1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vita vya Syria vyaingia mwaka wake wa nane

Sylvia Mwehozi
15 Machi 2018

Mgogoro wa vita vya Syria umeingia mwaka wake wa nane hii leo wakati nchi hiyo ikioonekana kugawanywa na mataifa yenye nguvu duniani.

Syrien Operation Olivenzweig Afrin
Picha: picture-alliance /AA/H. Al Homsi

Uturuki imeuzingira mkoa wa kaskazini wa kikurdi wa Afrin, huku majeshi ya serikali yanayoungwa mkono na Urusi yakishambulia eneo linalodhibitiwa na waasi karibu na mji mkuu wa Damascus. 

Umwagaji damu, ambao umeharibu maeneo mengi ya Syria tangu vita hiyo ianze tarehe kama ya leo mwaka 2011, wakati serikali ya rais Bashar Al-Assad ilipokabiliana na maandamano ya amani, umegeuka kuwa moja ya mgogoro migumu kabisa duniani. Katika mapigano ya karibuni, majeshi yanayoungwa mkono na Uturuki yameanzisha mashambulizi ya mabomu kwenye mkoa wa Afrin karibu na mji mkuu wa jimbo hilo, katika mashambulizi ambayo yanaweza kubadili ramani ya kaskazini mwa Syria.

Rais Bashar al-Assad, Vladmir Putin na waziri wa ulinzi wa Urusi Sergei ShoiguPicha: picture alliance/ dpa/TASS/M. Klimentyev

Maendeleo hayo yalikuja wakati vikosi vya serikali na mshirika wake Moscow, kufanikiwa kuingia katika mji muhimu kwenye eneo linalodhibiwa na waasi huko Ghouta mashariki usiku wa Jumatano, na kusonga zaidi kwenye eneo la mwisho la upinzani nje ya Damascus.

Jumla ya raia 350,000 wameuawa tangu vita ianze

Zaidi ya raia 1,220, theluthi tano wakiwa watoto wameuawa katika eneo hilo la waasi tangu vikosi vya serikali vilipozindua mashambulizi ya angani na ardhini mnamo februari 18.

Jitihada za kimataifa mara kadhaa zimeshindwa kumaliza moja ya vita mbaya katika karne, ambapo watu zaidi ya 350,000 wameuawa tangu kuanza kwake na nusu ya wakazi wa kabla ya vita karibu milioni 20 hawana makazi. Mmoja ya wakazi wa Syria aliyeko katika makambi anasema."Watu wetu walitoka kudai uhuru na mageuzi, wako wapi sasa? uhuru uko wapi? ni nchi zote tu zinapigana zenyewe ndani ya ardhi yetu. Tumekuwa uwanja wa majaribio, ni watu wangapi watauawa na maroketi na makombora? Mataifa yenye nguvu yanapambana yenyewe kwenye nchi yetu."

Wakati miezi michache ya karibuni ilishuhudia anguko la kundi la Dola la Kiislamu IS, lililotangazwa mwaka 2014 katika baadhi ya maeneo ya Syria na Iraq, mataifa yaliyo na nguvu tangu wakati huo yamefikiria kuondoa ongezeko la ushawishi wake katika ukanda huo.

Raia wakiondoka Afrin baada ya majeshi ya Uturuki kukitwaa kijiji cha KhaldiehPicha: Reuters/K. Ashawi

Wakurdi wanaoungwa mkono na Marekani wandhibiti eneo lenye utajiri wa mafuta kaskazini mashariki mwa syria ambayo ni sawa na asilimia 30 ya nchi na waasi wa Kiarabu wanaoungwa mkono na Uturuki wakikata theluthi tatu kaskazini magharibi. Ankara ambayo ilianzisha mashambulizi makali ya angani na ardhini dhidi ya mkoa unaokaliwa kwa wingi na Wakurdi wa Afrin, iliapa siku ya jumatano kwamba ukombozi wa mji mkubwa utakuwa umekamilika ifikapo jioni. "Jumla ya magaidi 3444 wamedhibitiwa hadi sasa. Hatuwalengi raia kama yalivyofanya mataifa ya magharibi siku za nyuma. Kama Uturuki imelenga kuwaua raia, Afrin ingekuwa tayari imedhibitiwa. raia wanaondolewa katika magari na kupitia ukanda maalumu. Magaidi wanawatumia raia kama ngao katika mkoa huo," alisema rais wa Uturuki Tayyip Erdogan. 

Shirika la uangalizi wa haki za binadamu la Syria limesema kwamba majeshi yanayoongozwa na uturuki yanadhibiti asilimia 70 ya mkoa huo wa kikurdi baada ya kuvikamata vijiji kadhaa.

Mashambulizi ya Ghouta Mashariki

Nje kidogo ya mji wa Damscus, mgogoro mwingine wa kibinadamu unazidi kushika kasi Ghouta mashariki. Umoja wa Mataifa umetoa wito wa huduma ya dharura ya matibabu kwa zaidi ya watu 1000 ambao wana uhitaji wa haraka wa huduma za afya nje ya maeneo yaliyozingirwa.

Kamati ya kimataifa ya Msalaba Mwekundu  ICRC nchini Syria imesema msafara wa malori 25 ya usaidizi

umeingia kwenye eneo la Ghouta mashariki hii leo Alhamisi. Nalo shirika la Hilal nyekundu la kiarabu la Syria limesema karibu tani 340 za misaada ya chakula zimeingia Ghouta mashariki kwa ushirikiano na ICRC na Umoja wa Mataifa.

Baraza la usalama la Umoja wa mataifa lilipitisha mpango wa siku 30 wa kusitisha mapigano mwezi uliopita ili kuruhusu usambazaji wa misaada na kuondolewa kwa wagonjwa.

Mwandishi: Sylvia Mwehozi/AFP/Reuters

Mhariri: Daniel Gakuba

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW