Viwanda vya nyuklia vyapata uhai mpya
1 Septemba 2010Miaka ya hivi karibuni, viwanda vya nishati ya nyuklia barani Ulaya, vilipata uhai mpya kama nishati safi inayolinda mazingira. Nchi nyingi ama zinajenga au zinapanga kujenga mitambo mipya.Lakini Ujerumani,kama Uhispania, Austria na Ubeligiji iliamua kuachana na miradi ya kuzalisha nishati ya nyuklia. Sasa, Kansela wa Ujerumani Angela Merkel anaeongoza serikali ya muungano wa vyama ndugu vya kihafidhina CDU - CSU na cha kiliberali FDP angependa kurefusha muda wa viwanda hivyo kwa miaka 10 hadi 15.
Katika mkataba wa muungano, vyama hivyo vinasisitiza kuwa nishati ya nyuklia ni daraja la kuelekea enzi ya nishati mbadala. Wataalamu walikabidhiwa na serikali jukumu la kuchunguza vipi mazingira,bei ya nishati na usalama wa nishati utanufaika kwa kurefusha muda wa viwanda hivzo. Merkel angependa kurefusha muda huo kwa miaka 10 hadi 15, lakini anafahamu vyema kuwa kisiasa itakuwa vigumu sana kufanya hivyo. Akaongezea:
"Ningesema kuwa kiufundi miaka 10 hadi 15 inaingia maanani.Hata hivyo kama kiongozi wa serikali napaswa kuzingatia vipi usalama utapewa kipaumbele katika nishati ya nyuklia."
Vyama vyote vya upinzani, kuanzia cha Kijani, SPD na Die Linke vimeshasema kuwa ikihitajika, vitakwenda hadi Mahakama ya Katiba ili kuizuia serikali kurefusha muda wa viwanda hivyo. Vyama hivyo vina wasiwasi kuwa muda huo haurefushwi kwa kipindi maalum tu bali hiyo ni hatua ya mwanyo za kuendelea na nishati ya nyuklia.
Miaka kumi iliyopita, serikali ya wakati huo ya muungano wa vyama vya SPD na Kijani, chini ya uongozi wa Gerhard Schroeder ilikubaliana na kampuni za nishati kuzalisha kiwango maalum cha nishati na kiwanda cha mwisho kilitazamiwa kufungwa ifikapo mwaka 2025. Lakini kuambatana na mipango ya Merkel, sasa kuna uwezekano wa viwanda hivyo vya nyuklia kuendelea kufanya kazi hadi mwaka 2040.
Mwanasiasa wa SPD, Hubertus Heil anaamini kuwa serikali itakumbana na wakati mgumu ikiwa itarefusha muda wa viwanda hivyo. Amesema:
"Kuna mzozo mkubwa wa kijamii. Umma uliridhika na maafikiano yaliyofikiwa pamoja na sekta ya nishati.Sasa inajaribu kwenda kinyume na yale yaliyokubaliwa."
Anauliza,itakuje ikiwa serikali bungeni itakuwa na wingi tofauti baada ya miaka mitatu au minne ijayo. Vyama vya upinzani na wapinzani wa nishati ya nyuklia wameonya kuwa miezi ijayo itashuhudia maandamano mbali mbali. Kwa maoni ya kiongozi wa chama cha Kijani, Cem Özdemir,kurefushwa kwa muda wa viwanda hivyo, kutainufaisha sekta ya viwanda vya nishati ya nyuklia pekee.
Mwandishi:Gräßler,Bernd/ZPR
Mhariri:Othman,Miraji