Vita vya nne bora na kushushwa daraja vyanoga Bundesliga
2 Mei 2022Tunaanza na Bundesliga ambapo Eintracht Frankfurt wameuangazia kikamilifu mchuano wao wa nusu fainali ya Europa League dhidi ya West Ham lakini kocha Oliver Glasner ameahidi kuwa vijana wake watakuwa na akili ya kiushindani na kikosi kizuri kitakachocheza leo usiku dhidi ya Bayer Leverkusen.
Frankfurt watawaalika West Ham katika mkondo wa pili Alhamisi, na wakishinda kombe hilo la Europa watapata tiketi ya kucheza Champions League msimu ujao. Frankfurt walishinda 2-1 mjini London wiki iliyopita.
Leverkusen wako na pointi sawa na Freiburg (55) na moja mbele ya RB Leipzig katika kile kinachoonekana kuwa ni mapambano ya farasi watatu ya kuwania nafasi za Champions League. Cologne na Union Berlin wana nafasi kimahesabu. Freiburg wamecheza mechi moja zaidi ambayo walipata ushindi wa 4-3 dhidi ya Hoffenheim.
Leipzig wana mkondo mwingine wa kujikatia tiketi ya Champions League kwa sababu wako kwenye nusu fainali nyingine ya Europa League dhidi ya Rangers, ambapo wanaelekea Glasgow wakiwa kifua mbele 1-0.
Leo hata hivyo watacheza dhidi ya Borussia Moenchengladbach na watataka kushinda ili kutafuta nne bora.
Kwingineko, mabingwa wa Bundesliga Bayern Munich wamekosolewa kwa ziara ya siku mbili waliyofanya mwishoni mwa wiki kwenda eneo la mapumziko ya kitalii la Ibiza nchini Uhispania mara tu baada ya kipigo cha 3-1 dhidi ya Mainz.
Wiki moja baada ya kutawazwa mabingwa wa 10 mfululizo wa Bundesliga, Bayern walionyesha mchezo mbaya dhidi ya Mainz. Nguli wa zamani wa Bayern Lathar Mattheus amesema ziara hiyo ya kisiwa cha Ibira haikustahili hasa baada ya mchezo kama ule akisema unatoa picha mbaya kwa kikosi kizima.
Mkurugenzi wa spoti wa Bayern Hasan Salihamidzic amesema safari hiyo ni muhimu kwa kikosi kutafakari na kurejesha mshikamano.
afp