1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vita vya Urusi na Ukraine vyaingia siku 100

3 Juni 2022

Ukraine Ijumaa inaadhimisha siku 100 tangu uvamizi wa Urusi kuanza nchini humo huku mapigano yakizidi mashariki mwa nchi hiyo ambapo majeshi ya Urusi yanazidi kupambana ili kulidhibiti jimbo la Donbas.

100 Tage Krieg in der Ukraine
Picha: Natacha Pisarenko/AP

Hatua hii ya siku 100 inakuja wakati ambapo Ukraine imetangaza kuwa Urusi kwa sasa inadhibiti sehemu ya Ukraine ikiwemo Crimea na maeneo ya Donbas yaliyotekwa mwaka 2014.

Baada ya kushindwa katika azma yao ya kuuteka mji mkuu Kyiev, majeshi ya Urusi sasa yameelekeza juhudi zote katika kuiteka Ukraine mashariki jambo ambalo huenda likaupelekea mzozo huo kujikokota na kuchukua muda mrefu zaidi.

Ukraine nayo imepata mafanikio katika mapambano ya mashariki

Mapigano makali sasa yako Severodonetsk katika eneo la Donbas ambapo asilimia 80 ya eneo hilo tayari lishatekwa na Urusi ila majeshi ya Ukraine yanaweka upinzani mkali bado. Rais Volodymyr Zelenskiy hapo Alhamis alisema Ukraine imepata ufanisi kiasi cha haja katika mapambano hayo ya mashariki.

"Hali ni ngumu huko kama ilivyo katika miji na makaazi ya karibu. Lysychansk, Bakhmut na maeneo mengine. Kuna miji mingine pia ambapo mashambulizi makali kama hayo yanafanywa na Urusi. Jeshi la Urusi linatumia nguvu zake zote za kijeshi, halijali watu kabisa," alisema Zelenskiy.

Gavana wa Donetsk Pavlo Kyrylenko amesema raia wawili wameuwawa Donetsk wakiwemo wawili wengine katika mji wa Avdiivka na wengine tisa kujeruhiwa ingawa taarifa hizo hazikuweza kuthibitishwa na shirika la habari la Reuters.

Ingawa Urusi inakanusha kuwalenga raia katika mashambulizi yake, inakiri kuwa inalenga miundo mbinu inayotumiwa kuingiza zana kutoka mataifa ya Magharibi.

Rais Zelenskiy amesema Ukraine inatarajia kupokea silaha zaidi kutoka kwa marafiki zake baada ya Marekani kutoa ahadi ya kutuma msaada. Urusi imeituhumu Marekani kwa kuchochea vita hivyo baada ya ahadi hiyo ya silaha zenye thamani ya dola milioni 700 kwa Ukraine ambazo zitajumuisha roketi zinazoweza kurushwa hadi kilomita 80.

Ikumbukwe kwamba awali Rais Joe Biden alikanusha kwamba Marekani haitoitumia Ukraine roketi ili kulenga maeneo ndani ya Urusi.

Chad yatangaza njaa kutokana na vita vya Ukraine

Haya yanafanyika wakati ambapo Shirika la Umoja wa Mataifalinalowashughulikia watoto UNICEF linasema vita vya Ukraine ni mzozo dhidi ya haki za watoto kwa kuwa takriban watoto 100 wameuwawa katika mwezi mmoja uliopita tu na mamilioni wengine kulazimika kuyakimbia makaazi yao.

Huku hayo yakiarifiwa taifa la Chad limetangaza hali ya dharura ya chakula kutokana uhaba wa nafaka uliosababishwa na vita vya Ukraine. Serikali ya kijeshi nchini humo inasema, hali ya chakula imekuwa mbaya mno na misaada ya kiutu inahitajika mara moja.

Zania Muhammed akimbembeleza mwanawe aliye na utapia mlo nchini ChadPicha: ANDREW CABALLERO-REYNOLDS/AFP/Getty Images

Rais wa Umoja wa Afrika Macky Sall Ijumaa atafanya mazungumzo na Rais wa Urusi Vladimir Putin mjini Sochi ili kutoa wito wa kuondolewa kwa vikwazo vya usafirishaji wa nafaka na mbolea.

Chanzo: Reuters/AFP/AP

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW