Vita vya ndege zisizo rubani za Marekani vyaikasirisha Pakistan
7 Juni 2012Msimamo wa Pakistan ni kwamba mashambulizi ya ndege zisizokuwa na watu za jeshi la Marekani ndani ya mipaka yake ni kinyume na sheria. Lakini kutokana na yale yanayoonekana kuwa mafanikio ya operesheni hiyo, hakuna dalili kwamba Marekani iko tayari kuachana na mpango wake huo. Inafahamika kuwa chini ya Rais Obama, matumizi ya ndege hizo yameongezeka sana. Kisheria, Rais wa Marekani ndiye mwenye kauli ya mwisho juu ya mashambulizi ya angani.
“Mashambulizi haya yanajaribu kuwalenga wale watu tu wanaotambuliwa kwenye orodha yetu kama magaidi, kwa sababu wanajaribu kuidhuru Marekani. Mashambulizi haya yamelenga maeneo ya ndani ya Pakistan, ambako wapiganaji wa al-Qaida wanajificha, na ambako kama tukiwafuata huko kwa njia nyengine, utakuwa ni uingiliaji mkubwa zaidi wa kijeshi.” Amesema Rais Obama.
Ndani ya kipindi cha wiki mbili tu zilizopita, mashambulizi hayo yameshafanyika mara nane katika maeneo hayo ambayo serikali ya Pakistan haina udhibiti nayo. Kwa ujumla, tangu mwanzoni mwa mwaka huu, tayari yameshafikia ishirini. Lakini kiwango kamili cha madhara yake ni shida kukithibitisha kupitia vyanzo huru vya habari.
Taarifa za uhakika hazipatikani
Ndege hizo zinazoendeshwa bila rubani na zikitumia kiwango cha juu cha teknolojia, zinarusha makombora yake katika maeneo ambayo hayafikiki kwenye mpaka wa Pakistan na Afghanistan. Na Waislamu wenye siasa kali, Jeshi la Pakistan na hata maafisa wa usalama wa taifa, wanajaribu kuwazuia waandishi wa habari kuchukua picha za mwahala humo.
Taarifa nyingi kuhusiana na mashambulizi ya ndege hizo hutoka kwa wapasha habari wasiotajwa majina kutoka mashirika ya kijasusi, serikalini na viongozi wa makabila. Kutenganisha ukweli na propaganda kwenye mazingira kama haya inakuwa ni vigumu sana, ama haiwezekani kabisa, kwa sababu mara nyingi maslahi ya wapasha habari ndiyo hutawala habari yenyewe.
Lakini ni jambo lisilobishaniwa kuwa viongozi wa kisiasa na kijeshi wa Pakistan wanakabiliwa na shinikizo kali la raia wao ambao wanataka mashambulizi hayo ya ndege zisizokuwa na abiria yakome mara moja. Waziri wa Mambo ya Kigeni, Hina Rabbani Khan, anasema kwamba wao wanafikiria maslahi ya sehemu kubwa ya jamii ya Pakistan.
“Kwa maoni yetu, utumiaji wa ndege hizi zisizokuwa na rubani ni haramu na unakatazwa kabisa na sheria zote. Unapingana na sheria za kimataifa. Zaidi ni kuwa ndege hizo zinaweza kukinzana na vita dhidi ya Uislamu wa siasa kali na ugaidi. Hata kama inatokea wakati wa mashambulizi, mtu mmoja aliyekusudiwa anashambuliwa, bado huwaua watu wengine watano au sita ambao hawakukusudiwa.” Anasema Khan.
Chuki dhidi ya Marekani zinaongezeka nchini Pakistan. Na vita vinavyotumia ndege zisizo rubani vinazidi kuliongeza pengo hilo. Marekani inataka kuondosha wanajeshi wake kutoka eneo hilo, na kupambana na makundi ya kigaidi kama al-Qaida hapo baadaye kwa kutumia teknolojia ya kijeshi ya hali ya juu.
Huu ni mwaka wa kampeni za uchaguzi kwa Marekani, lakini ukweli mmoja uko wazi: hakuna upande unaoshinda vita hivi .
Mwandishi: Sandra Petermann/DW
Tafsiri: Mohammed Khelef
Mhariri: Mohamed Abdulrahman