VITA VYA MAU MAU KENYA
22 Februari 2005Uingereza, katika kumbukumbu za kihistoria zinazotia aibu na za propoganda za kivita, ilikuwa ikieneza uvumi kuwa Mau Mau nchini Kenya ni watu wakatili waliokuwa na kiu ya kunywa damu ya watu. Lakini Watawala wake walikuwa mashujaa.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Oxford nchini Uingereza, David Anderson, ambaye amefichua ushahidi mpya unaoonyesha kuwa Waingereza walikuwa wakatili zaidi wakati wa uasi wa Mau Mau anasema, "Kwa mshangao mkubwa bado kuna baadhi ya watu wanaoamini hisia hizi za kibaguzi."
Ukweli wa mambo ni kuwa Mau Mau ilianzishwa mwanzoni mwa miaka ya hamsini miongoni mwa Wakikuyu waliofukuzwa na Wazungu kutoka katika mashamba yao tokea mwanzoni mwa karne ya 19.
Ni watu wachache sana wanaotambua kuwa ni Walowezi wa Kizungu 32 peke yao waliouawa wakati wa vita hivyo vilivyodumu miaka saba. Kwa upande mwingine watu 150,000, waliokuwa wanashukiwa kuwa ni Mau Mau au wanawakumbatia, walitumbukizwa katika kambi za mateso, wengi wao bila ya kufikishwa mahakamani. Waasi wasiopungua 20,000 wameuawa wakati wa mapambano hayo na zaidi ya 1,000 wamenyongwa.
Mhadhiri Anderson anasema, "Kinachoshangaza ni kuona kuwa ulipizaji kisasi uliofanywa na Wazungu nchini Kenya ulikuwa mbaya zaidi na uliowagusa watu wengi kuliko vile ilivyokuwa Malaya, Palestina au hata Cyprus. Kenya ilikuwa maalumu kabisa na ndiyo maana inahitaji uangalifu mkubwa na uchambuzi wa kina."
Mwanzo halisi wa Mau Mau haujulikani. Kuna wanaosema kuwa wamechukua jina hilo kutokana na milima inayopakana na magharibi mwa Bonde la Ufa wakati wengine wanasema kuwa kilikuwa kilio cha Wakikuyu cha vita.
Jambo ambalo ni hakika kabisa ni kuwa uasi uliokuwa unaenea kimya kimya hatimaye ulizuka na kuwa vita vya wazi mwezi wa Oktoba mwaka 1952 wakati Gavana wa kikoloni alipotangaza hali ya hatari na kuomba majeshi zaidi kutoka Uingereza.
Mtu wa kwanza aliyekamatwa alikuwa Mzee Jomo Kenyatta, ambaye miaka kumi baadaye, alikuwa Rais wa kwanza wa Kenya huru.
Kenyatta, kwa makosa, alituhumiwa kuwa Kiongozi wa Mau Mau. Akahukumiwa kifungo cha miaka kumi gerezani na kazi ngumu.
Baadhi ya mbinu zilizokuwa zinatumiwa na Waingereza zinaudhi, zinafahamika na zina fanana. Kwa mfano, sheria mpya za kupambana na Magaidi zilizotangazwa kati ya 1952 na 1960 zimeondoa haki za kiraia za watuhumiwa, zimeruhusu mali zao kunyakuliwa na Watawala wa kikoloni na hukumu ya kifo kupanuliwa pia kwa makosa mengine.
Msingi wa kitabu hicho unatokana na nyaraka zilizopatikana kwa watu ambao majina yao hayakutajwa zinazoitwa "Kesi za Mau Mau" zilizosababisha Wakenya 1,090 kunyongwa kati ya mwaka 1952 na 1959.
Idadi hii ni kubwa kupita kiasi hata mtu akifikiria ule ukatili uliofanywa na Wakoloni wa Kiingereza barani Afrika na katika Mashariki ya Kati.
Jambo la kushangaza zaidi ni kuona kuwa unyongaji umefanywa wakati ambapo Bunge la Uingereza limekuwa likifikiria uwezekano wa kuondoa sheria za kunyonga watu nyumbani.
Mpaka hivi sasa hakuna hata Afisa mmoja wa Kiingereza, wa jeshi au raia aliyefanyiwa uchunguzi au kufikishwa Mahakamani kujibu mashtaka ya mauaji ya kiholela wakati wa kukandamiza Mau Mau.
Bw. Anderson, ambaye ni Mhadhiri wa masuala ya Kiafrika katika Chuo Kikuu cha Oxford nchini Uingereza, amesema, "Serikali ya Uingereza inapaswa kukiri kile kilichotokea na kuomba radhi."
Halmashauri ya Kupigania Haki za Binaadamu nchini Kenya kwa wakati huu inaunga mkono kampeni ya kutaka kuwafikisha Mahakamani baadhi ya watu waliofanya vitendo viouvu wakati wa Mau Mau.
Ingawaje dhana hii kimsingi inaungwa mkono na Wakenya wengi lakini ina matatizo yake.
Mhadhiri Anderson amesema, "Wazo la kuwalipa fidia Wahanga wa Mau Mau walioteswa na Waingereza linaweza kutekelezwa iwapo litafikishwa mbele ya Mahakama ya Kimataifa. Lakini pia liwajumuishe Wakenya elfu kadhaa walioangukia mikononi mwa Mau Mau."