Vituo vya wagonjwa wa Ebola vinajaa haraka
15 Agosti 2014Msemaji wa WHO, Gregory Hartl, amesema leo kuwa hatua ya kufurika kwa wagonjwa katika vituo maalum vilivyofunguliwa kwa ajili ya kuwahudumia wagonjwa wa Ebola, inaashiria kuwa mripuko huo ni mkubwa kuliko ilivyodhaniwa.
Hartl amesema kituo chenye vitanda 80 vya wagonjwa kilichofuguliwa kwenye mji mkuu wa Liberia, Monrovia, katika siku za hivi karibuni, kinajaa kupita uwezo wake.
Kwa mujibu wa WHO, ugonjwa wa Ebola ulioanzia nchini Guinea na kusambaa hadi Liberia, Sierra Leone na Nigeria, umesababisha vifo vya watu 1,060 na wengine kiasi 2,000 wameambukizwa virusi vya Ebola.
Ama kwa upande mwingine, Shirika la Madaktari wasio na Mipaka-MSF, limesema itachukua muda miezi sita kuweza kuudhibiti ugonjwa hatari wa Ebola ambao unahitaji msaada mkubwa na muongozo kutoka kwenye Shirika la Afya Duniani-WHO.
Rais wa shirika hilo, Joanne Liu amewaambia waandishi wa habari mjini Geneva kwamba iwapo hali nchini Liberia haitadhibitiwa, basi ugonjwa huo utashindwa kudhibitiwa kwenye ukanda wa Afrika Magharibi.
Akizungumza leo baada ya ziara yake ya siku 10 Afrika Magharibi, Bibi Liu amesema msaada mkubwa wa kimataifa unahitajika na kwamba wataalamu zaidi wa afya wanahitajika katika ukanda huo.
AFD yaonya kuhusu dawa zinazouzwa kwenye mitandao
Aidha, Shirika la Madawa na Chakula la Marekani-AFD, limeonya kuhusu bidhaa zinazouzwa kwenye mitandao kwa madai kwamba zinazuia au zinatibu Ebola.
Onyo hilo la FDA, limetolewa baada ya afisa mwandamizi wa afya wa Nigeria kuripotiwa akisema kuwa wagonjwa wa Ebola mjini Lagos watapatiwa dawa za majaribio zinazoitwa Nano-Silver. Hata hivyo, msemaji wa AFD, Erica Jefferson, hajafafanua zaidi kuhusu bidhaa anazozizungumzia.
Nao Umoja wa Mataifa umeahidi kutoa msaada wa chakula kwa mamilioni ya watu walioathiriwa na ugonjwa wa Ebola Afrika Magharibi.
Wakati huo huo, Rais wa Nigeria, Goodluck Jonathan amewafukuza kazi maelfu ya madaktari walioshiriki kwenye mgomo wa taifa wa wiki kadhaa, huku kukiwa na tahadhari kutoka WHO kwamba ugonjwa wa Ebola unaendelea kusambaa.
Kwa mujibu wa gazeti la Premium Times lililochapishwa leo, Waziri wa Afya wa Nigeria, Onyebuchi Chukwu, ameamuru barua za kufukuzwa kazi ziandikwe kwa madaktari wote waliogoma.
Wakati hayo yakijiri, Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki-IOC, imewazuia wachezaji wa timu zilizoathirika na Ebola kushiriki katika michezo ya olimpiki kwa vijana inayoanza kesho nchini China.
Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/RTRE,APE,DPAE, AFPE
Mhariri: Yusuf Saumu