1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Viwango vya uzazi kupungua sana duniani kufikia mwaka 2100

21 Machi 2024

Ripoti ya watafiti wa nchini Marekani inaonyesha kuwa viwango vya uzazi karibu katika mataifa yote ya ulimwengu vitashuka kufikia 2100, kiasia cha kutowezekan kurudisha idadi ya watu, huku mataifa maskini yakizaa zaidi.

Korea Kusini | Kiwango cha uzazi
Kiwango cha uzazi nchini Korea Kusini kinaripotiwa kushuka kwa kiasi kikubwa kufikia mtoto 1.1 kwa kila mwanamke.Picha: Yonhap/picture alliance

Mwelekeo huo utasababisha pengo kati ya "ongezeko kubwa la vizazi" na "upungufu mkubwa wa vizazi" kote duniani, ambapo ongezeko litajikita zaidi katika mataifa yenye kipato cha chini ambayo huyumbishwa zaidi kiuchumi na kisiasa, mtafiti mkuu Stein Emil Vollset kutoka Taasisi ya Metrics ya Afya na Tathmini (IHME) katika chuo kikuu cha Washington mjini Seattle, alisema katika taarifa.

Kufikia mwaka 2050, zaidi ya theluthi tatu ya mataifa duniani hayataweza kuzaa watoto wa kutosha kuweza kuendeleza idadi yao ya watu kwa muda mrefu, imesema ripoti hiyo. Kwa upande wa pili ongezeko la watu litachochewa na idadi kubwa ya vizazi katika mataifa maskini, hasa yalioko kanda za magharibi na mashariki mwa eneo la Afrika kusini mwa Sahara.

Je umri unakuzuia kupata ujauzito?

05:11

This browser does not support the video element.

Utafiti huo uliyoripotiwa katika Jarida la Kitabibu la Lancet unakadiria kwamba mataifa 155 kati ya 204 na maeneo kote duniani, au asilimia 76, yatakuwa na viwango vya uzazi vilivyo chini ya uwezo wa kurudisha idadi ya watu kufikia 2050. Kufikia mwaka 2100, watafiti wanakadiria kuwa idadi ya mataifa yenye viwango vya chini vya uzazi itafikia 189, au asilimia 97 ya mataifa yote ya ulimwengu.

Soma pia: Uganda: Ruksa wasichana wadogo kutumia uzazi wa mpango

Makadirio hayo yametokana na utafiti, sensa na vyanzo vingine vya data zilizokusanywa kuanzia mwaka 1950 hadi 2021, kama sehemu ya utafiti mpana kuhusu mzigo wa kimataifa wa magonjwa, majeruhi na masuala yanayosabisha hatari.

Utafiti unawiana na tathmini ya WHO

Professor Melinda Mills ni Mkurugenzo wa Kituo cha Sayansi ya Demografia cha Leverhulme katika chuo kikuu cha Oxford. Mills anasema gharama kubwa za maisha, gharama za kulea watoto, na wasiwasi kuhusiana na maendeleo ya kitaaluma unawazuwia wanawake katika mataifa mengi kupata watoto.

Mills, ambaye hakuhusika na utafiti wa Chuo Kikuu cha Washington anasema makadirio hayo yanaendana na tathmini za Shirika la Afya Ulimwenguni.

Mwanamke Safina Namukwaya wa nchini Uganda alipata watoto wake wa kwanza mapacha akiwa na umri wa miaka 70.Picha: Badru Katumba/AFP

"Tunaona katika mataifa kama vile Japan, ambako watu wengi wanapata mtoto wao wa kwanza kwa umri wa miaka 32, sawa na Italia. Hiyo inamaanisha kuwa watu wanazaa baadaye sana na wanazaa watoto wachache. Hii inaitwa mgomo wa watoto. Wanawake hawataki kutunza familia zao, wazazi wao, na wakati huo kufanya kazi. Na katika jamii zenye viwango vikubwa vya uzazi katika mataifa ya Afrika Kusini mwa Sahara, Indonesia, Pakistan, Bangladesh mjadala huko ni zaidi kuhusu wanawake na wanandoa kuweza kutambua nia zao za uzazi," anasema.

Soma pia:Japan yalenga kuimarisha viwango vya uzazi 

Watafiti wa mjini Washington wanasema viwango vya uzazi duniani kwa ujumla vimeshuka kutoka karibu watoto watano kwa kila mwanamke mwaka 1950, hadi watoto 2.2 kwa kila mwanamke mwaka 2021. Ripoti yao inasema kushuka huko kunaonekana hasa katika maeneo kama Korea Kusini na Serbia, ambako viwango vya uzazi ni chini ya mtoto 1.1 kwa kila mwanamke.

Katika mataifa ya Afrika Kusini mwa Sahara, kiwango ni watoto wanne kwa kila mwanamke mwaka 2021, mwaka ambao Chad ilikuwa kiwango cha juu zaidi cha watoto saba kwa kila mwanamke. Kulingana na Mills, baadhi ya mataifa yanaaza kuunda ufumbuzi wa kiteknolojia kwa watu wake wanaozeeka, na anasema inaleta mantiki kuhoji iwapo kupungua kwa watu ni jambo baya.

Chanzo: Mashirika