1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaIsrael

Vituo vya ukaguzi wa misaada ya Gaza kufunguliwa leo

12 Desemba 2023

Uchunguzi wa usalama unatarajiwa kuanza hii leo katika vivuko vya Kerem Shalom na Nitzana ambao utasaidia kuongeza maradufu kiasi cha misaada inayowasilishwa katika Ukanda wa Gaza.

Kivuko cha Kerem Shalom kinachotumika kusafirisha misaada ukanda wa Gaza
Afisa wa polisi wa Palestine akisisima karibu na kivuko cha Kerem Shalom kusini mwa ukanda wa Gaza.Picha: Khaled Omar/Xinhua/IMAGO

Israel leo imeendelea na mashambulizi katika ukanda wa Gaza ikiwasaka viongozi wa kundi la wanamgambo wa Hamas, katika mashambulizi ambayo Israel inasema yanaweza kuendelea kwa wiki au miezi kadhaa ijayo.

Hayo yanatokea wakati Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linatarajiwa baadaye leo kupiga kura juu ya rasimu ya azimio la kutaka kusitishwa mara moja kwa mapigano huko Gaza. Hata hivyo iwapo azimio hilo litapitishwa halitakuwa na uzito wowote wa lazima. 

Soma pia: Baerbock: Ujerumani inatumai Israel itazuia madhila kwa Wapalestina 

Jeshi la Israel limefanya mashambulizi usiku kucha na mapema leo kusini mwa Gaza - eneo ambalo watu wamelikimbilia ili kutafuta hifadhi. Kwa mujibu wa mwandishi wa habari wa shirika la Associated Press, mashambulizi hayo yamesababisha vifo vya takriban watu 23.

Katika mkutano na waandishi wa habari, waziri wa ulinzi wa Israel Yoav Gallant alikataa kuzungumzia juu ya muda wa oparesheni ya kijeshi ya nchi yake, japo ameashiria kuwa awamu ya sasa ya mashambulizi ya ardhini na angani huenda ikadumu kwa wiki kadhaa zijazo au hata miezi.

Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu amesema kuwa Israel itadumisha udhibiti wa usalama katika ukanda wa Gaza kwa muda usiojulikana.

Gallant asema Israel haina nia ya kuikalia kwa nguvu Gaza

Waziri wa ulinzi wa Israel Yoav Gallant katika mkutano na waandishi wa habari katika kambi ya jeshi ya Kirya mjini Tel Aviv.Picha: Abir Sultan/AP Photo/picture alliance

Wakati huo huo Israel imesema uchunguzi wa usalama unatarajiwa kuanza hii leo Jumanne katika vivuko vya Kerem Shalom na Nitzana ambao utasaidia kuongeza maradufu kiasi cha misaada inayowasilishwa katika Ukanda wa Gaza.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres, mataifa ya kiarabu na jamii ya kimataifa imetoa wito wa kusitishwa mapigano mara moja katika ukanda wa Gaza.

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linatarajiwa baadaye leo kupiga kura juu ya rasimu ya azimio la kutaka kusitishwa mara moja kwa mapigano huko Gaza.

Soma pia: Israel yakanusha kutaka kuwahamishia Misri wakaazi wa Gaza 

Hata hivyo iwapo azimio hilo litapitishwa halitakuwa na uzito wowote wa lazima.

Wakati hayo yakiarifiwa, Mkuu wa shirika la afya duniani WHO ameelezea wasiwasi wake juu ya ukaguzi wa muda mrefu wa misafara iliyobeba vifaa vya matibabu katika ukanda wa Gaza na kuzuiliwa kwa wahudumu wa afya.

WHO imesema ukaguzi huo umesababisha kifo cha mgonjwa aliyehitaji msaada wa dharura.

Katika taarifa iliyochapishwa kwenye jukwaa la mtandao wa X, Tedros Adhanom Ghebreyesus amesema timu ya madaktari wa WHO iliyokuwa njia kuelekea katika hospitali ya Al-Ahli siku ya Jumamosi, ilisimamishwa mara mbili katika kituo cha ukaguzi cha Wadi Gaza kinachosimamiwa na jeshi la Israel.

Ghebreyesus ameeleza kuwa baadhi ya wafanyikazi wa shirika la hilali nyekundu la Palestina pia wamezuiliwa na jeshi la Israel.

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW