Vladmir Putin, Xi Jinping na mikakati yao ya kutawala maisha
21 Januari 2020Tangazo la ghafla la rais Putin wiki hii kuhusu mabadiliko ya kikatiba yanayoweza kumruhusu kurefusha udhibiti wake baada ya kumalizika kwa muhula wake mwaka 2024 linarudia hatua ya Xi mwaka 2018 alipoondoa ukomo wa muhula kwa mkuu wa nchi.
Hilo linaweza kuwapa miaka mingine mingi tu madarakani katika mawili kati ya madola makuu ya dunia yanayosuguana mara kwa mara na Marekani na mataifa mengine ya magharibi kuhusiana na masuala yanayoanzia kwenye ujasusi wa kiuchumi na sera ya kigeni hadi demokrasia na haki za binadamu.
Hatua za viongozi hao wote zinaakisi haiba zao za kimabavu na dhamira ya kurejesha fahari ya zamani ya mataifa yao baada ya miaka kadhaa ya kile wanachokiona kama udhalilishaji wa mataifa ya magharibi.
Wanaingiana pia na mwelekeo wa viongozi wa kiimla wanaochukuwa madaraka kuanzia Hungary na Brazil hadi Ufilipino. Urusi na China ziko kwenye ngazi nyingine ingawa, linapokuja suala la kushawishi matukio ya kimataiga.
China kupitia nguvu yake ya kiuchumi na inayoinukia kijeshi, Urusi kupitia utayari wake kujiingiza katika mizozo kama vile nchini Syria, na kujaribu kashawishi uchaguzi wa mataifa ya kigeni kupitia taarifa ya upotoshaji au kufanya uhalifu kupitia mashambulio ya kimtandao.
Wakati wa kusalia madarakani
Putin anaamini Urusi ina nguvu zaidi hii leo kuliko ilivyowahi kuwa tangu kumalizika kwa vita baridi, ikiwemo katika mataifa kama vile Mashariki ya Kati, anasema Ramon Pacheco Pardo, kutoka kitivo cha utafiti kuhusu Ulaya na kimataifa katika chuo King's collaege cha mjini London.
"Na hivyo ni wakati mzuri kusalia madarakani na kutumia nguvu hii," anafafanua mwanataaluma huyo akielezea fikra za Putin.
Ni kwa kiasi gani Putin na Xi wanatoa changamoto kwa ruwaza za magharibi, maadili na demokrasia ya vyama vingi, hii inategemea na upande gani umesimama. Ruwaza wa China na Urusi inahamasisha baadhi miongoni mwa mataifa madogo na makubwa.
Rais Donald Trump amewasifu Xi na Putin, licha ya kwamba Marekani inapambana na mataifa yao kwa ajili ya udhibiti wa kiuchumi na kimkakati.
China inausifu mfumo wake wa kiimla kwamba unahakikisha kuwapo na utulivu na maendeleo ya kisera ulioifanya kuwa uchumi wa pili kwa ukubwa duniani na kuwaondoa watu wapatao milioni 700 kutoka kwenye umaskini uliokithiri.
Warusi wengi wamemuunga mkono rais Putin kwa kusimama kidete dhidi ya mataifa ya magharibi na kuboresha maisha yao kufuatia sokomoko la kupomoroka kwa Jamhuri ya Kisovieti.
'Hakuna haja ya kuwa na hofu'
Lakini balozi wa Umoja wa Ulaya nchini China, Nicolas Chapui, anasema ushindani wa kisiasa kati ya mifumo tofauti ya utawala duniani siyo jambo geni, na kuongeza kuwa Ulaya inapaswa kuwa na imani na kanuni zake, maadili na mfumo wa utawala.
Katika hali zao zote, Putin na Xi wanaakisi tabia ya viongozi wa kiimla kung'ang'ania madarakani kwa kadiri iwezekanavyo na hata kufia ofisini, anasema David Zweig, profesa wa sayasi ya jamii katika chuo kikuu cha Hong Kong cha Sayansi na Teknolojia.
Licha ya mlandano, Xi, Putin na mifumo wanayoiendesha inatofautiana kwa mambo mengi. Xi emetaja kuanguka kwa Jamhuri ya Kisovieti kama simulizi ya tahadhari, akismea viongozi wake walishindwa kutetea kwa nguvu mamlaka ya chama tawala cha Kikomunisti.
Nchini China chama cha Kikomunisti kimesambaratisha upinzani wote na wanakaza uthibiti wao wa uchumi na kinachosalia katika asasi za kiraia, yote hayo wakati wakitoa taswira ya nje ya mshikamamo wa dhati kwa Xi.
Urusi alau inaendeleza baadhi ya mifumo kama siyo majukumu ya demokrasia ya vyama vingi, licha ya Putin, idara za usalama na matajiri wanaoendesha uchumi kuwa ndiyo wenye maamuzi.
Putin ameyataja mapedekezo yake ya mageuzi kama njia ya kuimarisha bunge na kukuza demokrasia. Wakosoaji hata hivyo wanasema ni jaribio la Putin kujipatia utawala wa maisha.
Chanzo: AP