Ukraine yakumbwa na shambulizi baya la mtandaoni
16 Desemba 2023Kampuni kubwa zaidi ya simu nchini Ukraine ilikumbwa shambulio kubwa la mtandao wiki hii, Uingereza imesema katika taarifa yake ya hivi karibuni ya kijasusi kuhusu mzozo huo.
Huduma za Kyivstar, ambayo inatoa huduma za mtanadao na simu za nyumbani kwa zaidi ya nusu ya wakaazi wa Ukraine ziliathirika kwa takriban saa 48 kuanzia Jumanne, taarifa hiyo fupi iliyochapishwa kwenye mtandao wa X, zamani Twitter, ilisema.
Shambulio hilo liliwaacha watumiaji bila signo za simu za mkononi au uwezo wa kutumia mtandao, Wizara ya Ulinzi ya Uingereza, MOD, iliongeza.
Huduma nyingine zilizoathiriwa na shambulio hilo ni mashine za kutolea fedha za za benki, ATM, ving'ora vya kutahdharisha juu ya mashambulizi ya angani na vituo vya mauzo katika maduka.
Kyvistar alisema hakuna data binafsi za watumiaji wake zilizoathirika.
Soma pia:Intaneti yarejea Kyiv baada ya shambulizi la mtandao
MOD ilielezea tukio hilo kama "mojawapo ya mashambulizi ya mtandao yenye athari kubwa zaidi dhidi ya mitandao ya Ukraine tangu kuanza kwa uvamizi kamili wa Urusi."
Vikosi vya Urusi vyasema kombora la Ukraine limeua wawili kijiji cha Kherson
Shambulio la kombora la Ukraine kwenye kijiji kinachoshikiliwa na Urusi kusini mwa Ukraine limeua watu wawili, mamlaka yaukaliaji ya Moscow ilisema.
Kombora la HIMAR lililotengenezwa na Marekani lilipiga kijiji cha Nova Mayachka, kwenye ukingo wa Mto Dnipro unaokaliwa na Urusi, afisa aliyeteuliwa na Moscow Vladimir Saldo katika eneo la Kherson alisema.
Nova Mayachka iko umbali wa kilomita 70 (maili 40) mashariki mwa mji unaoshikiliwa na Ukraine wa Kherson.
Makombora mengine, ambayo alisema yalirushwa na Kyiv, yaliangushwa na mifumo ya ulinzi wa anga ya Urusi, Saldo aliongeza.
"Raia wawili waliuawa. Wengine wawili (raia) walijeruhiwa," alisema, akidai kuwa kombora hilo lilipiga "wakati wa utoaji wa misaada ya kibinadamu."
Wanajeshi waliokuwa wakisaidia kutoa msaada huo pia walijeruhiwa.
"Waliojeruhiwa wamepewa msaada unaohitajika wa matibabu na idara ya huduma za dharura inafanya kazi katika eneo la tukio," alisema Saldo.
Ukraine yaasema imedungua droni 30 za Urusi
Ukraine imesema kwamba mifumo yake ya ulinzi wa anga, kwa ushirikiano na vikosi vya jeshi la anga na jeshi la kawaida, ilidungua droni 30 kati ya 31 zilizotengenezwa na Iran aina ya "Shahed" zilizotumwa na Urusi mapema Jumamosi.
Soma pia: Urusi yarusha makombora, droni 23 kuelekea Ukraine
Shambulio hilo lilianzishwa kutoka pande tatu tofauti, Jeshi la anga la Ukraine lilisema katika chapisho kwenye jukwaa la ujumbe la Telegram.
Kisha droni hizo ziliharibiwa katika anga za mikoa 11 - Dnipropetrovsk, Kyiv, Vinnytsia, Chernihiv, Sumy, Poltava, Cherkasy, Kherson, Zaporizhzhya, Mykolaiv, na Khmelnytsky.
Chapisho hilo halikutaja kilichotokea kwa droni moja ambayo haikudunguliwa.
Lithuania yakarabati vifaru vya Leopard 2 vilivyoharibiwa Ukraine
Vifaru vya kwanza aina ya Leopard 2 vilivyowasilishwa Ukraine na kuharibiwa wakati wa vita dhidi ya Urusi vimerekebishwa nchini Lithuania. Vifaru hivyo vinatarajiwa kurejea katika uwanja wa vita wa Ukraine mwezi Januari.
Vifaru vya Leopard 2 vilirekebishwa katika kituo cha matengenezo kilichoanzishwa nchini Lithuania na makampuni mawili ya ulinzi ya Ujerumani, Krauss-Maffei Wegmann (KMW) na Rheinmetall.
"Lithuania waakti wote inaunga mkono mapambano ya Ukraine ya kupigania uhuru na haiishii tu kutuma msaada wa kijeshi, lakini pia inasaidia kutengeneza vifaru vya Leopard," alisema Waziri wa Ulinzi wa Lithuania Arvydas Anusauskas.
Soma pia: Ujerumani itaipa Ukraine msaada wa kijeshi wa euro bilioni 2.7
Lithuania pia imeitumia Ukraine katriji milioni kadhaa na makombora elfu kadhaa kwa ajili ya mifumo ya kivita ya masafa mafupi inayobebeka kwa ulinzi dhidi ya Urusi. Takriban vitanda 1,000 vya kukunjwa pia vimewasilishwa.
Ukraine yamuweka mkuu wa kanisa la Urusi kwenye orodha ya 'wanaosakwa'
Wizara ya Mambo ya Ndani ya Ukraine imetangaza kumweka mkuu wa Kanisa la Kiorthodoksi la Urusi, ambaye aliunga mkono uvamizi kamili wa Kremlin nchini Ukraine, kwenye orodha ya wanaotafutwa baada ya idara za usalama kumshutumu kuunga mkono mzozo huo.
Hatua hiyo ni ya kiishara zaidi, kwa sababu Patriaki Kirill yuko Urusi na hayuko katika kitisho cha kukamatwa. Ilikuwa hatua ya hivi karibuni zaidi katika kampeni ya Ukraine ya kuvunja ushawishi wa makasisi ambao inadai wanaendeleza uhusiano wa karibu na Urusi na kuangamiza jamii ya Ukraine.
Soma pia:Serikali ya Ujerumani yaidhinisha vifaru vya Leopard kwa Ukraine
Chapisho kwenye orodha ya wanaotafutwa ya wizara ya Ukraine lilimtambulisha Kirill kwa jina, na kumuonyesha akiwa amevalia mavazi yake ya ukasisi na kumtaja kama "mtu aliyejificha dhidi ya uchunguzi wa awali." Ilisema "alitoweka" tangu Novemba 11.
Ukristo wa Kiorthodoksi ndio imani kuu nchini Ukraine, na mamlaka mjini Kyiv zimeanzisha kesi za uhalifu dhidi ya makasisi wanaohusishwa na tawi la kanisa la Othodoksi lililokuwa na uhusiano wa moja kwa moja na kanisa la Urusi na Kirill. Kanisa linasema lilikata uhusiano wote na Moscow mnamo Mei 2022.