Vita vya Urusi na Ukraine vyaingia siku elfu moja
19 Novemba 2024Haya yanafanyika wakati ambapo mwanadiplomasia anayeondoka wa Umoja wa Ulaya Josep Borrell, amewashinikiza wanachama wa umoja huo kuungana na Marekani kuikubalia Ukraine ishambulie ndani ya ardhi ya Urusi kwa kutumia makombora ya masafa marefu iliyopewa.
Katika taarifa, wizara ya mambo ya nje ya Ukraine imesema nchi hiyo haitoyakubalia matakwa ya Urusi iliyoikalia ardhi yao na kwamba nchi hiyo itaadhibiwa kwa kukiuka sheria ya kimataifa.
Balozi wa Ukraine katika Umoja wa Mataifa Yevheniia Filipenko ameliambia shirika la habari la Reuters kwamba hakuna haja ya kutafuta amani na Rais Vladimir Puztin akidai mashambulizi ya hivi majuzi makubwa nchini Ukraine yanaonyesha hana haja ya amani.
Putin hataki amani
Filipenko amesema hatua ya kuishambulia gridi ya umeme ya Ukraine katika shambulizi kubwa la angani mwishoni mwa wiki inaonyesha kwamba Putin anataka vita hivyo vilivyoingia siku elfu moja viendelee na kwamba nia yake kuu ni kuitumbukiza Ukraine gizani na kwenye baridi.
Mwanadiplomasia huyo ameyasema haya wakati ambapo wengi wanatarajia mazungumzo ya amani na Rais Putin mwakani kutokana na kubadilishwa kwa utawala nchini Marekani na kuonekana kwa dalili za uchovu wa vita.
Kwa upande wake makamu wa rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya Josep Borrell amewaambia waandishi wa habari kuwa mabadiliko ya sera ya Marekani ya kuitaka Ukraine ishambulie ndani ya Urusi kuwa ni "habari njema."
Ingawa Rais Joe Biden hajazungumzia hadharani suala hilo, afisa mmoja wa Marekani amethibitisha Washington sasa itaikubalia Ukraine kutumia makombora yake ya masafa marefu dhidi ya Urusi.
Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz hapo Jumatatu kwa mara nyengine aliondoa uwezekano wa kuipa idhini Ukraine kushambulia ndani ya Urusi kwa kutumia makombora yake ya Taurus.
Urusi yasaini amri ya kutumia nyuklia
Hayo yakiarifiwa Rais Volodymyr Zelenskiy wa Ukraine amesema watu saba wamefariki dunia akiwemo mtoto, kufuatia shambulizi la Urusi katika eneo la kaskazini mashariki mwa Ukraine la Sumy.
"Makamanda wetu wamenipa ripoti hizo ikiwemo ripoti kuhusu hali ya usalama na kijamii katika maeneo ya Donetsk na Kharkiv. Tunashikilia misimamo yetu, shukran kwa majeshi yetu, Ushindi kwa Ukraine!" alisema Zelenskiy.
Shambulizi hilo lililofanyika usiku wa kuamkia Jumanne lililenga jengo moja la makaazi katika mji mdogo wa Hlukhiv unaopakana na Urusi na kusababisha watu 12 kujeruhiwa, wakiwmo watoto wawili.
Haya yote yanafanyika wakati ambapo Rais Vladimir Putin Jumanne amesaini amri rasmi inayoikubalia Moscow kutumia zana za nyuklia dhidi ya taifa lolote lile ambalo halina silaha hizo, iwapo taifa hilo linaungwa mkono na nchi zenye silaha za nyuklia.
Vyanzo: Reuters/AFP