Vita vya Ukraine kuongeza mpasuko kati ya Urusi na Japan
16 Aprili 2024Umoja wa Ulaya umekuwa ukihimiza misaada zaidi kwa Ukraine, jukumu ambalo umoja huo umekuwa ukidhani kuwa ni lake na Marekani pekee, ingawa kwa miezi kadhaa sasa, Bunge la Marekani halijafikia makubaliano juu ya mpango mpya wa mabilioni ya fedha ya msaada kwa Ukraine.
Matokeo yake, nchi nyingine sasa zimeamua kuchukua jukumu la kuongeza sehemu yao ya misaada kwa Ukraine.
Miongoni wa mataifa hayo ni Japan, ambayo, kulingana na Wizara ya Fedha ya Ukraine, imekuwa ikifadhili misaada mbalimbali ya kifedha huku ufadhili huo ukitajwa ndio mkubwa zaidi kwa kipindi cha miezi miwili ya kwanza kwa mwaka 2024.
Katika mkutano uliofanyika Japan wa mwezi Februari, Waziri Mkuu wa Ukraine, Denys Shmyhal alisema msaada uliotolewa na kuahidiwa utafikia dola bilioni 12.
Kulingana na Taasisi ya Kiel ya Uchumi wa Dunia, Japan ilikuwa katika nafasi ya sita kwa kutoa misaada wa kimataifa kwa Ukraine mnamo Januari ikitajwa kutoa zaidi ya euro bilioni 7.
Soma pia:Zelensky ataka washirika kuwasaidia kama wanavyosaidia Israel
Msaada huo kutoka Japan umeisaidia kwa kiwango kikubwa Ukraine. Benki Kuu inakadiria kuwa pato la taifa limepungua kwa theluthi moja tangu uvamizi wa Urusi ulipoanza Februari, 2022.
Kulingana na kanuni za kimataifa, Japan hairuhusiwi kuipatia silaha za kivita Ukraine na badala yake inaweza kupeleka chakula, magari na dawa, pamoja na vitu vingine vya muhimu vitani, lakini siyo silaha.
Ukraine yenyewe kwa muda sasa imekuwa ikitoa mwito wa kupatiwa msaada wa silaha za kisasa ili kuendeleza mapambanio yake ya kujilinda dhidi ya uvamizi wa Urusi.
Uhusiano wa Urusi na Japan kuingia dosari
Vyombo vya habari vya Japan vimeripoti kuwa huenda Marekani ikapeleka makombora huko Ukraine ambayo mtengenezaji wake ni Japan, suala ambalo limeiibua Wizara ya Mambo ya Nje ya Urusi ikisema kwamba kama ikitokea makombora hayo yakapelekwa Ukraine basi uhusiano wake na Japan utaingia dosari.
Atsuko Higashino, Profesa anayeusomea mzozo wa Ukraine katika Chuo Kikuu cha Tsukuba, yeye anaunga mpango huo wa Marekani wa kupeleka makombora hayo nchini Ukraine kwa sababu anaamini kwamba makombora hayo sio silaha ya kuua bali ni kwa ajili ya kuwalinda watu wa Ukraine.
Kwa upande wake, Professa James Brown, ambaye ni mtaalam wa masuala ya uhusiano kati ya Urusi na Japan katika chuo kikuu cha Temple kilichoko Tokyo, anaamini kuwa upelekaji wa makombora chapa Patriot kwenda Marekani tayari umekubaliwa kwa kiasi kikubwa.
Ameongeza kusema kuwa ucheleweshaji wa mpango huo unatokana na kanuni, akifafanua kuwa ni muhimu sana kwa Japan kwamba makombora yake hayapelekwei moja kwa moja kwa Ukraine.
Soma pia:Ukraine yaomba misaada ziada ya kijeshi kuikabili Urusi
Mchambuzi wa masuala ya kisiasa Higashimo ameongeza kuwa mtazamo wa Japan kwa Urusi na Ukraine umebadilika kwa kiasi kikubwa tangu Urusi ilipolinyakua kimabavu eneo la Ukraine la Crimea mwaka 2014, na uvamizi wake kamili wa mwaka 2022 umeongeza doa zaidi kwenye uhusiano wa mataifa hayo mawili.
Kwa sasa, Japan haijasitisha kabisa uhusiano wake na Urusi. Ingawa kuna tofauti kwenye baadhi ya maeneo ya kiuchumi hasa kwenye sekta ya nishati.
Makampuni ya magari ya Kijapani yamejiondoa kwenye soko kubwa la Urusi, lakini Japan bado inashiriki katika mradi wa mafuta na gesi wa Sakhalin 2 unaoongozwa na Gazprom, ingawa mataifa mengine ya Magharibi hayashiriki tena.
Mradi huo unaisambazia Japan gesi asilia. Japan inapata takribani asilimia 9 ya gesi yake kutoka Urusi.