchi hiyo, visiwa vya Kharg na Abu Musa vilishambuliwa na Marekani kutoka maeneo mawili ndani ya Umoja wa Falme za Kiarabu ambayo ni Ras Al Khaimah na sehemu nyingine "karibu sana na Dubai."

Alisema hali hiyo ni ya hatari na kuonya kwamba Iran itajibu lakini "itajaribu kuwa makini ili isishambulie eneo lolote linalokaliwa na watu wengi" kwenye taifa hilo.

Kamandi Kuu ya Marekani ilisema haikuwa na majibu kwa madai ya Iran.

Anwar Gargash, mshauri wa kidiplomasia wa rais wa UAE, amepinga madai ya Iran kwamba Marekani ilitumia ardhi ya falme hiyo ya Ghuba au anga kwa mashambulizi yake katika Kisiwa cha Kharg.

Iran imerusha mamia ya makombora na ndege zisizo na rubani kwa majirani wa Ghuba - Bahrain, UAE, Saudi Arabia, Qatar na Oman - wakati wa vita.

Inasema inalenga mali za Marekani, hata kama mashambulizi ya Iran yanaripotiwa katika maeneo ya raia kama vile viwanja vya ndege na vituo vya mafuta. Ingawa ulinzi wao wa anga umezuia zaidi mashambulizi ya Iran, vita hivyo vimesababisha uharibifu mkubwa na kuyumba kwa uchumi wa nchi za Ghuba.

Araghchi pia aliliambia gazeti la Al-Araby al-Jadeed lenye makao yake London siku ya Jumapili kwamba Iran iko tayari kuzingatia pendekezo lolote linalojumuisha "mwisho kamili" wa vita na akasema juhudi za upatanishi zinaendelea kati ya Iran na majirani zake ili kupunguza makabiliano. Hata hivyo hakutoa ishara yoyote juu ikiwa kuna maendeleo yaliyopatikana.

 Trump awataka washirika kupeleka meli za kivita kwenye ujia bahari wa Hormuz

Rais Donald Trump wa Marekani.Picha: Mark Schiefelbein/AP Photo/picture alliance

Wakati wasiwasi wa kimataifa unapoongezeka juu ya bei ya mafuta na vifaa, Trump alisema Jumamosi kwamba anatumai China, Ufaransa, Japan, Korea Kusini, Uingereza na zingine zitatuma meli za kivita kuweka Mlango wa Hormuz "wazi na salama." Haikuwa wazi kama kuna aliyepanga kuitikia rai ya kiongozi huyo wa Marekani.

Uingereza ilijibu kwa kusema ilikuwa inajadiliana na washirika wake juu ya hatua mbalimbali za kuwezesha kufunguliwa kwa Mlango Bahari wa Hormuz.

Mataifa mengi ya Ulaya yanategemea sana uagizaji wa mafuta na gesi kutoka eneo la Ghuba,

Araghchi, katika chapisho la mtandao wa kijamii, aliwataka majirani "kuwafukuza wavamizi wa kigeni" na akaelezea wito wa Trump kama "omba."

Kamandi ya pamoja ya kijeshi ya Iran imesisitiza tishio lake la kushambulia "miundombinu ya mafuta, kiuchumi na nishati" inayohusishwa na Marekani katika eneo hilo ikiwa miundombinu ya mafuta ya Jamhuri ya Kiislamu itaathiriwa.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW