1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vita vyazidi makali kanda ya Mashariki ya Kati

3 Machi 2026

Hali hiyo ya mashaka ulimwenguni na kauli za kutunishia misuli zimeshuhudiwa kutwa nzima jana Jumatatu, katikati ya mashambulizi makali ya Marekani na Israel nchini Iran.

Iran Tehran 2026 | Raia wakiokoana baada ya Israel kuushambulia mji mkuu wa Iran, Tehran
Raia wakiokoana baada ya Israel kuushambulia mji mkuu wa Iran, Tehran.Picha: Erfan Kouchari/Parspix/ABACAPRESS/IMAGO

Tehran nayo ilijibu kwa kuishambulia Israel na kuyalenga maeneo kadhaa ya nchi za ghuba, ikiwemo miundombinu ya nishati nchini Qatar na Saudi Arabia.

Usiku wa kuamkia leo, Iran imeushambulia ubalozi wa Marekani nchini Saudi Arabia kwa ndege mbili zisizo na rubani na kuzusha moto na uharibifu mdogo. Hayo yameelezwa na Wizara ya Ulinzi ya Saudi Arabia.

Mkaazi mmoja kwenye eneo uliko ubalozi huo ameliambia shirika la habari la Associated Press kwamba ameona moshi ukifuka kutoka kwenye jengo la ubalozi wa Marekani. Hapo jana pia, Iran iliushambulia ubalozi wa Marekani nchini Kuwaita.

Shambulizi la mjini Riyadh limesababisha hasira nchini Marekani na Rais Donald Trump amesema Iran "itatambua muda usio mrefu, majibu" ya Washington kwa uamuzi wake wa kuulenga ubalozi.

Trump pia amesema, Marekani italipa kisasi kwa vifo vya wanajeshi sita wa nchi hiyo vilivyotokea tangu nchi yake na Israel zilipoishambulia kwanza Iran, Jumamosi iliyopita.

Hapo jana Trump alizungumza na waandishi wa habari na kuarifu kuwa vita dhidi ya Iran vitaendelea hadi kwa muda wa wiki au tano ama kwa kadri itavyohitajika.

Marekani yawataka wananchi wake kuondoa nchi 12 za Mashariki ya Kati 

Shambulizi la Iran baada ya kutua kwenye mji wa Israel wa Tel Aviv.Picha: Chen Junqing/Xinhua/IMAGO

Katika ishara kwamba mzozo huo unazidi makali,Wwizara ya Mambo ya Kigeni ya Marekani imewataka raia wote wa Marekani kuondoka haraka kutoka kwenye zaidi ya nchi 12 za Mashariki ya Kati.

Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Marekani, Marco Rubio amesema "mashambulizi makali zaidi kutoka jeshi la Marekani dhidi ya Iran" bado hayajaanza. Ameonya kuwa awamu ijayo ya mashambulizi itakuwa nzito kuliko inayoshuhudiwa sasa.

Licha ya vitisho hivyo, maafisa waandamizi nchini Iran wamesisitiza vita vitaendelea na hakuna dalili ya kupatikana mwafaka. Katibu Mkuu wa Baraza la Taifa la Usalama la Iran, Ali Larijani, aliandika kupitia ukurasa wake wa mtandao wa X kwamba, nchi hiyo haitozungumza na Marekani.

Kwa upande wake Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran, Abbas Araghchi, amesema Iran ilijiandaa kwa muda mrefu kwa vita na imejifunza mbinu zote za kivita za Marekani na kwamba jamhuri hiyo ya kiislamu haitosalimu amri.

Mashambulizi ´yachacha´ huku bei ya nishati ikipanda kwa kasi 

Safari nyingi za ndege kwenye eneo la Mashariki ya Kati zimefutwa kutokana na mapigano yanayoendelea. Picha: Altaf Qadri/AP Photo/dpa/picture alliance

Pamoja na maneno hayo ya ujasiri, makombora ya ndege za kivita za Israel yaliutikisa mji mkuu wa Iran, Tehranusiku wa kuamkia leo. Jeshi la Israel limesema limeyalenga makao makuu ya shirika la utangazaji la Iran ililolituhumu kuwa "chombo cha propaganda" cha utawala ilioutaja kuwa wa "kigaidi wa Iran".

Mzozo huo wa kivita tayari umeanza kuteteresha masoko ya hisa na kutishia kutokea athari kubwa za kiuchumi.

Bei ya nishati ya mafuta inatazamiwa kupanda zaidi leo, baada ya hapo jana kufikia dola 82 kwa pipa moja la mafuta ghafi kutoka angalau dola 60 kwa pipa wiki iliyopita.

Tathmini ya awali pia ya masoko ya hisa na mitaji imeonesha makampuni ya safari yamepoteza karibu dola bilioni 22 kutokana na kutatizika kwa usafiri wa anga kwenye viwanja vikubwa vya Mashariki ya Kati.

Safari karibu zote za ndege zimefutwa kwenye viwanja vingi vya nchi za ghuba tangu mzozo wa kivita ulipozuka mwishoni mwa juma lilipota baada ya Marekani na Israel kuishambulia Iran na kumuua Kiongozi Mkuu wa nchi hiyo Ayotallah Ali Khamenei.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW