1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vita vya Urusi vyaongeza haja ya kuimarisha ulinzi Ujerumani

Grace Kabogo /Marcel Fürstenau
12 Desemba 2025

Idara ya ujasusi ya Ujerumani inashinikiza kuwepo kwa nguvu zaidi katika mapambano dhidi ya shughuli za kijasusi na hujuma, kutokana na vitisho vya Urusi, ili kuimarisha usalama wa Ujerumani.

Deutschland |Vitisho kwa vita vya Urusi vyashinikiza uimarishaji usalama Ujerumani
Vita vya Urusi vyaongeza haja ya kuimarisha ulinzi UjerumaniPicha: Angelika Warmuth/REUTERS

Tangu Urusi ilipoishambulia Ukraine mnamo Ferbuari mwaka 2022, kumekuwa na mazungumzo kuhusu mbinu tofauti za vita vya kimkakati miongoni mwa wataalamu wa usalama na wanasiasa wa Ujerumani. Ujerumani inaathiriwa pakubwa na mchanganyiko wa shughuli za kijeshi na kijasusi, mara nyingi zikiambatana na propaganda za kupotosha.

Mwezi Septemba, Kansela wa Ujerumani Friedrich Merz alisema ''nchi yake haiko vitani, lakini haina amani tena.'' Kazi kuu ya Idara ya Ujasusi wa Ndani ya Ujerumani, BfV ni kutambua mapema vitisho ili kuzuia mashambulizi. Kwa kuzingatia kiwango cha vitisho vya sasa, Mkurugenzi Mkuu wa BfV, Sinan Selen anasema shirika lake linahitaji nguvu zaidi.

Akizungumza katika kongamano la kila mwaka la Ulinzi na Katiba mjini Berlin, Selen anasema wana aina za mawasiliano ambazo hawawezi tena kuzifafanua kwa sehemu, kwani kuna maafisa wanaofanya kazi kwa kutumia majina bandia. Kulingana na Selen, kama idara ya ujasusi wanapaswa wafanikiwe kupenya katika maeneo hayo, na anategemea mabadiliko ya sheria za usalama ili kulifikia lengo hilo.

Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Ujasusi wa Ndani ya Ujerumani, BfV, Sinan Selen Picha: Bernd von Jutrczenka/dpa/picture alliance

Tayari Waziri wa Mambo ya Ndani wa Ujerumani, Alexander Dobrindt ametangaza mageuzi, huku uungwaji mkono ukiwa umeonyeshwa pia na ofisi ya kansela, ambapo Philipp Wolff anaratibu mashirika matatu ya kijasusi nchini: Ofisi ya Shirikisho ya Ulinzi wa Katiba, Idara ya Shirikisho ya Ujasusi, na Idara ya Kijeshi ya Kupambana na Ujasusi.

Upinzani umekuwa ukipinga sheria kali za usalama

Wolff anasisitiza kuwa kuongezeka kwa ufuatiliaji ulioongezeka mtandaoni na uhifadhi wa anwani za IP ni muhimu. Pia anataka mashirika ya usalama yaweze kubadilisha data binafsi kwa urahisi zaidi.Hata hivyo, bado haijabainika wazi kama hilo litawezekana

Vyama vya upinzani na mashirika ya kiraia kila mara yamekuwa yakipinga sheria kali za usalama katika Mahakama ya Katiba ya Shirikisho la Ujerumani, na mara nyingi kwa mafanikio.

Lakini Selen, bado ana matumaini. Anasema nchi nyingine za Ulaya kama vile Ufaransa na Uholanzi, ziko mbele zaidi, akimaanisha nchi mbili zenye vikwazo vichache vya kisheria kuhusu ufuatiliaji wa washukiwa na sheria zisizo kali za ulinzi wa data.

Kutokana na mkakati wa hivi karibuni wa Rais wa Marekani, Donald Trump kuhusu Usalama wa Kitaifa, ni vigumu kujua jinsi uhusiano wa kijasusi wa BfV na Marekani utakavyokua. Selen anasisitiza umuhimu wa kupitia upya na kuendeleza miungano. Kwa mtazamo wake, Ulaya lazima iwe huru zaidi na kutoitegemea Marekani.

Rais wa Urusi Vladimir Putin Picha: Gavriil Grigorov/AFP

Kulingana na Wollf, BfV na mashirika mengine ya usalama ya Ujerumani tayari yanafanya kazi. Anasema Warusi wanalijua hilo pia, na tayari wanaichukulia Ujerumani kwa umakini mkubwa, na kwamba mjadala wa kitaifa kuhusu jinsi ya kukabiliana na vitisho vya mbinu tofauti za vita vya kimkakati, unafuatiliwa kwa karibu huko Moscow.

Mkakati wa Urusi ni Imara

Carlo Masala, mtaalamu wa kijeshi katika Chuo Kikuu cha Kijeshi cha Munich, anauelezea mkakati wa Urusi kuelekea nchi za Jumuiya ya Kujihami ya NATO kama unaozidi kuwa imara na jasiri.

Wataalamu kama Masala wanashuku kuwa Urusi inahusika na kuongezeka kwa vitendo vya hujuma katika reli, viwanja vya ndege, na miundombinu ya kusambaza maji na umeme.

Hata hivyo, Masala anaonya kuwa miundombinu muhimu pia inaweza kuharibika kwa njia isiyo ya moja kwa moja. Anasema kuna kituo kidogo cha umeme nchini Austria, na kikiharibiwa, basi sehemu kubwa ya Ujerumani itakosa umeme.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW