1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaAsia

Vita vya miaka 10 vyauwa watu wapatao 400,000 Syria

14 Machi 2021

Idadi ya watu waliokufa kutokana na vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Syria imekaribia laki nne tangu vilipoanza muongo mmoja uliopita, na hadi sasa hakuna ishara ya lini vitamalizika.

BG Photos and testimonies from Syrian photographers | Abood Hamam
Picha: Abood Hamam/OCHA

Kwa mujibu wa Shirika la Kufuatilia Haki za Binaadamu la Syria lenye makao yake nchini Uingereza, idadi kamili ya watu waliopoteza maisha yao kwenye vita hivyo ni 388,652 kufikia tarehe 13 Machi 2021, mwaka wa kumi kamili tangu mapigano hayo yaanze.

Wengi katika hao waliopoteza maisha ni raia wa kawaida, ambao ni 117,368 na ambapo zaidi ya 22,000 kati yao ni watoto wadogo. 

Mashambulizi yaliyofanywa na vikosi vya serikali ya Syria na makundi ya wanamgambo yanayoiunga mkono ndiyo yaliyoangamiza maisha ya watu wengi zaidi, kwa mujibu wa shirika hilo la haki za binaadamu ambalo linategemea vyanzo vya ndani ya Syria kwenye ripoti zake.

Idadi ya mwisho kabisa ya vifo iliyotolewa na shirika hilo ilikuwa mwezi Disemba 2020, ambapo wakati huo vifo vilikuwa 387,000, ingawa mkuu wa shirika hilo, Rami Abdel-Rahman, alisema mwaka huo ndio uliokuwa na idadi ya chini kabisa ya vifo tangu vita vianze amavyo havikuzidi 10,000.

Mapigano yapunguwa

Mtu na nduguye wakilia kwa uchungu baada ya mama yao na kaka yao kuuawa kwenye mashambulizi ya angan mjini Idlib.Picha: Ghaith Alsayed/OCHA

Mapigano yalipunguwa tangu mwaka 2020 kufuatia mkataba wa kusitisha vita kwenye eneo kaskazini magharibi mwa Syria na pia kutokana na makini kuelekezwa kwenye janga la virusi vya corona.

Shirika hilo pia limesajili kwa uchache vifo 16,000 kwenye magereza na mahabusu ya serikali tangu mzozo ulipoanza mwaka 2011, baada ya ukandamizaji wa kikatili uliofanywa na serikali dhidi ya maandamano ya amani.

Hata hivyo, lilisema idadi kamili ya vifo inaweza kuwa kubwa zaidi kwa sababu hisabu yake haikujumuisha watu wengine 88,000 wanaoaminika kufaa kutokana na mateso wakiwa kwenye jela za serikali.

Mbali ya wale waliotambulika kufa na wale waliogeuka wakimbizi, shirika hilo linasema wengine 200,000 hawajulikani walipo hadi sasa.

Assad arejesha udhibiti 

Vikosi vya serikali ya Rais Bashar Al Assad wa Syria (kulia) anaonekana sasa kushinda vita kwa kurejesha maeneo kadhaa yaliyokuwa yametekwa na waasi.Picha: picture-alliance/dpa/E. Samarin

Kwa sasa, serikali ya Rais Bashar al-Assad inadhibiti zaidi ya asilimia 60 ya nchi baada ya mafanikio makubwa ya kijeshi yaliyochangiwa na msaada wa kijeshi kutoka Urusi na Iran dhidi ya wanamgambo wa makundi ya siasa kali na waasi wa kawaida ulioanza mwaka 2015.

Miongoni mwa maeneo ambayo bado hayajarejea mikononi mwa serikali ni pamoja na ngome ya mwisho kabisa ya waasi ya Idlib iliyo kaskazini magharibi, maeneo yanayoshikiliwa na Uturuki kwenye mpaka wa kaskazini, na yale ya kaskazini mashariki ambayo yanashikiliwa na waasi wa Kikurdi wanaoungwa mkono na Marekani. 

Vita hivi vya miaka kumi vimewalazimisha zaidi ya nusu ya raia wa nchi hiyo kuyakimbia makaazi yao na kusaka hifadhi kwengineko duniani, wengi wao kwenye mataifa jirani, hasa Uturuki.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW