1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vita vya Ukraine vimeupindua mfumo wa dunia - Olaf Scholz

Daniel Gakuba
19 Januari 2023

Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz ameliambia kongamano la Davos kuwa vita vya Ukraine vimeupindua mfumo wa masuala ya dunia kichwa chini miguu juu, na kuongeza kuwa vyaweza kuwa fursa adimu ya kuachana na nishati chafu.

Schweiz Forum Davos | Bundeskanzler Olaf Scholz
Kansela wa Ujerumani, Olaf ScholzPicha: Markus Schreiber/AP Photo/picture alliance

Katika hotuba yake Kansela Scholz amesema uvamizi wa Urusi ambao ulifanyika siku chache tu baada ya kumalizika kwa kongamano kama la kimataifa kuhusu uchumi la mwaka jana, ulikuja wakati dunia ilipokuwa ikitarajia ukuaji wa uchumi wa kiwango kizuri, huku mipango ya kuhamia katika nishati safi kwa mazingira ikiwa imeshika kasi.

Soma zaidi: Guterres:Tuwajibike ili kuwa na dunia salama

Amesema baada ya uvamizi huo, nchi nyingi, Ujerumani ikiwemo zilijikuta zikipambana na changamoto ya kuacha utegemezi wa nishati kutoka Urusi, mchakato ambao ulisababisha mfumko wa bei na kupanda kwa gharama ya maisha.

Fursa ya kupata vyanzo mbadala vya nishati

Hata hivyo, amesema kiongozi huyo wa serikali ya Ujerumani, machungu haya yanaweza kuambatana na fursa adimu ya kuipa kisogo nishati chafu kwa mazingira, na yameifanya Ujerumani iache kuitegemea Urusi kama chanzo kikuu cha nishati yake.

Vifaru chapa Leopard 2 ambavyo Ujerumani inashinikizwa kuridhia vipelekwe UkrainePicha: Michael Kappeler/dpa/picture alliance

''Katika muda wa miezi michache, Ujerumani iliweza kuachana kikamilifu na utegemezi kwa gesi, mafuta na makaa ya mawe kutoka Urusi,'' amesema Scholz, na kuongeza kuwa  Ujerumani ilikamilisha ushirikiano na nchi za Asia, Afrika na America ili kupunguza utegemezi huo, ''na naweza kusema kuwa tuko salama lihusikapo suala na nishati mnamo majira haya ya baridi.''

Zelenskiy aongeza shinikizo kutaka Ukraine ipatiwe vifaru

Hotuba nyingine muhimu katika kongamano hili la Davos ilitolewa kwa njia ya vidio na rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy, ambaye alijikita zaidi katika ombi la nchi yake kutaka ipatiwe vifaru vya kisasa kutoka washirika wake wa magharibi, akionekana kuilenga Ujerumani ambayo licha ya shinikizo kutoka kwa washirika wake katika jumuiya ya kujihami ya NATO, bado inasitasita kuridhia kupelekwa kwa vifaru chapa Leopard-2 nchini Ukraine. Vifaru hivyo hutengenezwa nchini Ujerumani.

Rais wa Colombia, Gustavo PetroPicha: Markus Schreiber/AP/picture alliance

Madawa ya kulevya, tatizo sugu

Viongozi wengine waliozungumza jana jioni ni pamoja na rais wa Colombia Gustavo Petro ambaye alikosoa vikali mkakati wa Marekani katika kupambana na madawa ya kulevya. Akichangia juu ya suala hilo kwenye jukwaa lililowashirikisha wanasiasa kutoka Amerika Kusini, rais huyo alisema mkakati huo wa Marekani umesababisha kufungwa jela kwa maelfu ya watu, wengi wakiwa Wamarekani weusi, na wapatao milioni kuuawa katika ukanda wa Amerika Kusini.

Soma zaidi:Davos mjadala watawala ushirika wa China kimataifa 

Amesema ikiwa dunia haitakuwa tayari kuwa na mjadala kuhusu sera hiyo ya Marekani iliyoshindwa, dawa za kulevya zitaendelea kuwa tatizo sugu. Yeye alipendekeza mkakati wenye msingi katika kuelimisha, kuzuia na kuwapa matibabu wale ambao tayari wameanguka katika uraibu wa dawa hizo.

 

Vyanzo: ape, dpae