Jiji la Moscow kwa mara ya kwanza lashambuliwa kwa Droni
30 Mei 2023Mashambulio kama hayo hayajawahi kushuhudiwa, hata hivyo msaidizi wa rais wa Ukraine amekanusha nchi hiyo kuhusika moja kwa moja na mashambulio hayo yaliyoulenga mji wa Moscow. Wizara ya ulinzi ya Urusi imeilaumu Ukraine kwa mashambulio hayo ya ndege zisizo na rubani dhidi ya jiji la Moscow na maeneo jirani, ambapo imesema watu wawili wamejeruhiwa kidogo pamoja na kusababisha uharibifu mdogo katika baadhi ya majengo ya makazi ya watu.
Meya wa jiji la Moscow Sergei Sobyanin amethibitihsa kwamba raia wawili wamejeruhiwa katika mashambulizi ya leo alfajiri ambapo pia yamesababisha uharibifu mdogo kwenye majengo. Meya Sobyanin amesema wakazi ambao majengo yao yameharibiwa wamehamishwa kwa muda mfupi kutoka kwenye sehemu hiyo.
Soma:Urusi yafanya mashambulizi mapya ya anga mjini Kiev
Majengo hayo yaliyoshambuliwa yapo kusini-magharibi ya mji mkuu wa Moscow kitongoji ambapo wanaishi watu wenye uwezo mkubwa kifedha karibu na katikati mwa jiji la Moscow. Na eneo jingine lipo karibu na mbuga maarufu. Wakazi katika mojawapo ya majengo ya ghorofa yaliyopigwa wamesema walisikia milio isiyo ya kawaida mapema leo asubuhi.
Wizara ya ulinzi ya Urusi imesema ndege nane zisizo na rubani zilitumika katika mashambulio hayo na kwamba mfumo wa ulinzi ulizuia ndege hizo zote kuleta maafa katika maeneo yaliyolengwa.
Msaidizi wa rais wa Ukraine amekanusha kwamba nchi yake imehusika moja kwa moja katika mashambulio hayo lakini amesema Ukraine inafurahia kuona matukio kama hayo nchini Urusi na ametabiri kuongezeka kwa mashambulizi ya aina hiyo. Wakati huo huo Urusi inaendelea na mashambulio ya mchana na usiku dhidi ya mji mkuu wa Ukraine, Kiyv. Mashambulizi hayo yalianza usiku wa kuamkia Jumatatu.
Soma:Urusi yaonya mipango ya kuipatia Ukraine ndege za kivita
Tangu Urusi ilipowapeleka wanajeshi wake katika nchi jirani yake ya Ukraine mnamo mnamo Februari mwaka uliopita kwa kiasi mkikubwa vita hivyo vimekuwa vinapiganiwa ndani ya Ukraine, ingawa Moscow imeripoti baadhi ya mashambulizi katika maeneo yake ikiwa ni pamoja na madai ya jaribio la mauaji dhidi ya Rais Vladimir Putin.
Vyanzo:RTRE/AP