1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vita vya Ukraine vyautikisa uchumi wa dunia - IMF

19 Aprili 2022

Shirika la Fedha la Kimataifa, IMF, limeshusha makisio ya ukuwaji wa uchumi wa dunia mwaka huu, likisema uvamizi wa Urusi dhidi ya Ukraine umechangia kwenye kuichafuwa biashara ulimwenguni na kupandisha bei za bidhaa.

 Kristalina Georgieva
Picha: Yves Herman/REUTERS

Siku ya Jumanne (Aprili 19), IMF, ambayo ni mkopeshaji mkubwa kwa zaidi ya mataifa 190 duniani, iliyakata makisio yake ya ukuwaji wa uchumi wa dunia hadi asilimia 3.6 tu kwa mwaka huu, kutoka asilimia 6.1 mwaka jana na asilimia 4.4 uliokwishatazamiwa mwaka huu wa 2022 mnamo mwezi Januari.

Shirika hilo lilisema uvamizi wa Urusi dhidi ya Ukraine uliokuja wakati dunia ikiwa bado inakabiliana na athari za janga la virusi vya corona, vinaonekana kuutikisa zaidi uchumi.

Akiandika kwenye dibaji ya Mwelekeo wa Uchumi wa Dunia uliochapishwa Jumanne, mchumi mkuu wa IMF, Pierre-Olivier Gourinchas, alisema "ulimwengu ulikuwa karibuni kabisa kufufuka kutoka giza la janga la UVIKO-19, lakini sasa vita vilivyoanzishwa na Urusi vimeyafuta mafanikio hayo kwa wiki chache tu na kwa kasi kubwa zaidi."

Kwa mujibu wa IMF, uchumi wa Urusi yenyewe utatikisika kwa asilimia 8.5, huku wa Ukraine ukiyumba kwa asilimia 35.

Marekani, Ulaya kuathirika

Mwanajeshi wa Urusi katika eneo eneo la Iskander.Picha: Russian Defence Ministry/TASS/dpa/picture alliance

Marekani, ambayo inashiriki vita hivyo kupitia shinikizo lake la kimataifa na msaada wa vifaa vya kijeshi kwa Ukraine, itashuhudia uchumi wake ukishuka kwa asilimia 3.7 kutoka asilimia 5.7 mwaka jana, iliyokuwa kasi kubwa zaidi ya ukuwaji kuwahi kushuhudiwa tangu mwaka 1984. 

Ulaya, ambayo ni tegemezi sana kwa nishati kutoka Urusi, itakabiliwa na machungu ya kiuchumi kutokana na vita vya Urusi na Ukraine.

Mataifa 19 yanayotumia sarafu ya Euro yatashuhudia uchumi wake ukiwa kwa asilimia 2.8 tu ikilinganishwa na mategemeo ya asilimia 3.9 yaliyokuwa nayo mwezi Januari.

Katika hotuba yake ya wiki iliyopita, mkurugenzi mkuu wa IMF, Kristalina Georgieva, alionya juu ya kitisho kikubwa cha njaa, kuongezeka kwa umasikini na kuripuka machafuko makubwa ya kijamii duniani, kutakakochochewa na vita vya Urusi nchini Ukraine. 

Urusi yatangaza njia salama kwa wanajeshi wa Ukraine

Vikosi vya Urusi katika mji wa Mariupol.Picha: Alexei Alexandrov/AP/picture alliance

Ripoti ya IMF imechapishwa wakati mashambulizi ya Urusi yakishamiri kwenye maeneo ya mashariki ya Ukraine, ambapo inaelezwa kuwa jeshi la Urusi linadhamiria kuchukuwa udhibiti kamili wa majimbo ya Luhansk na Donetsk yaliyotangaza kujitenga na Ukraine.

Urusi yenyewe ilisema kuwa vikosi vyake vimefunguwa njia za salama kupita kwa wanajeshi wa Ukraine waliokubali kujisalimisha na kuondoka mji wa Mariupol mchana wa leo. 

Taarifa iliyotolewa na mkuu wa operesheni ya kijeshi wa Urusi, Mikhail Mizintsev, ilisema kuwa jeshi lake limesitisha mashambulizi yake kwenye eneo la kiwanda cha chuma cha Azovstal, ambako wanajeshi hao wa mwisho wa Ukraine walikuwa wamejificha. 

Ikiwa mji wa Mariupol umeangukia mikononi mwa Urusi, hayo yatakuwa mafanikio makubwa ya kwanza tangu kuanza uvamizi mnamo tarehe 24 Februari.
 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW